skipToContent
🌐All policy

Jinsi Gachagua alivyomkaba koo Rais Ruto kwenye uchaguzi mdogo Emurua Dikirr

Jinsi Gachagua alivyomkaba koo Rais Ruto kwenye uchaguzi mdogo Emurua Dikirr
KIONGOZI wa chama cha Democracy for Citizns Party (DCP), Rigathi Gachagua aliweza kupenya katika ngome ya kisiasa ya aliyekuwa mkubwa wake Rais William Ruto katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Emurua Dikirr. Hali hiyo ilitafsiriwa kama ishara ya mabadiliko ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Ingawa mgombea wa DCP, Felix Kibet Rotich, hakushinda uchaguzi huo wa Alhamisi dhidi ya mgombea wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), David Kipsang Keter, wachambuzi wanasema chama hicho kilitoa ushindani mkubwa katika eneo ambalo limekuwa likionekana kuwa ngome ya kisiasa ya Rais Ruto. Bw Keter alipata kura 18,266 huku Bw Rotich akipata kura 10,760 katika eneo lenye wapigakura 44,457 na kutangazwa mshindi wa uchaguzi huo na Afisa Msimamizi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Caleb Kegonde Ijumaa asubuhi. Uchaguzi huo mdogo ulifuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Johana Ngeno aliyefariki Februari 28 katika ajali ya helikopta huko Mosop, Kaunti ya Nandi. Katika ajali hiyo, Bw Ngeno alifariki pamoja na rubani George Were, mpiga picha Nick Kosgei, mwalimu Carlos Kibet Keter, askari wa Huduma ya Misitu Kenya Amos Kipngetich Rotich na afisa wa itifaki wa serikali ya Kaunti ya Narok Wycliff Kiprotich Rono. Bw Ngeno alikuwa mwanasiasa aliyependa kubadili vyama. Mwaka wa 2013 alichaguliwa kupitia chama cha Kenya National Congress (KNC), mwaka wa 2017 kupitia Kanu na mwaka wa 2022 kupitia UDA. Eneo la Emurua Dikirr lina wakazi wengi kutoka jamii ya Kipsigis waliohamia eneo hilo miaka ya 1950 katika eneo la Transmara Mashariki, Kaunti ya Narok, huku jamii ya Wamaasai ikiwa wenyeji asili. Aliyekuwa Meya wa Bomet, Kipkemoi Barsumei, alisema matokeo hayo yanaonyesha wazi kuwa wapigakura wa Rift Valley wanaanza kuonyesha kutoridhika kabla ya uchaguzi wa 2027. “Kwamba Bw Gachagua, hata bila kufika eneo hilo binafsi, aliweza kusaidia mgombea wake kupata zaidi ya kura 10,000 ni ishara kuwa wapigakura wa eneo hili wanaonyesha hali ya kutoridhika kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027,” alisema Bw Barsumei. Aliongeza kuwa viongozi wa juu wa UDA hawawezi kupuuza ishara hiyo wakidhani wapigakura wa Rift Valley watampigia kura Rais Ruto moja kwa moja mwaka wa 2027. “Tusisahau kuwa Rais anaishi katika eneo jirani la Kilgoris, lakini mgombea wa Gachagua bado alipata matokeo mazuri,” alisema. Bw Barsumei pia alisema wiki tatu zilizopita Rais Ruto alikiri kuwa wakazi wa Rift Valley hawakuwa wakijitokeza kwa wingi kujisajili kama wapigakura katika zoezi la IEBC, jambo ambalo linaonyesha wananchi wengi hawako tayari kumchagua tena 2027. Bw Keter, mfanyabiashara ambaye zamani alikuwa mshirika wa Bw Ngeno kabla ya kuwa mpinzani wake wa kisiasa, alisema atahudumia wakazi wote bila kujali misimamo yao ya kisiasa. Alisema changamoto kubwa katika eneo hilo ni barabara mbovu, hospitali zisizo na vifaa vya kutosha, shule chache na miundombinu duni. “Masuala yanayoathiri eneo hili ni miundombinu mbovu hasa barabara, vituo vya afya, shule na taasisi nyingine za masomo. Nitayapatia kipaumbele kwa ushirikiano wa serikali ya kaunti na serikali kuu,” alisema Bw Keter. Aliongeza kuwa licha ya ushindani wa kisiasa, marehemu Ngeno alikuwa rafiki yake. “Nilijua siku moja nitakuwa Mbunge wa Emurua Dikirr lakini sikutarajia uchaguzi mdogo ambao Bw Ngeno hangekuwa kwenye karatasi ya kura. Kifo chake kabla ya kumaliza muhula wake wa tatu kinahuzunisha sana,” alisema. Katika mchujo wa UDA, Bw Keter alipata kura 13,749 dhidi ya kura 13,394 za Benard Ngeno aliyekuwa msaidizi wa marehemu Johana Ngeno. Bw Benard Ngeno hakukubali matokeo hayo, hali iliyochangia migawanyiko miongoni mwa wafuasi wa UDA. Aidha, mjane wa marehemu mbunge huyo, Nayianoi Ngeno, ambaye awali alitangazwa kuwa mgombea wa familia, alijiondoa ghafla katika kinyang’anyiro hicho chini ya mazingira ambayo hayajaelezwa wazi. Baadaye aliteuliwa katika bodi ya shirika la serikali na kumuunga mkono Bw Keter, hatua iliyosaidia kuimarisha kampeni za UDA dhidi ya mgombea wa DCP.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.