“VIJANA wengi wanapofuzu kutoka vyuoni humu nchini, maombi yao huwa ni wapate kazi katika nyanja walizozisomea ndiposa wakubali kuwa wamepata ufanisi katika masomo yao. Ni nadra sana kuwakuta wahitimu kutoka vyuo vikuu, wakijishughulisha na kilimo kama njia moja ya kujikwamua kiuchumi wanapozisubiria kazi hizo. Lakini hali ni tofauti kwa Caleb Matundura, 27, ambaye ameamua kuzamia kilimo cha zao la maparachichi kama njia moja ya kujiendeleza na kujichumia riziki yake ya kila siku katika Kaunti ya Kisii. Jarida la Akilimali lilimzuru mhitimu huyo wa Shahada ya Fedha kutoka Chuo Kikuu cha Cooperative nyumbani kwao kijijini Kegati, eneobunge la Nyaribari Chache, Kisii kujionea alivyojiendeleza katika ukulima wa maparachichi ya Hass. Amekuwa akijihusisha na kilimo cha maparachichi hayo ya kisasa tangu mwaka wa 2017 alipokuwa mwanafunzi wa shule ya upili. “Nilianza kupanda maparachichi ya Hass miaka tisa iliyopita nilipokuwa katika shule ya upili. Nilianza na miti 20 lakini sasa nina zaidi ya miti 300 katika kipande maalumu shambani mwetu. Nilivutiwa na kilimo hicho kutokana na tija yake ambayo wakulima wengine walikuwa wakipata kutoka maeneo mengine,” Matundura anasema. “Nilinunua miche ya parachichi hizo kutoka kwa Idara ya Kilimo na nyingine kutoka kwa mkulima wa hapa karibu aliyekuwa ameiotesha katika kitalu chake. Nilichimba mashimo ya futi 2 kwa 2 na kutenganisha miche yangu kwa upana wa mita 6 kwa 6,” anaongeza Matundura. Alichanganya mbolea na udongo wa juu na baada ya mwezi mmoja, miche yake ilistawi kwa kuwa eneo hilo linapokea mvua nyingi kwa mwaka mzima. Baada ya miaka miwili, Matundura anahoji kuwa miparachichi yake ilianza kuzaa matunda. Kwa kuwa wakati huo hakuwa amelielewa soko vizuri, Matundura alisema aliuza matunda yake kwa madalali. “Niliuza matunda yangu kwenye soko la humu nchini kwa madalali kwani sikuwa nimelifahamu soko vyema,” barobaro huyo alihoji huku akiongeza kuwa kadri siku zilipozidi kusonga, uzalishaji wake ulizidi kuongezeka. Matundura sasa ana uwezo wa kuzalisha zaidi ya kilo 1,000 za maparachichi kutoka kwa shamba lake na anauza matunda yake moja kwa moja kwa kampuni zinazonunua maparachichi hayo Ughaibuni. Yeye huuza tunda moja kwa kati ya Sh15 na Sh20 kulingana na ukubwa na ubora wake au kwa kilo. Baada ya kampuni kununua matunda, mabaki hutumiwa kwa matumizi ya nyumbani. Matundura anaeleza kuwa maparachichi aina ya Hass yana soko bora ikilinganishwa na aina nyingine za maparachichi. Anaongeza kwamba matunda ya Hass yanaweza kukaa muda mrefu baada ya kuchumwa ikilinganishwa na yale ya kawaida. Kwa kuwa bado hajapata kazi aliyoisomea, Matundura anasema analenga kupanua kilimo chake cha maparachichi hata zaidi. “Katika siku zijazo, ninapanga kupanua sehemu yangu ya ardhi hadi ekari moja, asema Matundura ambaye ametoa wito kwa wakulima wengine hasa vijana kujitosa katika kilimo cha maparachichi." Mwaka uliopita, uzalishaji ulikuwa mzuri ambapo anasema ulichangiwa na mvua ya kutosha. Anaona kuwa hilo huenda likajirudia tena mwaka huu kwani mvua hiyo ingali inaendelea. Mapato “Kutokana na miti kati ya 17 na 22 ya maparachichi, nilipata zaidi ya Sh100, 000 kwa mauzo, ambayo ilikuwa ya juu zaidi kuwahi kupata tangu nianze ukulima wa matunda haya,” Matundura anaeleza. Kulingana naye, maparachichi ya Hass yanaweza yakavunwa mara mbili kwa mwaka kutegemea msimu. Kila mwaka, yeye huvuna maparachichi kati ya Februari hadi Juni na kuwauzia wafanyabiashara wadogo wadogo au baadhi ya kampuni zinazouza maparachichi au bidhaa kutokana na zao hili katika nchi za kigeni. Kila mti wa parachichi unaweza toa matunda kati ya 500 na 600 huku idadi hii ikiongezeka hadi matunda 1,000 kadri yanavyoendelea kukua. Anawataka wakulima kutumia samadi na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu ili kuwa na kilimo endelevu. Yeye huhudhuria semina na vikao vingine vya siku ya shambani ili kupata ujuzi zaidi kutoka kwa wataalamu wa kilimo na maafisa wa nyanjani wanaotembelea mashamba yao. Anatoa wito kwa wakulima kuunda vikundi kwani vitawasaidia kupata masoko bora badala ya kutafuta kama mtu binafsi. Pia anarai serikali ya kitaifa na kaunti kutoa mafunzo na warsha kwa wakulima ili kuwaelimisha kuhusu mbinu bora za kilimo, tiba, wadudu na udhibiti wa magonjwa. Kulingana na Matundura, kilimo cha parachchi kina faida na huwa kinamwezesha kupata riziki yake ya kila siku kwani shughuli za kilimo kwake ni sawa na ajira rasmi. Ni kutokana na maparachichi ambapo Matundura anamiliki duka la kuuza bidhaa za ujenzi na bidhaa za nyumbani kijijini kwao. Anaeleza kuwa kilimo cha parachichi hakihitaji muda mwingi wa kuwa shambani kwani mmea unapokomaa, mkulima huhitajika tu kupalilia na kutilia dawa mimea yake ili kuitunza ipasavyo. Baadhi ya changamoto anazokumbana nazo ni pamoja na bei ya chini ya maparachichi anapowauzia wafanyabiashara wadogowadogo ambao hununua kwa bei ya chini ilhali wanapofikisha mazao haya sokoni, hupata faida kubwa kwa kuwauzia wateja kwa bei ghali zaidi. Mbali na magonjwa ya kila sampuli hasa yanayotokana na kiangazi au baridi kali kupita kiasi, changamoto nyingine ni mvua ya mawe inayoharibu matunda au kuoza kwa maparachichi iwapo soko litakosekana baada ya zao kukomaa shambani. Ushauri wake ni pawepo na mipango maalum kutoka kwa serikali za ngazi zote ili kutafuta masoko ya kigeni ili wakulima wa parachichi wafaidike zaidi. “Wakulima wengi wa parachichi hawana ujuzi mwingi wa teknolojia ya kisasa inayohitajika kuboresha au kuongeza mazao yao. Hivyo basi, litakuwa jambo la busara kwa wakulima kuelimishwa na maafisa wa kilimo wa serikali,” Matundura anasema.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
