“KIFO cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga mwaka jana kimeitumbukiza familia yake katika mojawapo ya migogoro mikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika chama chake cha ODM. Chama hicho ambacho kwa muda mrefu kilidhibitiwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa wa Bw Odinga, sasa kinakabiliwa na migogoro ya uongozi, ushindani wa makundi huku umaarufu wake ukiendelea kudidimia. Kiini cha mzozo huo ni mvutano kati ya makundi mawili; moja likiunga mkono uongozi wa sasa wa chama hicho chini ya Oburu Oginga, mwenyekiti wa kitaifa Gladys Wanga, na manaibu viongozi wa chama Simba Arati na Abdulswamad Nassir. Kundi jingine linalohusishwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Gavana wa Siaya James Orengo, na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino nalo linapinga mrengo wa Dkt Oburu. Migawanyiko hiyo imeendelea kujitokeza hadharani, jambo linalozua wasiwasi miongoni mwa wafuasi wa ODM kuhusu umoja wa chama na umaarufu wake. Waziri wa Hazina ya Kitaifa, John Mbadi, amezua chache zaidi baada ya kuwalaumu baadhi ya viongozi kwa kutumia pengo lililoachwa na kifo cha Raila kusukuma mbele maslahi yao ya kisiasa. Akizungumza wakati wa kongamano la viongozi wa ODM jijini Mombasa wiki jana, Bw Mbadi aliwashutumu baadhi ya wanachama kwa kupanga njama za kudhoofisha chama na kufuta mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Raila. “Tunapaswa kuwa waaminifu kuhusu nani amejitolea kwa chama hiki. ODM si mali ya jamii moja, wala si mali ya familia moja,” akasema Bw Mbadi. Katika matamshi yaliyoonekana kulenga baadhi ya wanafamilia wa Odinga, Bw Mbadi alisema kuna watu wanaohisi wana haki ya kuamrisha wengine kwa sababu tu wanahusishwa na kiongozi mwanzilishi wa chama. “Tuna chama ambapo mtu, kwa sababu yeye ni dada wa kiongozi wa chama, anafikiri anaweza kutuamrisha. Haiwezekani. Baba alikuwa kiongozi imara sana,” akaongeza. Pia aliwataka wanachama waache kutumia jina la Raila kuhalalisha misimamo yao ya kisiasa. “Huwezi kuendelea kusema Baba alisema hivi au Baba hakusema vile. Yuko wapi huyo Baba kuthibitisha mambo mnayosema? Hayupo tena,” akasema Bw Mbadi. Mwakilishi wa Kike wa Kisumu, Ruth Odinga, ambaye ni dada yake Raila, naye amemshutumu Bw Mbadi kwa kulenga visivyo familia ya marehemu Raila. Bi Odinga akimjibu Bw Mbadi, alisema haungi mkono kundi a Linda Ground na Linda Mwananchi na umakinifu wake ni kwa ODM kuungana. “Ninasimama na ODM iliyoungana, ambayo ndiyo ilikuwa ndoto ya Raila Odinga,” akaandika kwenye mtandao wake wa kijamii. Bi Ruth pia alitetea uongozi wa nduguye Dkt Oginga akishutumu baadhi ya wanasiasa kwa kutumia ukarimu wake na imani kujinufaisha kibinafsi. Pia alitetea jina la familia ya Odinga ambayo imetawala siasa za Luo Nyanza tangu uhuru, akisema hawalitumii kutwaa vyeo vya kisiasa. Mwakilishi huyo alimpuuza Bw Mbadi na kuwataka Wakenya wasizingatia kauli yake. “Kama mzawa wa familia ya Odinga ninaamini kile ambacho Jaramogi na Raila walisimamia, siwezi kuruhusu madai hayo ya Mbadi yapite bila kujibiwa. “Ni wazi kuna wanasiasa ndani ya ODM ambao wanaamini kuwa tumekuwa tukikwamilia jina la Odinga ili kuhimili mawimbi ya kisiasa,” akasema Bi Ruth. Aliongeza kuwa wakati wa kampeni atajitafutia kura kutokana na rekodi yake ya maendeleo na akisaka uungwaji mkono kutoka kwa marafiki wa Raila, anafahamu mahali pa kuwapata.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
