“KUHAMISHWA kwa magunia 26, 220 ya sukari inayoshukiwa kuwa hatari kutoka bohari ya Mombasa kwenda Nairobi kupitia Reli ya Kisasa (SGR) kumeibua hofu bungeni, huku wabunge wakieleza kwamba huenda tayari imeingia sokoni na kutumiwa na wananchi wasio na habari. Shehena hiyo ni sehemu ya zaidi ya tani 27,839 za sukari iliyodaiwa kuingizwa nchini kwa matumizi ya viwandani Januari 15 2026. Hata hivyo, sasa wabunge wanataka Bodi ya Sukari Kenya kutoa majibu ya kina kuhusu mchakato mzima wa usafirishaji, uhifadhi na iwapo sukari hiyo imeingia katika biashara ya kawaida. Katika kikao na Kamati ya Bunge kuhusu Biashara, Viwanda na Ushirika, wabunge walihoji Kaimu Afisa Mkuu wa Kaunti wa Bodi ya Sukari Kenya, Jude Chesire, kuhusu jinsi sukari hiyo ilivyohamishwa kutoka Mombasa hadi Nairobi bila taarifa za wazi za usalama. Bw Chesire alishindwa kueleza kwa kina nambari za mabehewa ya SGR yaliyobeba magunia hayo 26,220 na pia hakuweza kutoa majina ya mabohari ambayo sukari hiyo inadaiwa kuhifadhiwa baada ya kufikishwa Nairobi, jambo lililozua shaka zaidi miongoni mwa wabunge. “Tunahitaji stakabadhi hizi kwa dharura ili kuhakikisha maisha ya Wakenya yanalindwa,” alisema Mwenyekiti wa kamati hiyo, Benard Shinali, akionya kuwa ukosefu wa uwazi unaweza kuhatarisha afya ya umma. Naibu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Marianne Keitany, alihoji kwa nini mzigo huo uliondolewa Mombasa na kupelekwa Nairobi kabla ya kukamilika kwa taratibu za uhakiki na usalama. “Afisa huyu si mkweli; hivi ndivyo sukari hatari ilivyoingia sokoni miaka iliyopita. Kwa nini haikubaki Mombasa hadi mmiliki apate vibali?” alihoji Bi Kitany. Mbunge wa Mathare, Anthony Oluoch, aliunga mkono kauli hiyo akisema kuwa historia ya bidhaa hatari kuingia sokoni mara nyingi huanza kwa kuhamishwa ghafla kati ya mabohari. “Mara nyingi tunaambiwa bidhaa iko salama, kuna timu ya mashirika mbalimbali, lakini baadaye tunakuta bidhaa hiyo sokoni tayari,” alisema. Hata hivyo, Bw Chesire alijaribu kuwahakikishia wabunge kwamba sukari hiyo haijawahi kuingia sokoni na bado iko chini ya ulinzi mkali wa polisi. Alieleza kuwa sukari hiyo iliingizwa ikiwa ghafi kwa matumizi ya viwandani na bado iko katika bohari la forodha ndani ya Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA), Mombasa, ikisubiri kukamilishwa kwa taratibu za forodha. “Mzigo huu haujawahi kusambazwa nchini. Bado umehifadhiwa salama Mombasa chini ya ulinzi mkali,” alisema. Stakabadhi zilizowasilishwa bungeni zinaonyesha kuwa mzigo huo ulipata kibali cha forodha Aprili 24 2026, na usafirishaji wake ulianza Mei 2, 2026, huku mabehewa 19 ya kwanza yakifika Nairobi Mei 3, 2026 yakiwa na magunia 26,220. Bodi ya Sukari ilisisitiza kuwa sukari hiyo ni ya viwandani, ambayo si salama kwa matumizi ya binadamu na hutumika katika viwanda kama vile mikate, vinywaji na usindikaji wa chakula. Serikali pia ilieleza kuwa iliunda kikosi cha mashirika mbalimbali ikijumuisha Bodi ya Sukari, KRA, KEBS, Wizara ya Viwanda na Polisi ili kusimamia uingizaji na matumizi yake na kuzuia kuingizwa sokoni. Hata hivyo, wabunge walitaka majibu zaidi, wakionya kuwa ukosefu wa uwazi unaweza kuhatarisha afya ya mamilioni ya Wakenya iwapo sukari hiyo itaingia sokoni kwa siri.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
