skipToContent
🌐All

Bunifu za kilimo zilivyotuza vijana hawa

Bunifu za kilimo zilivyotuza vijana hawa
WAKATI vijana wengi wakikimbilia ajira za mijini, kundi la wabunifu wa teknolojia ya kilimo nchini sasa linaonyesha kuwa sekta ya kilimo inaweza kuwa chanzo kikubwa cha mapato, ajira na suluhu kwa changamoto zinazokabili wakulima wa mashamba madogo. Kutoka usindikaji wa maparachichi yaliyokataliwa sokoni, utengenezaji wa chakula cha mifugo, hadi matumizi ya akili mnemba (AI) na vifaa vya kidijitali kupima ubora wa maziwa, vijana hawa wanageuza mawazo yao kuwa biashara zinazobadili maisha ya wakulima. Ubunifu huo ulijitokeza wazi wakati wa mashindano ya Agriculture, Youth and Technology (AYuTe) Challenge Kenya 2025/26 yaliyoandaliwa na Heifer International kwa ushirikiano na Kenya Climate Innovation Centre (KCIC), jijini Nairobi. Mashindano hayo yanalenga vijana wabunifu wanaotumia teknolojia kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya kilimo. Patrick Mutahi, mwanzilishi mwenza wa Mukurweini Oil Enterprises kutoka Nyeri, aliibuka mshindi mkuu katika kitengo cha kampuni zinazokua (Growth Stage), na kujishindia granti ya Sh1.5 milioni. Kampuni yake huzalisha mafuta kutokana na maparachichi – avocado, yasiyokidhi viwango vya soko la kuuza nje, hatua inayosaidia kupunguza upotevu wa mazao huku ikiongeza thamani kwa wakulima. Mutahi kwenye mahojiano ya kipekee na Akilimali alisema wazo hilo lilizaliwa baada ya kushuhudia wakulima wakipata hasara kubwa kutokana na matunda mengi kuharibika kwa kukosa soko. “Niliona wakulima wakihangaika licha ya kufanya kazi kubwa mashambani. Maparachichi mengi yalikuwa yanatupwa kwa sababu hayakuafikia viwango vya soko la nje ya Kenya,” alisema. Alisema hali hiyo ilimfanya kurejea nyumbani na kuanzisha biashara inayolenga kuboresha kipato cha wakulima wa mashamba madogo. Kwa sasa, kampuni hiyo hukusanya maparachichi yaliyokataliwa sokoni na kuyageuza mafuta yanayotumika kama vipodozi na kwa minajili ya afya. Mutahi alisema biashara hiyo imekua kwa kasi ndani ya miaka miwili iliyopita, kutoka uzalishaji mdogo hadi uwezo wa kuchakata kilo 50 za maparachichi kwa kila mzunguko wa uzalishaji. Aidha, alisema kwa sasa wanafanya kazi na wakulima 150 wa Nyeri, lakini lengo ni kufikia zaidi ya wakulima 1,000 katika miaka ijayo. [caption id="attachment_187817" align="aligncenter" width="300"] Mashindano ya AYuTe yanayoandaliwa na kufadhiliwa na Heifer International yanalenga kutambua vijana wenye vumbuzi na bunifu za kiteknolojia na kidijitali kuangazia changamoto kwenye sekta ya kilimo. Picha|Sammy Waweru [/caption] Katika nafasi ya pili ya kitengo cha Growth Stage ilikuwa Bellfeeds Farmcare, iliyojishindia Sh1.3 milioni. Kampuni hiyo hutengeneza chakula cha nguruwe na kutoa huduma za ushauri kwa wafugaji. Mwanzilishi mwenza wa kampuni hiyo, Brean Ogechi, alisema biashara yao ilianzishwa wakati wa janga la Covid-19 na sasa imekua hadi kuwa kampuni yenye mamilioni ya fedha na wafanyakazi 24, wengi wao wakiwa vijana na wanawake. “Sasa tunasambaza bidhaa zetu katika maeneo ya Mlima Kenya, Rift Valley, Magharibi, Nyanza na Pwani. Isitoshe, tunanunua nguruwe kutoka kwa wakulima na kuuza nyama kwa hoteli, maduka makubwa na mabucha,” alisema. Jolly Mushroom Enterprises ilishika nafasi ya tatu katika kitengo hicho, Growth Stage, na kujishindia Sh500,387 huku Zuphifarm ikipata Sh250,193. Katika kitengo cha kampuni changa (Early Stage), Dairy Sense iliibuka mshindi kwa kujishindia Sh800,000. Mwanzilishi wake, Daniel Litunya, alisema wamebuni vifaa vya kupima ubora wa maziwa moja kwa moja shambani ili kusaidia wafugaji kupata bei inayolingana na ubora wa maziwa yao. “Kwa muda mrefu wafugaji wamekuwa wakilipwa kulingana na kiwango cha maziwa pekee. Tunataka ubora pia uzingatiwe,” alisema. DroFarmer Ltd ilishika nafasi ya pili na kutuzwa Sh400,310. Kampuni hiyo hutumia huduma za kidijitali kusaidia wakulima katika maeneo kame (ASAL) kukuza mazao yanayostahimili ukame kama vile mtama na ndengu. Mwanzilishi wake, Ken Mbuki kutoka Kitui, alisema wameanza kusaidia wakulima wa Kitui na sasa wanapanua huduma hadi kaunti nyingine kama Kajiado. Soil Doctors Limited ilimaliza ya tatu kwa Sh300,232. Mwanzilishi wake, Charles Mwangi, alisema kampuni hiyo imebuni mashine za kupanda mbegu zinazosaidia wakulima katika maeneo kame na nusu-kame kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Alisema sasa wanaongeza matumizi ya teknolojia ya AI kusaidia wakulima kufanya maamuzi bora kuhusu kilimo. Chrisfa Poultry ilishika nafasi ya nne na kujishindia Sh250,193. Washindi wote walisema fedha walizopata zitasaidia kuongeza uzalishaji, kupanua huduma kwa wakulima na kuboresha upatikanaji wa masoko. [caption id="attachment_187818" align="aligncenter" width="300"] Mkurugenzi wa Heifer International Kenya, Wairimu Munyinyi-Wahome kwenye mahojiano jijini Nairobi baada ya kutoa tuzo za AYuTe 2025/26. Picha|Sammy Waweru [/caption] Mkurugenzi wa Heifer International Kenya, Wairimu Munyinyi-Wahome, alisema mpango wa AYuTe unalenga kusaidia vijana kubadilisha mawazo yao kuwa biashara endelevu zinazoweza kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo. “Tunashuhudia vijana wakitoa suluhu za kweli kwa changamoto kama vile upotevu wa mazao baada ya mavuno, mabadiliko ya tabianchi na matumizi ya teknolojia katika kilimo,” alisema. Naye Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Climate Innovation Centre (KCIC), Joseph Murabula, alisema mashindano hayo yalipokea maombi 486, lakini ni washiriki 18 pekee waliofika hatua ya mwisho. Kwa upande wake, Katibu katika Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Idara ya Mimea, Dkt Kipronoh Ronoh, alisema vijana wengi nchini wana mawazo yenye uwezo wa kubadilisha sekta ya kilimo. Alisema kinachohitajika ni mazingira bora, uwekezaji na majukwaa yatakayowawezesha kugeuza ubunifu wao kuwa biashara zinazowanufaisha wakulima na kuchangia uchumi wa taifa.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.