skipToContent
🌐All

Jinsi ya kumuonyesha mwanamume mapenzi

Jinsi ya kumuonyesha mwanamume mapenzi
KATIKA mahusiano mengi ya kimapenzi, wanawake wengi hutamani kueleweka, kusikilizwa na kupendwa kwa dhati. Hata hivyo, katika harakati hizo, wakati mwingine wanawake husahau kuwa wanaume pia wanahitaji kueleweka, kuheshimiwa na kuthaminiwa. Wataalam wa masuala ya mahusiano wanasema siri ya mapenzi ya kudumu ni pande zote mbili kujifunza kuelewana na kuvumiliana. Mshauri wa masuala ya ndoa na familia, Esther Perel, anasema wanaume wengi hukua wakifundishwa kuficha hisia zao, jambo ambalo huwafanya waonekane wagumu au wasiojali ilhali ndani yao wanahitaji upendo na kuthaminiwa kama wanawake. “Kila binadamu anahitaji kusikilizwa na kueleweka. Wanaume wengi hawasemi wanachohisi, lakini wanahitaji nafasi salama ya kueleza mawazo yao bila kuhukumiwa,” anasema Perel. Kauli hiyo inaonyesha umuhimu wa mwanamke kujifunza kumwelewa mwanaume wake hata katika nyakati ambazo hana maneno mengi au anapokuwa na msongo wa mawazo. Jambo la kwanza katika kumpenda mwanamume ni kuelewa kuwa hakuna mwanamume mkamilifu. Kuna siku atakuwa na hasira, wakati mwingine atakuwa na uchovu wa maisha na kushindwa kuonyesha mapenzi kama ulivyotarajia. Hilo halimaanishi kwamba hakupendi. Mahusiano yanahitaji uvumilivu na kukubali mapungufu ya kila mmoja. Wataalam pia wanaeleza kuwa kumpenda mwanamume hakumaanishi kumbana au kumfanya awe dunia yako yote. Mwanasaikolojia John Gottman, anasema mahusiano yenye afya yanahitaji kila mmoja kubaki na uhuru wake binafsi. “Mapenzi ya kweli hujengwa kwa kuaminiana, si kudhibiti kila hatua ya mwenzi wako,” anasema Gottman. Kwa mujibu wa wataalam hao, mwanamume anahitaji nafasi ya kufanya mambo anayopenda, kuwa na marafiki wake na kutekeleza majukumu yake bila kuhisi ananyimwa uhuru. Ikiwa anakupenda kwa dhati, hatafanya makusudi jambo la kukuumiza. Aidha, mapenzi yanahitaji ushirikiano wa pande zote mbili. Si mwanaume pekee anayepaswa kufanya juhudi katika mahusiano. Mwanamke naye anapaswa kuonyesha kujali kwa kumuuliza mwenzi wake siku yake imekuwaje au kumfariji anapopitia changamoto. Wanaume wengi hupitia matatizo kimya kimya kwa sababu jamii imewafundisha kuwa mwanaume hatakiwi kuonyesha udhaifu. Ndiyo maana mwanamke anayempenda mwanaume wake kwa dhati anapaswa kuwa mtu anayempa amani na faraja. Heshima nayo ni msingi muhimu katika mapenzi. Mwanamke anapomheshimu mwanamume wake, humfanya ajisikie kuthaminiwa. Heshima si kuogopa, bali ni kuthamini mawazo, maamuzi na nafasi yake katika mahusiano. Migogoro inapojitokeza, wataalam wanashauri wanandoa kuzungumza kwa utulivu badala ya kutumia matusi au kejeli. Pia, wanaume wanahitaji kuonyeshwa mapenzi waziwazi. Kukumbatiwa, kusifiwa au kuambiwa maneno mazuri kunaweza kubadilisha hali yake ya moyo. Wakati mwingine ishara ndogo za upendo huwa na maana kubwa kuliko zawadi za gharama kubwa. Vilevile, mwanamume anahitaji umakini na uhakikisho wa mapenzi kama mwanamke anavyohitaji. Anahitaji kujua kuwa ndiye mtu muhimu katika maisha yako. Kumfanya ahisi kupendwa na kuthaminiwa huimarisha uaminifu katika uhusiano. Wataalam wanaonya kuwa hakuna uhusiano mkamilifu. Kutakuwa na nyakati za kutofautiana na kukwazana. Lakini ikiwa kuna upendo wa kweli, uvumilivu na heshima, mahusiano yanaweza kudumu kwa muda mrefu. “Wanawake wanapenda kueleweka sana kiasi kwamba wanasahau kuwa wanaume pia wanahitaji kueleweka. Siri ya mapenzi yenye furaha ni pande zote mbili kujifunza kusikilizana, kuvumiliana na kuthaminiana kila siku,” asema Perel.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.