“SERIKALI imesema kuwa vijana wengi wanakosa ajira kwa sababu ya uraibu wa dawa za kulevya. Waziri wa Leba, Dkt Alfred Mutua, aliwataka wanaotafuta ajira kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya, akisema vijana wengi wanapoteza fursa wakati uchunguzi wa afya unapobainisha matumizi ya dawa hizo. “Vijana mjiepushe na kutafuna muguka na kuvuta bangi. Hutapata kazi ikiwa wewe ni mraibu,” alisema Dkt Mutua alipokuwa akizungumza na mamia ya vijana waliojitokeza katika zoezi la pamoja la kuajiri watu kwa kazi za nje ya nchi katika Mamlaka ya Kitaifa ya Mafunzo ya Viwandani (NITA) mjini Mombasa. Zoezi hilo lililenga kuwatafutia watu 4,000 ajira za nje kupitia mashirika ya uajiri yaliyoidhinishwa na serikali. Waziri huyo alieleza kuwa, nchi zinazoajiri wafanyakazi kutoka Kenya huweka masharti makali ya vipimo vya afya na dawa za kulevya, ambapo yeyote anayepatikana na dawa hizo hukataliwa moja kwa moja. Kulingana na Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya (Nacada), kijana mmoja kati ya kila 11 wenye umri wa miaka 15 hadi 24 hutumia angalau aina moja ya dawa za kulevya. Uraibu mkubwa zaidi ni wa pombe, miraa, bangi, tumbaku na matumizi ya mchanganyiko wa dawa mbalimbali. Dkt Mutua alisema ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana linadhoofisha juhudi za serikali za kuunda nafasi za ajira kupitia mikataba ya ajira kati ya nchi. Wakati huo huo, aliwaonya wanaotafuta kazi dhidi ya kulaghaiwa na mashirika bandia ya uajiri, akisisitiza kuwa ni muhimu kushirikiana tu na kampuni zilizosajiliwa rasmi. “Tuna kampuni 26 zilizosajiliwa katika zoezi hili la Mombasa. Hizi ndizo halali pekee. Kampuni bandia tumezifuta usajili,” alisema Mutua. Alisisitiza kuwa waombaji kazi wanaolipa mashirika yasiyo halali kwa hiari yao wako hatarini kupoteza fedha zao na hawapaswi kuilaumu serikali. Aidha, aliagiza kuwa mashirika ya uajiri yawarejeshee fedha waombaji ajira watakaofeli vipimo vya afya, yakikatakata tu gharama za uchunguzi wa kimatibabu. “Ikiwa shirika linachukua ada na unafeli kipimo cha afya, labda kwa sababu ya HIV au hali nyingine ya kiafya, wanapaswa kukurejeshea fedha zako, wakikata tu gharama za uchunguzi,” alisema. Baadhi ya kazi zilizokuwa zikitolewa ni za walinzi, wauguzi, madereva, upishi na wahudumu wa huduma mbalimbali. Wakati huo huo, Waziri huyo alilaani vurugu za kijamii na wizi wa mifugo, akizitaja kama vitendo vya “kizamani, vya kipumbavu na vya kikatili” visivyofaa katika Kenya ya kisasa. Mapigano ya hivi karibuni katika mpaka wa Kaunti za Kitui na Garissa yalisababisha vifo vya watu wasiopungua 15, kuwahamisha wakazi, kuharibu mali na kuvuruga shughuli katika Barabara ya Mwingi–Garissa. Alitaja maeneo yanayokumbwa mara kwa mara na matatizo hayo kuwa ni pamoja na Baringo, Samburu, Pokot, Kitui, Garissa na Marsabit, huku pia akiwakosoa viongozi wanaochochea vurugu hizo kwa maslahi ya kisiasa au binafsi. Waziri huyo aliwataka Wakenya kukataa uchochezi na kuzingatia maendeleo, akisema Kenya imeingia katika enzi mpya ya teknolojia ambapo vijana hawako tayari tena kutumika kuzua vurugu na kusababisha vifo vya wengine wasio na hatia.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
