skipToContent
🌐All

Junior Starlets yafuzu raundi ya mwisho ya kufuzu Kombe La Dunia U17

Junior Starlets yafuzu raundi ya mwisho ya kufuzu Kombe La Dunia U17
NDOTO ya Kenya kufuzu kwa Kombe la Dunia la Wanawake wasizidi miaka 17 mwaka huu, bado iko hai baada ya Junior Starlets kufuzu kwa raundi ya tatu na ya mwisho ya michujo jana. Starlets walitinga hatua hiyo kwa sheria ya bao la ugenini baada ya kutoka sare tasa dhidi ya Uganda katika mechi ya marudiano ya raundi ya pili iliyochezwa uga wa Nyayo, Nairobi. Timu hizo zilitoshana nguvu kwa sare ya mabao 1-1 katika mkondo wa kwanza uliochezewa Uwanja wa FUFA Kadiba, jijini Kampala Ijumaa iliyopita. Katika raundi ya mwisho ya kufuzu, Kenya itavaana na mshindi kati ya Afrika Kusini na Tanzania. Afrika Kusini inaongoza kwa mabao 2-0 kabla ya mechi ya marudiano itakayochezwa Pretoria leo. Mechi ya jana ilikuwa ya vipindi viwili tofauti. Uganda walitawala kipindi cha kwanza huku Kenya ikirejea kwa nguvu baada ya mapumziko. Waganda walipata nafasi nyingi za kufunga katika kipindi cha kwanza na wangeweza kuongoza kwa mabao kadhaa kama wangetumia vyema nafasi zao. Mshambuliaji Immaculate Achen alipoteza nafasi ya kwanza ya wazi katika dakika ya tano baada ya kuwazidi mabeki watatu wa Kenya lakini akapiga mpira juu ya lango. Dakika tatu baadaye, fowadi Shadia Nabirye alipenya katika eneo la hatari la Kenya lakini akanyang’anywa mpira kabla hajapiga shuti. Muda mfupi baadaye, Gerevans Dominick Angel alimlazimisha kipa Mishel Okoyo kufanya kazi ya ziada kuzuia shuti la mbali. Nafasi ya kwanza ya Kenya ilikuja dakika ya 14 kupitia mpira wa kona, lakini juhudi za beki Faith Boke hazikuwa na nguvu za kutosha kumtatiza kipa Sharifah Kizito. Uganda waliendelea kushambulia na kumlazimisha Okoyo kutoka golini mapema kumzuia Achen. Wachezaji hao wawili walipata majeraha baada ya kugongana lakini waliendelea na mchezo baada ya kufanyiwa matibabu. Kadri kipindi cha kwanza kilivyoendelea, Kenya ilianza kumiliki mpira zaidi katika eneo la Uganda lakini ilikosa nafasi za wazi za kufunga. Brenda Achieng alionyesha kiwango kizuri upande wa kushoto katika dakika ya 25, ingawa krosi yake ilizuiwa. Dakika saba baadaye, Okoyo aliokoa tena kwa ustadi baada ya Martha Babirye kupiga mpira wa adhabu uliolenga lango. Katika upande wa pili wa mashambulizi, Emily Adhiambo aliingia katika eneo la hatari la Uganda dakika ya 39 lakini shuti lake lilitoka nje kutokana na presha kutoka kwa mabeki. Uganda waliendelea kusaka bao kabla ya mapumziko, lakini safu ya ulinzi ya Kenya ilisimama imara kuhakikisha kipindi cha kwanza kinamalizika kwa sare ya 0-0. Uganda walifanya mabadiliko yao ya kwanza mwanzoni mwa kipindi cha pili, Joan Namakula akiingia kuchukua nafasi ya Cynthia Kirenga. Hata hivyo, Kenya ndiyo iliyoanza vyema kipindi hicho. Achieng aliendelea kuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Uganda kutokana na kasi na ujuzi wake. Dakika mbili baada ya mapumziko, alikosa bao kwa nusura baada ya kunufaika na mpira uliotoka kwenye kona. Baadaye alielekeza krosi hatari mbele ya lango lakini hakukuwa na mchezaji wa Kenya wa kucheka na wavu. Uganda walifanya mabadiliko mengine dakika ya 62, Grace Kawino akiingia badala ya Angel. Kenya nayo ilimleta Elizabeth Opiyo kuchukua nafasi ya Gaudancia Maloba dakika tatu baadaye. Starlets waliendelea kushinikiza wakisaka bao la ushindi lakini penalti ilikataliwa baada ya mwamuzi Emmanuela Akoo wa Sudan Kusini kupuuza madai yao ya kunawa mkono. Kenya ilikaribia zaidi kupata bao wakati mpira wao ulipogonga mwamba wa juu kabla ya mabeki wa Uganda kuondoa hatari. Uganda pia walipata nafasi za kushtukiza, lakini Okoyo aliendelea kung’ara kwa kuokoa michomo muhimu na kuhakikisha Kenya inafuzu kwa raundi ya mwisho ya michujo ya Kombe la Dunia.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.