“WAKENYA wanaotafuta njia mbadala za kukuza fedha zao mbali na akaunti za kawaida za benki sasa watapata fursa mpya kupitia mifuko ya uwekezaji iliyosajiliwa rasmi na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji nchini (CMA). Mfuko huo mpya una jumla ya vitengo sita vya uwekezaji ambavyo ni Pergamon Money Market Fund (KES), Pergamon Money Market Fund (USD), Pergamon Equity Fund, Pergamon Fixed Income Fund, Pergamon Balanced Fund na Pergamon Special Diversified Income Fund. Mifuko hiyo imeundwa kuwafaa wawekezaji wa viwango tofauti kulingana na uwezo wao wa kuvumilia hatari za uwekezaji. Usajili huo umefanyika wakati ambapo Kenya inaendelea kutafuta njia za kuimarisha masoko ya mitaji kupitia bidhaa mbalimbali za kifedha zinazodhibitiwa. Akizungumza baada ya kuidhinishwa kwa mfuko huo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Pergamon Investment Bank, Bi Wanjiru Gichuru, alisema hatua hiyo ni mafanikio makubwa kwa taasisi hiyo. “Usajili wa mfuko wetu wa uwekezaji umetuweka karibu zaidi na maono yetu ya kutoa suluhu bunifu za uwekezaji kwa wateja wetu huku tukichangia kukuza masoko ya mitaji nchini,” alisema Bi Gichuru. Aliongeza kuwa Wakenya wengi sasa wanatafuta njia mbadala za kukuza fedha zao mbali na kuweka akiba kwenye benki za kawaida. Sekta ya mifuko ya pamoja ya uwekezaji nchini imeendelea kukua kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni huku Wakenya wengi wakivutiwa na uwekezaji unaosimamiwa kitaalamu. Takwimu zinaonyesha kuwa kufikia Septemba 2025, fedha zilizokuwa zikisimamiwa katika sekta ya unit trust zilifikia takriban Sh679.6 bilioni kutoka Sh596.3 bilioni katikati ya mwaka huo. Kwa sasa, Kenya ina zaidi ya mifuko 55 ya unit trust yenye zaidi ya vitega uchumi 230, huku watu kati ya milioni mbili hadi tatu wakishiriki katika uwekezaji huo kupitia viwango vya chini vya kuanzia na usajili wa mtandaoni.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
