“VIONGOZI wa Linda Mwananchi ndani ya ODM wametoa makataa makali kabla ya kuridhiana na wenzao wa Linda Ground inayoongozwa na Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga. Linda Mwananchi inaongozwa na Gavana wa Siaya James Orengo na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna. Wamesema hawataridhiana na mrengo wa Dkt Oginga hadi maamuzi ya kisiasa ambayo yalifanywa baada ya mauti ya marehemu Raila Odinga, yabatilishwe. Pia yanataka kusitishwa kwa mazungumzo kati ya ODM na UDA na kutekelezwa kikamilifu kwa ajenda 10 zilizokuwa sehemu ya makubaliano kati ya marehemu Bw Odinga na Rais William Ruto. Mrengo huo ulitoa masharti hayo baada ya Gavana wa Kisii Simba Arati kuwaambia watathmini kurejea nyumbani. Bw Arati aliyatoa matamshi hayo siku ya kwanza ya warsha ya siku tatu ya ODM Pwani ambayo ilifanyika chama hicho kikiendelea kukumbwa na misukosuko ya kisiasa. Ombi la Linda Ground kwa Linda Mwananchi linakuja siku chache baada ya wabunge Millie Odhiambo (Suba Kaskazini) na Dkt Otiende Amollo (Rarieda) kudai kuwa hatua ya kumfukuza Bw Sifuna haikufaa. “Kabla ya Mkutano wa Baraza Kuu la Chama, nilikutana na Dkt Oburu na kumwonya kuwa hatua hiyo ingevunja chama. Nilimwaambia hakungekuwa na chochote cha kutunufaisha,” akasema Dkt Amollo. Jana, Dkt Oginga aliwakumbusha wanachama wa ODM kuwa lazima walinde chama hicho. Mwenyewe hakuhudhuria kongamano hilo huku hotuba yake ikisomwa na Bw Arati. “Lazima tuwe waaminifu kwa chama na tuyakomeshe malumbano ya ndani kwa ndani kwa sababu yatasambaratisha chama,” akasema Dkt Oginga. Alisisitiza kuwa wakizungumza na UDA, umoja unahitajika kwa sababu tofauti hizo za kisiasa zinayumbisha chama hicho. Aidha Dkt Oginga alisisitiza kuwa makubaliano yoyote yataidhinishwa na ngazi zote za chama huku akifichua kutakuwa na misururu ya shughuli za kupiga chama jeki. “Hatujaanza mazungumzo na UDA na naomba tukianza tumakinike, tuwe na umoja na nguvu ili mchakato huo ufaulu,” akaongeza. Naibu Katibu Mkuu wa ODM Catherine Omanyo alisema kuwa sasa wanalenga siasa kuunda serikali na kuendeleza ndoto ya marehemu Raila ambaye aliwaacha ndani ya Serikali Jumuishi.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
