skipToContent
🌐All

Mafuta ya Turkana yazua tofauti kali za kisiasa kati ya viongozi

Taifa Leo (Swahili) Global
Mafuta ya Turkana yazua tofauti kali za kisiasa kati ya viongozi
KUREJELEWA kwa shughuli za uchimbaji mafuta kumeanza kuibua tofauti kali za kisiasa Turkana Mashariki na Turkana Kusini, baadhi ya wanasiasa wanaosaka viti wakijitokeza na kujisawiri kama wanaopambania jamii. Utata umezuka jinsi ambavyo nafasi za kazi zitakavyosambazwa kwa usawa pamoja na nafasi za kibiashara. Isitoshe, kuna tofauti kuhusu mapato kwenye Mradi wa mafuta wa South Lokichar ambao unatarajiwa kugawanywa kwa usawa kwa jamii ya eneo hilo. Kampuni ya Kawi ya Gulf ndiyo itasimamia uchimbaji wa mafuta katika mradi huo kutoka kwa Kampuni ya mafuta ya Tullow iliyofanya kazi hiyo awali. Wakazi wa Aroo wameanza kulia kuwa hawatanufaika baada ya Mbunge wa Turkana Mashariki Nicholas Ngikor kudai kuwa nafasi zitakazojitokeza zitakuwa za wakazi wanaoishi karibu na maeneo ambako uchimbaji mafuta utaendelea. “Mimi natoka wadi ya Katili ambayo ni mbali na South Lokichar Basin. Tunahitaji viongozi ambao watahakikisha kuwa asilimia tano pia itatunufaisha kwa sababu hapo awali tulikuwa sehemu ya eneobunge la Turkana Kusini,” akasema mkazi Peter Nakauron. Diwani wa Wadi ya Lokichar Samwel Lomodo alisema mwongozo wa maendeleo ambao umepewa kampuni ya kawi ya Gulf hauna uwazi kuhusu nafasi za ajira na ushirikishaji wa umma. Hata hivyo, alikiri kuwa kuna baadhi ya wanasiasa wameanza kuzua uhasama na kuchochea jamii zinazoishi Turkana Mashariki na Kusini kuhusu manufaa yanayotarajiwa katika mradi huo. “Maendeleo yatakayotokana na mafuta hayo yanastahili kuwaunganisha raia, kuhakikisha usawa na pia kuwa wote wananufaika kutokana na nafasi zilizopo. Baadhi ya viongozi wanawagawanya raia ili kunufaika kisiasa,” akasema Bw Lomodo. Muungano wa Wasomi kutoka Lochakula/Kochodin ukiongozwa na Samwel Ariong nao ulishutumu wanasiasa kwa kutumia udhaifu wa kijamii kuhakikisha wao ndio wananufaika na mafuta ya eneo hilo. “Tutahakikisha kuwa tunawaunganisha wasomi kutoka kwa vijiji karibu na maeneo ya uchimbaji mafuta. Hii itahakikisha wanapata nafasi za ajira na pia wananufaikia tenda huku wakiimarisha maisha yao na pia kunufaika kimaendeleo,” akasema Bw Ariong. Aliyekuwa Mbunge wa Turkana Ali Lokiru naye aliwashutumu baadhi ya wanasiasa kwa kuanza kuwapendelea washirika wao kuhusu mradi wa uchimbaji wa mafuta. “Baadhi ya viongozi waliochaguliwa sasa wanatumia nafasi zao na kuwatenga wenyeji na washindani wao wa kisiasa kuhusu masuala muhimu yanayohusiana na uchimbaji wa mafuta. Tunataka mwekezaji mpya awe na uwazi katika kuwasiliana na jamii,” akasema Bw Lokiru. Pia tofauti kuhusu umiliki wa ardhi na uhasama wa kisiasa kati ya Governor wa zamani Joseph Nanok na aliyekuwa Waziri wa Kawi John Munyes umetajwa kama kikwazo kikuu kuhusu kufaulu kwa mradi wa uchimbaji wa mafuta Turkana.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.