“VIFO vya wanafunzi 16 kufuatia moto ulioteketeza bweni la shule ya wasichana ya Utumishi Girls Academy jana alfajiri, vimeibua upya wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya usalama shuleni na utekelezaji wa hatua zinazokusudiwa kuzuia maafa. Licha ya miongo kadhaa ya mageuzi, marekebisho ya sera na mapendekezo ya kuzuia matukio ya aina hii, utekelezaji wa tahadhari za usalama bado umeendelea kuwa hafifu. Ingawa chanzo cha moto huo katika shule hiyo iliyoko Gilgil bado kinachunguzwa, tukio hilo limefufua kumbukumbu za maafa ya awali katika shule mbalimbali nchini, yaliyodhihirisha mapengo makubwa katika hatua za kudumisha usalama na kutekeleza mifumo ya kukabiliana na majanga ya dharura. Taarifa za awali zinaashiria kuwa maafa kutokana na moto uliozuka shule ya Utumishi Girls iliyoko mjini Gilgil, Kaunti ya Nakuru, huenda yalizidishwa na tukio la milango ya bweni kufungwa kutoka nje na madirisha kuwa madogo pasina kuruhusu mwanya wa kutosha ili kutokea wakati wa dharura. Hali hii inajiri licha ya miongozo ya usalama kueleza wazi kuwa milango yote ya mabweni inapaswa kuwa na upana wa takriban futi tano, ifunguke kuelekea nje na isifungwe kutoka nje wanafunzi wakiwa ndani. Chama cha Walimu wa Shule za Sekondari na Vyuo (KUPPET) kinataka mamlaka husika ziwajibikie mkasa huo ambao umeacha majeruhi 79. “Mamlaka ya elimu ya kaunti, maafisa wa kudumisha ubora wa elimu, Idara ya Afya ya Umma, bodi na uongozi wa shule pamoja na polisi wanaosimamia usalama katika eneo ambako shule ipo wana maswali magumu ya kujibu,” alisema Katibu Mkuu wa KUPPET, Akelo Misori, katika taarifa yake. Kisa hiki kinajiri muda mfupi baada ya moto uliozuka katika shule ya Hillside Academy Endarasha, Kaunti ya Nyeri, mnamo Septemba 2024 ulioua wanafunzi 21. Hicho kilifuatia kisa kingine cha moto katika shule ya wasichana ya Moi mjini Nairobi mwaka 2017, kilichosababisha vifo 10. Mikasa mingine ya mioto shuleni yaliyoacha makovu katika sekta ya elimu nchini ni pamoja na mauaji na ubakaji dhidi ya wanafunzi wasichana katika shule ya sekondari ya St Kizito, Meru, yaliyoua wanafunzi 19. Miaka saba baadaye hitilafu ya umeme katika shule ya wasichana ya Bombolulu iliyoko Kaunti ya Kwale ilisababisha vifo vya watu 26. Mwaka 2001 Kenya ilishuhudia mkasa mkubwa zaidi wa moto shuleni wakati wanafunzi 67 walipoteza maisha katika sekondari ya Kyanguli, Machakos, baada ya wanafunzi wawili kuchoma bweni moja. Kwa miaka mingi serikali imeunda tume, kamati na majopo mbalimbali kuchunguza mioto na migogoro shuleni na kupendekeza hatua za kuboresha usalama wa wanafunzi. Miongoni mwazo ni Tume ya Kirima ya mwaka 1994, Jopo Kazi la Wangai mwaka 2001 na Kamati ya Koech ya mwaka 2008. Kufuatia wimbi la migomo ya wanafunzi na mioto katika mabweni mwaka 2016, Waziri wa Elimu wakati huo Fred Matiang’i, aliteua Jopo Maalum la Uchunguzi kudadavua matukio hayo, kupitia mapendekezo ya awali na kutathmini ufanisi wa kanuni zilizopo za usalama shuleni. Ritpoti ya jopo hilo ilitolewa mwaka 2017 na ilibaini kuwa shule nyingi bado hazina mikakati tayari ya kukabiliana na dharura za moto. Ilibainika kuwa ni taasisi chache tu zilizokuwa na vifaa vya kuzima moto vya kutosha, huku zingine zikiwa na vizima-moto visivyo na hewa au vilivyowekwa sehemu zisizofikika kwa urahisi wakati wa dharura. Wachunguzi pia waligundua kuwa shule nyingi hazikuwa na maeneo maalum ya pahali pa kukusanyika wakati wa dharura. Pia hakukuwa na ushahidi wa mazoezi ya kukabiliana na mioto kwa wanafunzi na wafanyakazi. Vile vile, ripoti ilisema mabweni yana msongamano mkubwa wa wanafunzi ambapo njia za dharura hazipo au zilikuwa zimezibwa, huku milango midogo ikizuia uokoaji wa haraka wakati wa moto. Katika baadhi ya shule, msongamano ulisababisha wanafunzi kulala kwenye vitanda vya ghorofa tatu au kushirikiana vitanda, hali iliyoongeza misongamano na kupunguza nafasi za kutorokea wakati wa dharura. Pia iliripotiwa kuwa baadhi ya mabweni yalikuwa yakifungwa kutoka nje usiku ili kuzuia wanafunzi kuhepa nje ya shule, jambo ambalo ni hatari kubwa endapo uokoaji wa haraka utahitajika. Shule pia zinatakiwa kuwa na vizima-moto vinavyofanya kazi na kufunga kengele za tahadhari katika maeneo muhimu na yanayofikika kirahisi. Wanafunzi na walimu wanatarajiwa kushiriki mazoezi ya dharura angalau mara mbili kila muhula, huku idara za zimamoto za maeneo zikialikwa kutoa mafunzo na maonyesho ya kuzuia moto na jinsi ya kukabiliana na dharura. Kujirudia kwa majanga haya, licha ya kanuni zilizopo na onyo la mara kwa mara kutoka kwa wachunguzi, kunaonyesha kuwa usalama shuleni bado ni changamoto sugu inayohitaji zaidi ya sera na ahadi.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
