skipToContent
🌐All

KINAYA: Ulichagua ‘kitu’ kikakuramba, sasa utachagua mtu?

KINAYA: Ulichagua ‘kitu’ kikakuramba, sasa utachagua mtu?
HIVI ulichagua nini kukuwakilisha bungeni? Nimeuliza ‘nini’, wala si ‘nani’, kwa kuwa Wakenya wengi walichagua vitu, si watu. Naam, yaani vitu vilivyopo tu, visivyo na dalili ya kuwa hai. Ni ‘kitu’ mtu anayefumba macho na kuunga mkono mpango wa serikali kulipia wanafunzi Sh95 pekee kwa muhula mzima! Ni ‘kitu’ mtu anayehongwa ili mambo yasiyo na tija yapitishwe bungeni. Atakuwa ni ‘kitu’ mbunge ambaye atakubali ombi la Wizara ya Usalama la Sh20 bilioni za kufunza polisi na kuwanunulia silaha nzito ili watuponde vichwa wakati wa kampeni za 2027. Kumbuka hiyo ndiyo wizara iliyo na ukiritimba wa kutumia nguvu dhidi yako, na ukiishtaki mahakamani ikukumbushe ndiyo mlinzi mkuu wa serikali. Ukicheza ikung’oe meno na kukwambia ukaishtaki, na ukizidi ikupe msimbo wa jina ‘adui wa taifa’. Mtu anayewapa wanafunzi Sh95, kisha akampa polisi Sh20 bilioni ili kutupiga tukiandamana hafai kuitwa mtu wala kiongozi, ni ‘kitu’. Mara hii hatupaswi kuchagua vitu kabisa! Labda ikiwa sisi wenyewe ni vitu. Hata tukiwa vitu hatuwezi kuaminia vitu vyenzetu maisha yetu kwani vitatuangamiza na kuangua vicheko vya kishetani. Kenya ni yetu sote, tuna haki ya kuamua tunataka kuongozwa vipi. Pia ni jukumu letu. Kwa bahati mbaya, wengi wetu tulichagua vitu tukidhani ni watu, kumbe vitu havijui utu! Kati ya sasa na Agosti 2027 tunamuomba Mungu atulinde dhidi ya vitu tulivyojichagulia wenyewe, visituangamize kabla kuvifagilia mbali, atupe na hekima ya kuchagua watu wenye utu na akili timamu. Baadhi ya vitu tulivyochagua vilisema kuwa vilitia saini Mswada wa Fedha wa 2024 kabla kuusoma, kufumba na kufumbua mswada wenyewe ukasababisha vijana wa Gen-Z wamwagike barabarani, wakauawa kwa mamia au maelfu. Mara hii, ikiwa wewe si kitu, na uzuzu haujakukolea, hakikisha umemfuta kazi mbunge yeyote aliyeunga mkono Mswada wa Fedha wa 2024. Damu ya vijana wetu ina thamani kubwa, haifai kumwagwa kama ya kondoo. Wala asikudanganye eti amejirekebisha, akawa mweupe kama pamba, eti tusahau yaliyopita. Nyoka pia hujitoa ngozi zee akaonekana kiumbe kipya, ila meno yake yakasalia makali, akikung’ata utafuata njia ya marahaba usipokimbia spitali kuangalia iwapo bima mpya ya SHA itakufaa. Ikiwa mbunge wako alitoweka mashinani baada tu ya kumchagua miaka minne iliyopita, na sasa ameanza kuhudhuria sherehe zote za mazishi na harusi, mkimbie kama jini. Huyo ni nyoka na ngozi yake mpya, anakunyemelea akung’ate tena! Hata hivyo, ikiwa hujali kung’atwa kiholela, tia kidole chako kinywani mwake, umpapase na ulimi, kisha urejee hapa kunipa ripoti kamili. -Douglas Mutua ni mwanahabari Mkenya anayeishi Amerika (mutua_muema@yahoo.com)
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.