skipToContent
🌐All

Jinsi Uhuru alivyokataa juhudi kadhaa za kuridhiana na Ruto

Jinsi Uhuru alivyokataa juhudi kadhaa za kuridhiana na Ruto
MAELEZO mapya yameibuka kuhusu jinsi Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta alivyokataa juhudi kadhaa za maridhiano na mrithi wake William Ruto huku mvutano wa kisiasa kati ya viongozi hao wawili ukiendelea kuongezeka. Kwa mujibu wa watu wa karibu na viongozi hao, Rais Ruto alianza juhudi za kutafuta handisheki na Uhuru mara tu baada ya kuapishwa Septemba 2022 ili kupunguza uhasama ulioanza baada ya uchaguzi wa 2017 na kuongezeka zaidi wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022. Maafisa wa Ikulu walisema Rais Ruto alimfikia Uhuru siku ya kuapishwa kwake na kumweleza umuhimu wa kushirikiana kwa ajili ya utulivu wa taifa na masuala ya kidiplomasia ya kikanda. Wakati huo, Bw Uhuru alikuwa akihusika katika juhudi za kuleta amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na SADC. Licha ya juhudi hizo, uhusiano wao uliendelea kuwa baridi huku viongozi wa Kenya Kwanza wakimshutumu Bw Uhuru kwa kuunga kisiri maandamano ya upinzani yaliyoongozwa na marehemu Raila Odinga mwaka wa 2023. Kwa mujibu wa maafisa wa serikali, Rais alimfikia tena Uhuru wakati wa maandamano ya vijana ya Juni 2024 yaliyotikisa serikali yake. Hatua hiyo ilifikia kilele Desemba 9, 2024 wakati Rais Ruto alipomtembelea Uhuru nyumbani kwake Ichaweri, Kiambu akiwa amebeba mbuzi 12 kama ishara ya maridhiano. Maafisa hao walisema mkutano huo ulikuwa wa kirafiki na kwamba Uhuru hakukataa waziwazi juhudi hizo, lakini matamshi na mienendo yake ya baadaye ilionyesha hakuwa tayari kwa ushirikiano kisiasa. Baada ya mkutano huo, serikali ilimteua Mutahi Kagwe kuwa Waziri wa Kilimo, William Kabogo kuwa Waziri wa Habari na Teknolojia huku Lee Kinyanjui akipewa wizara ya Biashara na Uwekezaji, hatua zilizofasiriwa kama juhudi za kujenga maridhiano ya kisiasa. Hata hivyo, miezi michache baadaye, Uhuru aliwahimiza vijana kuendelea kudai uwajibikaji kutoka kwa viongozi walio mamlakani. Alisema vijana hawapaswi kuogopa kupigania haki zao na mustakabali wao. Kauli hizo zilizua mashambulizi kutoka kwa viongozi wa UDA. Katika taarifa ya pamoja, Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar na mwenyekiti wa chama hicho Cecily Mbarire walimshutumu Uhuru kwa kuendeleza siasa za kisasi na kujaribu kudhoofisha serikali ya Rais Ruto. Kwa upande wake, Naibu Kiongozi wa Jubilee Jeremiah Kioni alisema Uhuru amekuwa akiwaambia viongozi wa serikali kushughulikia matatizo ya uchumi badala ya kulalamikia tofauti zao za kisiasa. Mvutano huo pia ulijitokeza katika mkutano wa Muungano wa Afrika nchini Ethiopia mapema mwaka huu ambapo Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alidaiwa kujaribu kuwapatanisha viongozi hao wawili. Wakati huo huo, viongozi wa Kenya Kwanza akiwemo Aaron Cheruiyot wameendelea kumshutumu Uhuru kwa madai ya kujaribu kuzuia Rais Ruto kupata muhula wa pili mwaka wa 2027. Kwa upande wake, Uhuru ameendelea kuikosoa serikali kwa kushindwa kupunguza gharama ya maisha na kuwasikiliza Wakenya wanaolalamikia hali ngumu ya uchumi.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.