skipToContent
🌐All

Magavana saba vitani kuondoa laana ya ‘Wantam’ iliyokumba watangulizi

Magavana saba vitani kuondoa laana ya ‘Wantam’ iliyokumba watangulizi
WALIKUWA miongoni mwa walionufaika na kile kinachoitwa “laana ya muhula mmoja wa ugavana” walipoingia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2022. Lakini sasa, takribani miezi 14 kabla ya uchaguzi wa 2027, magavana saba wanakabiliwa na presha kubwa na huenda wakawa waathiriwa wa mtindo huohuo wa kisiasa. Tangu uchaguzi wa 2013, wapigakura katika kaunti za Nairobi, Kiambu, Nakuru, Meru, Taita Taveta, Nyandarua na Isiolo hawajawahi kuwachagua tena magavana wao kwa muhula wa pili. Kaunti kama Nairobi, Kiambu na Meru zimekuwa na rekodi ya kuwa na magavana wanne tofauti kutokana na mizozo ya kisiasa na kuondolewa madarakani kwa Mike Sonko, Ferdinand Waititu na Kawira Mwangaza mtawalia. Katika mazingira ya sasa ya mabadiliko makubwa ya miungano ya kisiasa, wanasiasa kadhaa; ikiwemo wabunge wa sasa na magavana wa zamani, wameanza kupanga mikakati ya kunufaika na mtindo huo. Katika kaunti ya Nakuru, Gavana Susan Kihika ametoa wito kwa wapigakura kukomesha mtindo huo, akisema unakwamisha maendeleo ya kaunti. Gavana wa kwanza wa Nakuru, Kinuthia Mbugua, alishindwa kutetea kiti chake mwaka 2017 dhidi ya Lee Kinyanjui. Kinyanjui naye, ambaye sasa ni Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda katika serikali ya Rais William Ruto, pia alishindwa katika uchaguzi 2022. Awali, uteuzi wa Kinyanjui serikalini ulionekana kama nafuu kwa Kihika kupata muhula wa pili, kwa kuwa wote wangekuwa upande wa Kenya Kwanza. Hata hivyo, kauli za Kinyanjui zimeacha maswali, akitoa ujumbe wenye mafumbo unaoashiria huenda naye akagombea. “Tai anabaki kimya, lakini baadaye hurudi akiwa amepata nguvu mpya,” alisema. Kwa sasa, Seneta Tabitha Karanja ndiye mpinzani mkuu wa Kihika, ikitarajiwa huenda akagombea ugavana, ingawa bado hajatangaza tiketi atakayotumia. Katika kaunti ya Nairobi, Gavana Johnson Sakaja anakumbwa na shinikizo kubwa kuvunja laana ya muhula mmoja, huku akipokea mashambulizi kutoka kwa Chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na Gachagua pamoja na kundi la ODM la Linda Mwananchi lililomtaja Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kama mgombea wao wa ugavana. Mbunge James Gakuya naye ameonyesha nia kupitia DCP. Katika UDA, Sakaja anatarajiwa kukabiliana na aliyekuwa gavana wa kwanza wa Nairobi Evans Kidero, ambaye amekuwa akijipanga kurejea. Wapinzani wake, akiwemo Babu Owino na James Gakuya, wanamshutumu Sakaja kwa kudorora kwa huduma za jiji. “Hilo la muhula mmoja ni sauti ya wananchi wanaotaka uwajibikaji,” alisema Gakuya. Kiambu, Meru, Nyandarua, Taita Taveta na Isiolo nazo zimeshuhudia mzunguko wa mabadiliko ya uongozi, unaoweka magavana wa sasa chini ya presha kubwa kuelekea 2027.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.