“MUDA wa kutoa maoni kuhusu Mswada wa Fedha wa 2026 ulipokaribia kuisha Jumatatu jioni, vijana wengi wa Kenya hawakuwa katika mikutano ya hadhara, ofisi za serikali wala mikusanyiko ya kisiasa. Badala yake, wengi walikuwa wamejikita kwenye simu zao. Tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, maelfu ya vijana wamekuwa wakijipanga mtandaoni kupitia TikTok, X, WhatsApp, Instagram na Telegram wakisoma Mswada huo, kuchambua vipengele vya ushuru, kusambaza viunzi vya ushiriki wa umma na kutuma maoni yao kupitia tovuti ya Bunge. Tofauti na ushiriki wa jadi wa kiraia uliokuwa ukihusishwa na mikutano ya hadhara na maandamano, mwaka huu karibu kila kitu kilifanyika mtandaoni kwa kuongozwa na vijana wa kizazi cha Gen Z waliojihami kwa simu za kisasa, ALAMA ZA RELI na elimu ya uraia. Katika majukwaa hayo, watumiaji wamekuwa wakisambaza muhtasari rahisi wa Mswada huo, wakitafsiri lugha ngumu ya kisheria kwa lugha ya kawaida na kueleza jinsi ushuru uliopendekezwa unaweza kuwaathiri wananchi wa kawaida. Kilichoanza kama mazungumzo ya kawaida kuhusu ushuru sasa kimegeuka kuwa mojawapo ya harakati kubwa zaidi za vijana mtandaoni tangu maandamano ya Mswada wa Fedha wa 2024 yaliyozua maandamano makubwa nchini. Miongoni mwa waliokuwa wakihamasisha wananchi ni Allans Ademba, mwanzilishi wa mpango wa “TUKO KADI”, ambaye Jumatatu alichapisha kiunzi cha ushiriki wa umma akiwahimiza Wakenya kutoa maoni yao kuhusu mapendekezo yaliyomo kwenye Mswada huo. Miongoni mwa mapendekezo yanayopingwa zaidi ni ushuru wa asilimia 25 kwa simu za mkononi, ambao vijana wengi wanaamini utaongeza bei ya simu, ukarabati na vifaa vya kidijitali. Wengine wamepinga ushuru wa asilimia tano kwa mapato ya watayarishaji wa maudhui ya kidijitali wakisema tayari wanakabiliwa na mapato yasiyo ya uhakika na gharama kubwa za kuyaandaa. Ushuru wa asilimia 20 kwa ushindi wa kamari pia umeibua malalamiko. Vijana wengi pia wameonyesha wasiwasi kuhusu mapendekezo yanayotaka kampuni zinazoshughulikia mali za kidijitali kutoa taarifa za watumiaji kwa Mamlaka ya Ushuru Kenya (KRA), hatua inayozua hofu kuhusu faragha ya kifedha. Kwa Ellen Kalia, mwenye umri wa miaka 25 na mwanaharakati wa elimu ya uraia kutoka Pwani, jambo la kipekee katika harakati hizi ni kwamba hazina kiongozi mkuu. “Hakuna kiongozi nyuma ya hamasisho hii. Hii ni elimu ya uraia kwa sababu sisi sote ni walipa ushuru na tunaathirika,” alisema. Kalia alisema harakati hizi zilianza wakati wa maandamano ya Mswada wa Fedha wa 2024 ambayo yaliwaamsha kisiasa vijana wengi waliokuwa wamechoshwa na ukosefu wa ajira na gharama ya juu ya maisha. Mitandao ya kijamii sasa imekuwa jukwaa muhimu la mijadala ya uwajibikaji na sera za kitaifa. TikTok imejaa video fupi zinazofafanua vipengele vya ushuru huku wengine wakitumia vichekesho kueleza jinsi gharama ya maisha itakavyoathirika. Kutokana na ukosefu wa ajira, vijana wengi wamekimbilia uchumi wa kidijitali kupitia utengenezaji wa maudhui, biashara ya mtandaoni, sarafu za kidijitali na matangazo ya mitandaoni. Kwa wengi, intaneti sasa si ya burudani pekee bali ni njia ya kujikimu kiuchumi. Waziri wa Fedha John Mbadi, ametetea Mswada huo, akisema ushuru wa asilimia 25 kwa simu za mkononi hauleti ushuru mpya bali unalenga kurahisisha mfumo uliopo wa ushuru mwingi. Alisema simu kwa sasa hutozwa ushuru mbalimbali wakati wa kuagizwa na kusambazwa, hali inayosababisha mzigo mkubwa wa kodi wa karibu asilimia 55.5. “Tunabadilisha mfumo huo mgumu kwa mfumo rahisi ambapo ushuru mmoja wa asilimia 25 utatozwa simu inapowashwa,” alisema Bw Mbadi. Aidha, alitetea hatua ya kudhibiti mali za kidijitali akisema sekta hiyo imekua haraka na lazima iingizwe katika mfumo wa ushuru kama biashara nyingine. Hata hivyo, licha ya ushiriki mkubwa wa vijana mtandaoni, wengi bado wana mashaka iwapo maoni yao yatazingatiwa katika maamuzi ya mwisho ya serikali.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
