“DUBAI/DORAL, Florida: JESHI la Iran Jumatatu, Mei 4, 2026 lilionya wanajeshi wa Amerika kutoingia katika Mkondo wa Hormuz baada ya Rais Donald Trump kusema kuwa Amerika itaanza kusaidia katika kuzikomboa meli zilizokwama katika njia hiyo ya baharini kufuatia vita vya Amerika na Israeli dhidi ya Iran. Hata hivyo, rais huyo hakutoa maelezo ya kina kuhusu jinsi usaidizi wa meli hizo utakavyoendeshwa. Wahudumu wa meli hizo sasa wanakumbwa na uhaba wa chakula na mahitaji mengine ya kimsingi baada ya safari za vyombo hivyo kukatizwa na Iran. “Tumeziambia nchi hizi kwamba tutasaidia meli zao kuondoka kutoka njia hiyo ya majini iliyofungwa, ili ziweze kuwa huru kuendelea na shughuli zao,” Trump akasema Jumapili kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social . Lakini jeshi la Iran lilijibu kwa kuonya wanajeshi wa Amerika kutokaribia mkondo huo. Lilisema wanajeshi wake “watajibu kwa ukali” tishio lolote na kwamba “meli za mafuta na za mizigo zisiendelee na safari bila kushirikiana na jeshi la Iran.” “Tumesema kila mara kwamba usalama wa Mkondo wa Hormuz uko mikononi mwetu na usafiri wa meli unahitaji kibali na ushirikishi kutoka kwa jeshi la Iran,” Ali Abdollahi, mkuu wa kikosi cha pamoja alisema kwenye taarifa. Mamia ya meli zenye zaidi ya wahudumu 20,000 zimeshindwa kupitia katika Mkondo wa Hormuz tangu kuanza kwa vita kati ya Amerika na Israel, dhidi ya Iran, shirika la kimataifa kuhusu usafiri majini (IMO) linasema. Kikosi Maalum cha jeshi la Amerika (Centcom) kilisema litapiga jeki juhudi za kusaidia meli zilizokwama kwenye Mkondo wa Hormuz kwa kutumia wanajeshi 15,000, zaidi meli 100 za kivita, ndege za kivita na droni. “Operesheni hiyo inalenga kurejesha uhuru za usafiri wa meli za kibiashara kupitia mkondo huo,” kikosi hicho kikasema kwenye taarifa. “Usaidizi wetu kwa shughuli hii ni muhimu katika kuleta usalama wa kikanda na kulinda uchumi wa ulimwengu huku pia tukidumisha vizuizi katika bandari za Iran,” Admiral Brad Cooper, kamanda wa Centcom, akaeleza kwenye taarifa hiyo. Baada ya kauli ya Trump, Shirika Uingereza kuhusu Biashara Majini liliripoti kuwa meli moja ya kubeba mafuta iliripotiwa kugongwa na vitu visivyojulikana katika mkondo huo. Shirika hilo lilisema wanafanyakazi wote waliripotiwa kuwa salama kufuatia kisa hicho, kilichotokea kaskazini mwa Fujairah katika Umoja wa Milki ya Kiarabu (UAE), japo maelezo ya kina hayakutolewa. Kwa muda wa miezi miwili iliyopita, Iran imekuwa ikizuia karibu meli zote za kusafirisha mafuta na gesi kutoka eneo la Ghuba, isipokuwa meli zake; hatua iliyochangia kupanda kwa bei ya kawi. Baadhi ya meli zilizojaribu kupitia Mkondo huo ziliripotiwa kushambuliwa huku Iran ikinasa meli nyingine. Mnamo Aprili, Amerika imeweka vizuizi dhidi ya meli zote kutoka bandari za Iran. Utawala wa Trump umekuwa ukisaka usaidizi kutoka kwa nchini zingine kwa lengo la kushirikiana nazo kurejesha safari za meli kupitia mkondo huo. Kikosi cha Centcom kilisema juhudi za sasa za kusaidia meli kupitia njia hiyo zitashirikisha “hatua za kidiplomasia na ushirikishi wa kijeshi.” Haikujulikana mara moja ni nchi gani operesheni ya Amerika itasaidia au namna operesheni itavyoendeshwa. Ikulu ya White House haikujibu ombi la Reuters kwamba itoe kauli yake kuhusu operesheni hiyo. Rais Trump alitisha kwamba hatua zozote za kuvuruga operesheni ya Amerika “zitakabiliwa kwa nguvu kali”. Wakati huo huo, Iran ilisema Jumapili kwamba haijapokea majibu kutoka Amerika kuhusu pendekezo lake la hivi punde kuhusu mazungumzo ya amani. Ilisema hayo siku moja baada ya Trump kusema huenda akapinga pendekezo la Iran kwa sababu “hawajagharamika inavyopasa”. Kwa mfano, Iran ilitaka suala la mpango wake wa nyuklia lijadiliwe baadaye kwani “haina madhara yoyote.” Aidha, ilitaka Amerika iondoe vizuizi katika bandari zake na iondoe wanajeshi wake katika maeneo ya karibu.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
