skipToContent
🌐All

KenHA yatoa Sh4.3 bilioni kuwezesha ujenzi wa barabara Kaunti ya Mombasa

KenHA yatoa Sh4.3 bilioni kuwezesha ujenzi wa barabara Kaunti ya Mombasa
MAMLAKA ya Barabara Kuu nchini (KeNHA) imetoa Sh4.3 bilioni ili kuwezesha ujenzi wa barabara kuu eneo la Mombasa, hatua inayotarajiwa kuwanufaisha zaidi waathiriwa wa mradi huo kupitia fidia na kuimarisha kasi ya utekelezaji wa kazi. Serikali imesema mradi wa Barabara ya Kimataifa ya Bagamoyo-Tanga-Horohoro/Lunga Lunga-Malindi, ambao kwa muda mrefu ulikuwa umekwama kutokana na changamoto za fidia na ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi, sasa utaendelea bila vikwazo. Kwa mujibu wa KeNHA, fedha hizo zitawezesha kukamilika kwa malipo ya fidia kwa wananchi walioathirika na mradi, hatua ambayo itafungua njia kwa wakandarasi kuharakisha kazi zilizokuwa zimekwama kutokana na mchakato wa ununuzi wa ardhi. Naibu Mkurugenzi Mkuu wa KeNHA na Mratibu wa mradi huo, Mhandisi Cleophas Makau, alisema wakati wa ukaguzi kwamba Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) tayari imekamilisha tathmini ya walioathirika na mradi huo, huku Sh3.15 bilioni zikiwa tayari zimetolewa kwa ajili ya fidia ya ardhi. “Tume ya Kitaifa ya Ardhi inaendelea na mchakato wa kufidia walioathirika. Tayari tumeona idadi kubwa ya watu wakilipwa. Wengi wameanza kuondoa mali zao, na wale wenye majengo wanabomoa wenyewe ili kuokoa vifaa vyao kwa matumizi mengine,” alisema Makau. Mradi huo umegawanywa katika sehemu mbili, ambapo sehemu ya kwanza inahusisha kipande cha Daraja la Nyali hadi Daraja la Mtwapa, huku sehemu ya pili ikiwa Mtwapa-Kwa Kadzengo-Kilifi na kila sehemu inagharimu takriban Sh7.5 bilioni. Mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Kenya kwa gharama ya jumla ya Sh15 bilioni unalenga kuboresha usafiri wa kikanda, kukuza biashara na kuimarisha sekta ya utalii utakapokamilika. AfDB inafadhili asilimia 70 ya mradi huo wa ukanda wa pwani, huku Serikali za Kenya na Tanzania zikichangia asilimia 30 iliyosalia. Mradi huo pia unatarajiwa kupunguza muda wa safari, kurahisisha usafiri wa mpaka, kuimarisha biashara kati ya mataifa, na kufungua maeneo ya utalii sambamba na kuunganisha bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mombasa. Sehemu ya pili ya mradi huo sasa imekamilika kwa asilimia 75 na inatarajiwa kukamilika kikamilifu Machi 2027, baada ya kucheleweshwa hapo awali kutokana na changamoto za fidia na ununuzi wa ardhi.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.