“WAKATI mjadala kuhusu bidhaa zilizoboreshwa kijenetiki (GMO) ukiendelea kushika kasi nchini Kenya, Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Kibayolojia (NBA) inaendelea kuandikisha ukuzaji wa mimea iliyoboreshwa – shabaha ikiwa ni kusaidia wakulima kupunguza gharama ya uzalishaji. Kando na pamba iliyoboreshwa, ndiyo bt cotton, mimea mingine kama mahindi na mihogo, ipo kwenye laini ya kufikia wakulima japo kesi zilizowasilishwa kortini kuzuia usambazaji wa bidhaa za GMO umelemaza hatua hiyo. Jukumu la NBA si kuhamasisha wala kupinga matumizi ya teknolojia za kisasa kuimarisha kilimo, bali ni kuhakikisha bidhaa zote ni salama kwa binadamu, mifugo na mazingira. Mkurugenzi Mkuu wa NBA, Dkt Ann Karimi, anasema mamlaka hiyo ndiyo yenye wajibu kusimamia masuala yote yanayohusiana na GMO nchini, kuanzia utafiti, uagizaji na usafirishaji hadi biashara na matumizi yake. Anasema bidhaa yoyote ya GMO inayokusudiwa kwa matumizi ya binadamu, chakula cha mifugo au shughuli za kibiashara lazima ipitie tathmini ya kina ya kisayansi kabla ya kuidhinishwa. [caption id="attachment_189203" align="aligncenter" width="300"] Afisa Mkuu Mtendaji Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Kibayolojia (NBA). Picha|Sammy Waweru [/caption] Maombi yote ya kuingiza au kusafirisha bidhaa hizo hupokelewa na kuchunguzwa kwa makini ili kubaini iwapo yanakidhi viwango vya usalama vilivyowekwa. “Tunafanya kazi ya udhibiti na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi zinazotegemea ushahidi wa kisayansi. Hatulazimishi mtu kutumia GMO wala hatupingi matumizi yake,” anasema Dkt Karimi. Kazi za mamlaka hiyo zinaongozwa na Sheria ya Usalama wa Kibayolojia ya mwaka 2009, ambayo ilianzishwa kuweka mfumo wa kisayansi wa kuidhinisha maendeleo, majaribio, uagizaji na biashara ya GMO nchini. Kulingana na Dkt Karimi, bidhaa za GMO hupitia hatua kadhaa za tathmini kabla ya kupewa kibali. Taasisi za utafiti ikiwemo, Shirika la Utafiti wa Masuala ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo (Kalro), huwasilisha maombi ambayo huchunguzwa na wataalamu kutoka sekta mbalimbali ili kuhakikisha hakuna hatari kwa afya ya binadamu au mazingira. “Baadhi ya teknolojia hizo tayari zimepata kibali cha kutumika nchini. Pamba aina ya Bt, kwa mfano, iliidhinishwa kwa matumizi ya kibiashara mwaka 2019 na kwa sasa inalimwa katika kaunti mbalimbali,” Karimi anaelezea. Mahindi ya Bt yamefikia hatua za mwisho za tathmini huku mihogo ya GMO ikiwa imepitia majaribio ya mashambani na bado inafanyiwa uchunguzi zaidi kabla ya kupewa idhini ya mwisho. [caption id="attachment_189204" align="aligncenter" width="300"] Mfanyakazi wa Kalro, Kandara, Murang'a akivuna muhogo ulioboreshwa vinasaba na jenetiki. Picha|Sammy Waweru [/caption] Mbali na GMO, Kenya pia inaendelea kufanya utafiti kuhusu teknolojia mpya kama vile uhariri wa jeni ( gene editing ), ambapo watafiti wanaendeleza aina mpya za mtama. Teknolojia nyingine kama gene drive na synthetic biology bado hazijaanzishwa nchini. Dkt Karimi kwenye mahojiano ya kipekee na ‘Akilimali’, alisema anaamini kuwa GMO zinaweza kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za usalama wa chakula, hasa wakati ambapo mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuathiri uzalishaji wa mazao. “Baadhi ya mazao hayo yana uwezo wa kustahimili ukame au magonjwa, hivyo kusaidia kuongeza mavuno.” Kenya hutumia mabilioni ya pesa kuagiza chakula kutoka nje ya nchi kila mwaka, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuwekeza katika teknolojia mbalimbali za kuongeza uzalishaji wa ndani kwa ndani. Hata hivyo, Karimi anasisitiza kuwa GMO ni mojawapo tu ya suluhisho, sawa na umwagiliaji mimea na mashamba maji kwa mifereji, matumizi ya mbegu bora na uboreshaji wa huduma za shambani. [caption id="attachment_189205" align="aligncenter" width="300"] Muhogo ulioboreshwa vinasaba na jenetiki. Picha|Sammy Waweru [/caption] Licha ya hatua zilizopigwa, NBA bado inakabiliwa na changamoto kadhaa. “Kesi mbalimbali zilizowasilishwa mahakamani kuhusu matumizi ya GMO zimechelewesha uidhinishaji wa baadhi ya bidhaa, ikiwemo mihogo ya GMO,” Dkt Karimi anasema. Aidha, upotoshaji wa habari kuhusu teknolojia hiyo umeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi kuelewa. Ili kuimarisha usalama na kujenga imani ya umma, NBA imeongeza ukaguzi katika maeneo ya mipakani kama vile Busia na Malaba na kuimarisha ushirikiano na taasisi za utafiti kama KALRO. Hali kadhalika, mamlaka hiyo inaendesha kampeni za uhamasishaji kupitia mikutano ya umma, vyombo vya habari na mipango ya elimu ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu GMO na jinsi zinavyodhibitiwa nchini.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
