skipToContent
🌐All

JIFUNZE LUGHA: Makosa katika kukanusha sentensi za wakati uliopita hali ya kuendelea

Taifa Leo (Swahili) Global
JIFUNZE LUGHA: Makosa katika kukanusha sentensi za wakati uliopita hali ya kuendelea
KUKANUSHA ni kukataa kuwa jambo au tukio limetokea au litatokea. Tunapokanusha sentensi huwa tunazingatia kiambishi ngeli cha nomino iliyotumiwa kutungia sentensi hiyo. Pia sharti tuzingatie kiambishi cha wakati. Baadhi ya nyakati ni: wakati uliopo, wakati uliopita, wakati ujao, hali ya mazoea na wakati timilifu. Pia kuna nyakati na hali ya kuendelea. Sentensi inapokuwa katika wakati na hali ya kuendelea huleta dhana ya kuwepo kwa vitendo viwili. Kitendo cha kwanza hutokea huku kitenzi cha pili kikifuata na vyote kuendelea kufanyika pamoja. Baadhi ya nyakati na hali ya kuendelea ni: wakati uliopo hali ya kuendelea, wakati uliopita hali ya kuendelea na wakati uliopita hali ya kuendelea. Kitendo kilicho katika wakati uliopita hali ya kuendelea huwakilishwa kwa kutumia –kuwa pamoja na ki-. Mfano: Shangazi alikuwa akipika mama alipowasili nyumbani. Wapo baadhi ya wanafunzi ambao hukumbwa na changamoto katika kukanusha sentensi zilizo katika wakati uliopita hali ya kuendelea. Utapata sentensi kama vile: Mwalimu alikuwa akifundisha wageni walipoingia darasani mwetu, ikiwa imekanushwa kwa: Mwalimu hakukuwa akifundisha wageni walipoingia darasani mwetu. Nayo sentensi: Kipindi cha Kiswahili kilikuwa kimekamilika kocha alipowaita wachezaji imekanushwa kwa: Kipindi cha Kiswahili hakikukuwa kimekamilika kocha alipowaita wachezaji. Sentensi hizo zimekanushwa visivyo. Silabi ku- haifai kurudiwa katika ukanusho wa sentensi zilizo katika wakati uliopita hali ya kuendelea. Ili kuzikosoa tunafaa kusema: Mwalimu hakuwa akifundisha wageni walipoingia darasani mwetu. Kipindi cha Kiswahili hakikuwa kimekamilika kocha alipowaita wachezaji.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.