skipToContent
🌐All

IPOA yashindwa kuchunguza kesi ya malalamishi dhidi ya polisi kutokana na bajeti ndogo

Taifa Leo (Swahili) Global
IPOA yashindwa kuchunguza kesi ya malalamishi dhidi ya polisi kutokana na bajeti ndogo
MAMLAKA Huru ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA) imelemewa na mrundiko wa kesi 3,600 ambazo hazijashughulikiwa kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha. Kesi nyingi zilizokwama ni malalamishi kutoka kwa wananchi dhidi ya maafisa wa polisi. Mamlaka hiyo iliambia Kamati ya Bunge kuhusu Utawala na Usalama wa Ndani wakati wa uchunguzi wa makadirio ya bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2026/2027 kuwa mbali na kesi 3,600 zilizosalia, inahitaji rasilimali zaidi ili kukamilisha angalau kesi 971 na kusimamia zaidi ya kesi 300 zinazoendelea mahakamani katika mwaka ujao wa kifedha. Naibu Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa IPOA, Festus Kinoti aliambia kamati hiyo kuwa wanahitaji fedha zaidi ili kuharakisha uchunguzi na kumaliza kesi zilizokwama. “Tuna mrundiko wa kesi 3,600 zinazohitaji uchunguzi. Tunatarajia kukamilisha kesi 971 na pia kufanya uchunguzi mwingine 1,450,” alisema Bw Kinoti. Mamlaka hiyo iliwaomba wabunge kuidhinisha nyongeza ya Sh1.1 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2026/27 ili kusaidia uchunguzi, kufungua afisi za kikanda na kugharamia operesheni za siri wanapotekeleza majukumu yao kote nchini. Katika juhudi za kushughulikia ongezeko la kesi huku rasilimali zikiwa chache, Naibu Mwenyekiti wa IPOA, Ann Wanjiku alisema mamlaka hiyo imeanzisha mbinu mbalimbali ikiwemo sera ya utatuzi mbadala wa migogoro (ADR) kushughulikia malalamishi madogo kama vile polisi kutotekeleza wajibu wao. “Awali tulikuwa tunashughulikia kesi zote kwa usawa, lakini kupitia taratibu mpya za kazi sasa tunaweza kuzipa kipaumbele kesi zilizo na maslahi ya umma na kuharakisha malalamishi ya dharura,” alisema Bi Wanjiku. Aliambia kamati hiyo kuwa kufikia Desemba mwaka jana, mamlaka hiyo ilikuwa imefunga takriban faili 500 baada ya uchunguzi kubaini kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuendelea na kesi hizo. Ili kupunguza idadi kubwa ya kesi zinazowasilishwa IPOA, Bi Wanjiku alisema kuna haja ya kuimarisha Kitengo cha Masuala ya Ndani cha Huduma ya Kitaifa ya Polisi ili malalamishi mengi yashughulikiwe ndani ya idara hiyo kabla ya kufikishwa IPOA. “Sheria yetu inatutaka kusimamia Kitengo cha Masuala ya Ndani. Ikiwa kitengo hicho kitapewa wafanyakazi na fedha za kutosha, kesi nyingi zinazofikishwa IPOA zitatatuliwa ndani ya polisi,” alisema. Mwanachama wa bodi ya IPOA Boniface Samati alisema mamlaka hiyo hupokea maelfu ya malalamishi kila mwaka, mengi yakihusiana na polisi kushindwa kuchukua hatua baada ya wananchi kutoa ripoti katika vituo vya polisi. “Kesi nyingi tunazopokea zinahusu polisi kutotekeleza wajibu wao. Wananchi wanaripoti kesi vituoni lakini hakuna hatua inayochukuliwa, na hivyo kulazimika kuja IPOA,” alisema Bw Samati. Kamati hiyo ilieleza wasiwasi kuhusu ucheleweshaji wa uchunguzi licha ya matumizi ya kawaida ya IPOA kuongezwa kutoka Sh1.406 bilioni hadi Sh1.457 bilioni katika mwaka huu wa kifedha.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.