skipToContent
🌐All

Hofu wazee hewa wanafaidi mpango wa Inua Jamii

Taifa Leo (Swahili) Global
Hofu wazee hewa wanafaidi mpango wa Inua Jamii
SERIKALI imeeleza wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa watu hewa katika mpango wa Inua Jamii, jambo linalofichua mianya mikubwa katika utoaji wa mabilioni ya pesa zinazonuiwa kusaidia wazee na watu wanaoishi na ulemavu nchini. Katibu katika Idara ya Ulinzi wa Jamii na Masuala ya Wazee Joseph Motari, alisema kuwa orodha ya watu 1.2 milioni wanaolengwa huenda haiakisi idadi halisi ya wanaonufaika na mpango huo kote nchini. Akizungumza Jumatano mjini Ilbisil, Kaunti ya Kajiado, wakati wa kuzindua zoezi la majaribio ya usajili wa kidijitali kwa wote wanaonufaika na mpango huo, Bw Motari, alisema serikali inalenga kuziba mianya ya wizi wa fedha kupitia walengwa hewa. Zoezi hilo litafanyika nchi nzima kuanzia Juni hadi Julai mwaka huu. “Mpango huu unahusisha uthibitisho wa uhai wa kila anayenufaika pamoja na walezi wao ambao watalazimika kujitokeza binafsi kila baada ya miezi mitatu ili data yao ichukuliwe,” alisema Bw Motari. Alikiri kuwa imekuwa vigumu kwa serikali kujua iwapo baadhi ya wanaolengwa katika mpango huo wamefariki au kuondoka kwenye mpango huo huku ikitegemea taarifa za machifu. “Tumepoteza pesa za walipa ushuru tangu malipo ya M-Pesa yaanzishwe mwaka jana. Sasa tunachukua hatua kali kuziba mianya hiyo,” aliongeza. Ingawa hakufichua kiwango cha fedha kilichopotea, serikali imekuwa ikitoa takriban Sh2.4 bilioni kila baada ya miezi miwili, sawa na Sh28.8 bilioni kwa mwaka. Usajili huo mpya utahusisha kuchukuliwa kwa alama za vidole na picha za uso kwa wanaonufaika na mpango wa wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 70 pamoja na walezi wa watu wanaoishi na ulemavu mkali. Bw Motari alisema serikali itapeleka vifaa vya usajili hadi vijijini ili kuwafikia wazee wasioweza kutembea kwa urahisi. “Tuna vifaa vya kutosha kuhakikisha kila anayenufaika anasajiliwa hata katika maeneo ya mbali. Tukigundua kuwa watu 10 wameondoka kwenye mpango, basi wengine 10 wataongezwa,” alisema.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.