skipToContent
🌐All

Joyce Lay afunguka kuhusu masaibu yake kisiasa

Joyce Lay afunguka  kuhusu masaibu yake kisiasa
Aliyekuwa Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Taita Taveta na mhubiri wa injili Joyce Lay amevunja kimya chake kuhusu picha zilizosambaa mitandaoni wakati wa ziara ya hivi majuzi ya Rais William Ruto Pwani, akisema kuketi kwake mstari wa mbele katika hafla ya kitaifa hakukuwa kuvunja itifaki bali ni ishara ya kutambuliwa na viongozi wenzake . Katika taarifa ya hisia kali aliyochapisha mtandaoni, Joyce Lay alisimulia jinsi alivyosafiri kutoka Voi alfajiri kuhudhuria hafla katika bustani ya Mama Ngina, ambako alijikuta katikati ya mjadala mtandaoni baada ya picha kuibuka zikimuonyesha akiwa ameketi karibu na viongozi wakuu akiwemo Mbunge wa Taveta John Bwire na Mwakilishi wa Wanawake Taita Taveta Lydiah Haika. Joyce Lay alisema anaelewa vyema itifaki za serikali na kwamba mwanzoni alichagua kuketi safu kadhaa nyuma ya viongozi waliochaguliwa baada ya kujitambulisha kwa maafisa wa usalama katika eneo la wageni waalikwa. Kulingana naye, Bw Bwire alimshawishi mara kadhaa ahamie viti vya mbele akisisitiza kuwa yeye pia ni kiongozi na alikuwa amewasili mapema katika hafla hiyo. “Ninafahamu itifaki,” alisema huku akieleza kuwa hata alifikiria kuondoka kwenye kiti hicho viongozi wengine wa Pwani walipowasili lakini aliraiwa abaki. Hata hivyo, mbali na suala la kuketi, Joyce Lay alitumia fursa hiyo kuelezea kile alichodai kuwa ni miaka ya kutengwa kisiasa na changamoto za kibinafsi. Alidai kuwa baada ya uchaguzi wa 2017, alitengwa katika mikutano ya viongozi wa hadhi ya juu Taita Taveta na kuzuiwa kutangamana na maafisa wakuu serikalini. Mwanasiasa huyo pia alisimulia tukio moja wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2022 ambapo anadai alialikwa kwenye mkutano ulioandaliwa na aliyekuwa Naibu Rais William Ruto mjini Mombasa, lakini akiwa safarini kutoka Voi aliambiwa asihudhurie kwa sababu baadhi ya viongozi walipinga uwepo wake. “Niligeuza tu gari langu na kurudi nyumbani,” alisema. Joyce Lay pia alidai kuwa kulikuwa na taarifa zilizosambazwa kumuonyesha kana kwamba alikuwa amefilisika na mwenye msongo wa mawazo baada ya kuelekeza nguvu zake katika uinjilisti na huduma ya injili. Licha ya changamoto hizo, alisema aliendelea kusimama imara katika maombi na huduma ya Mungu, akiongeza kuwa “milango iliyokuwa imefungwa kabisa ilianza kufunguka” tangu mwaka jana. Alidokeza kuwa Rais Ruto anafahamu baadhi ya changamoto alizopitia na kwamba kiongozi huyo wa nchi alionekana kufurahia kumuona wakati wa hafla hiyo. Katika ushuhuda wake mrefu, mhubiri huyo alisema msamaha na imani vimemsaidia kushinda uchungu na uhasama wa kisiasa. “Niliwasamehe wote, hata wale waliopigana nami kisiasa, walionipinga na kujaribu kuniangusha,” aliandika. Alisisitiza kuwa njia yake ya sasa inaongozwa na kile alichokitaja kama wito wa Mungu na akaapa kuendelea na uinjilisti pamoja na huduma kwa umma licha ya kukosolewa. Katika miaka ya hivi karibuni, Joyce Lay ameunganisha siasa na huduma ya injili kupitia kundi la “The Believers Voice”, ambapo mara nyingi huwa anasambaza ujumbe kuhusu imani, ustahimilivu na uongozi
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.