skipToContent
🌐All

Jinsi kilimo cha hoho kinavyompiga jeki mashinani

Taifa Leo (Swahili) Global
Jinsi kilimo cha hoho kinavyompiga jeki mashinani
TAKRIBAN kilomita tatu kutoka barabara ya Elburgon-Njoro, tulifika kwenye mpaka wa mashamba ya Tegat na Nyakiambi katika Kaunti Ndogo ya Molo ambapo Susan Wairimu hukuza pilipili hoho ndani ya kivungulio. “Nilianza kukuza ndani ya kivungulio hiki mwaka wa 2024 baada ya kujua kwamba uzalishaji wangu ungeongezeka ikilinganishwa na kupanda kwenye maeneo yaliyo wazi. Pilipili hoho ni nzuri sokoni, hukomaa kwa haraka na huvutia wateja wengi,” anasema Wairimu. Anaeleza kuwa kukuza homo ndani ya kivungulio husaidia kupunguza gharama, kwa sababu zao haliathiriki na magonjwa sana. Wairimu alitumia mtaji wa kati ya Sh250,000 na Sh300,000 kuunda kivungulio cha ukubwa wa mita 17 kwa mita 8 na kununua vifaa vya ujenzi. Anaeleza kuwa baada ya kivungulio kukamilika, alinunua miche 750 hoho nyekundu na njano iliyothibitishwa kutoka kwa wafanyabiashara tofauti katika Kaunti ya Nakuru kwa Sh15 kwa kila mche. "Niliweka safu kati ya 75cm na 65cm na kupanda miche yangu. Kutoka kwa mche mmoja hadi mwingine nilitenganisha kwa 30cm na 45cm huku nikiweka mbolea asilia kutoka kwa mifugo na kuku.” Kati ya siku tatu na saba, aliongeza mbolea ya msingi juu ya miche kwani husaidia katika uundaji na ukuaji wa mizizi. Katika wiki hiyo hiyo, mkulima alinyunyizia dawa ya kuua wadudu wanaokaa kwenye udongo. Katika wiki ya pili na ya tatu, Wairimu alianza kupalilia mazao yake na pia kuyanyunyizia mbolea ya CAN ambayo husaidia kuimarisha ukuaji kutokana na nitrojeni. Anaeleza kuwa katika kipindi hichopia, alinyunyizia dawa ya kuua wadudu na bakteria ili kuzuia mashambulizi huku akiendelea kunyunyizia kila baada ya siku 10 hadi 14. Wakati huu pia aliongeza mbolea ya folia kwa ajili ya matunda na maua. "Maua yalianza kuchipuka baada ya miezi miwili ambapo nilipalilia kwa mara ya pili na kuwa mwangalifu kwa mazao yangu ili iwe na lishe inayofaa ambayo huisaidia kwa kukua vizuri. Pilipili hoho huchukua kati ya miezi mitatu na nusu hadi minne kukomaa na kuwa tayari kuvunwa," anasema. Anaeleza kuwa kupitia usimamizi bora, mmea mmoja unaweza kutoa wastani wa kilo 6.5. Katika mavuno yake ya kwanza, mkulima alivuna kilo 70 na kuuza katika soko la ndani kwa kati ya Sh100 na Sh200 kwa kilo kulingana na mahitaji ya mteja. Uvunaji uliendelea baada ya kila wiki moja, na kusajili ongezeko la uzalishaji kwa kila mavuno. Wakati wa msimu wa mvua, mkulima anasema soko ni zuri ikilinganishwa na misimu ya kiangazi. Msimu wa kuchuma huanza Aprili lakini huongezeka kati ya Juni na Septemba. Katika vipindi hivyo, mkulima huuza kati ya Sh300 na Sh400 kwa kila kilo katika soko la ndani. "Soko la pilipili hoho zenye rangi ni zuri na lina mahitaji mengi kwa sababu sijaweza kukidhi mahitaji ya wateja wangu. Kwa sasa, mimi huvuna kati ya kilo 250 na 300 kila wiki na kuuza kilo moja kwa Sh125,” anaeleza Wairimu, akiongeza kuwa wakati mwingine hununua bidhaa hiyo kutoka kwa wakulima wengine ili kuwaridhisha wateja wake. Wairimu anasema kuwa hawezi kulinganisha kilimo chake cha hoho kwa kupanda mahindi ambayo anasema madalali wametawala kwenye sekta ya mahindi huku wakulima wakijitahidi kupata masoko bora. Hata hivyo, amepanda sehemu ndogo ya mahindi ili kuvuna sileji na kuwalisha ng'ombe wake kwani humpa mbolea na maziwa kwa matumizi ya nyumbani. Anaeleza kuwa ameajiri wafanyakazi wawili ambao humsaidia kwa kazi shambani lakini huwaajiri wafanyakazi zaidi kulingana na kazi. Ili wakulima wafanikiwe katika kilimo cha pilipili hoho, Wairimu anawasihi wale walio tayari kuanza kuwa na maarifa kutoka kwa wale waliojitosa kwa kilimo hiki, kujua hali ya ukulima ambao hutegemea kile wateja wanahitaji, kununua miche iliyothibitishwa na kutafuta masoko ya kuuza mazao yao. Wairimu anasema amepata maarifa kupitia utafiti na kujifunza kupitia mtandaoni, semina, maonyesho na kutafuta ushauri kutoka kwa wakulima wengine walioimarika. “Ninafanya upimaji wa udongo kupitia sekta ya kibinafsi baada ya kila msimu na kupokea matokeo baada ya siku saba. "Maafisa ugani kutoka serikali ya kaunti wanapaswa kuwatembelea wakulima ili kuwahamasisha na kuwaelimisha kama inavyofanyika kwenye mazao mengine kama vile viazi, maparachichi na wakulima wa maziwa ili kujifunza kuhusu usimamizi, magonjwa na udhibiti wa wadudu miongoni mwa mahitaji mengine,” anasema. Anataja gharama ya pembejeo za shamba, usimamizi wa wafanyakazi, ukosefu wa umeme na barabara duni kama changamoto kuu katika eneo hilo. Barabara hizo huwa mbovu kwa wateja wanapofika shambani au kusafirisha mazao yao ya shambani hadi sokoni, hasa wakati wa mvua. Mkulima sasa hutumia jenereta kusambaza maji kutoka kwenye kisima alichochimba shambani hadi kwenye tangi kubwa lililopo karibu na kivungulio. Anasema kuwa anatumia fedha nyingi kwa jenereta hiyo kufuatia gharama kubwa ya bei ya mafuta. "Mpango wangu ni kupanua sehemu yangu hadi ekari 10 katika miaka mitatu ijayo na kufanya kilimo cha kikaboni ambacho kinahitajika ili kuboresha afya ya mtumiaji kwa kutoa matunda yaliyo bora kwa matumizi ya binadamu. Pia nataka kuwa sokoni wakati wote na kuwa mkulima anayeongoza katika eneo hilo kwa kutoa na kukidhi mahitaji ya wateja wangu," anaongeza Wairimu.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.