“MAAFISA wa afya ya umma wako katika hali ya tahadhari kubwa kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya nyani maarufu kama Mpox katika Kaunti ya Embu. Kulingana na Gavana Cecily Mbarire, kisa kimoja cha ugonjwa huo kimethibitishwa katika eneo hilo. Akizungumza katika Uwanja wa Nembure, Kaunti Ndogo ya Manyatta, Bi Mbarire alisema maafisa wa afya ya umma wako mashinani kuhakikisha ugonjwa huo hausambai. Aliwataka wakazi kutembelea vituo mbalimbali vya afya katika eneo hilo mara tu wanapoanza kuonyesha dalili za ugonjwa huo. "Tunawaomba wakazi kuchukua ugonjwa huu kwa uzito na kutafuta matibabu mara moja wanapoanza kuonyesha dalili," alisema. Hivi karibuni, mwanamke mwenye umri wa miaka 29 kutoka eneo la Kagaari aligunduliwa kuwa na homa hiyo ya nyani. Bi Mbarire alisema kuwa mgonjwa huyo amewekewa masharti ya kutosafiri ili kuzuia kuenea kwa maradhi hiyo. Kuhusu ugonjwa wa Ebola, Bi Mbarire aliitaka serikali kuzingatia maoni ya Wakenya kabla ya kuanzisha kituo cha kuwatenga wagonjwa wa Ebola wa Amerika, nchini "Wakenya wana wasiwasi, na serikali haipaswi kuharakisha ujenzi wa kituo hicho," akasema. Gavana huyo alisema tathmini ya kina inapaswa kufanywa na maoni ya Wakenya kuzingatiwa kabla ya kituo hicho kujengwa Kenya. Mwakilishi wa Wadi ya Ruguru-Ngandori, Muturi Mwombo, alisema anapinga kabisa wazo la kuanzishwa kwa kituo hicho cha Ebola. "Kama viongozi, tunapaswa kuungana na kukataa pendekezo la kuanzishwa kwa kituo hicho cha Ebola," akasema Bw Mwombo.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
