skipToContent
🌐All

Mahakama yapiga mhuri mkataba wa Ruto na Trump uliozua hofu ya data za Wakenya

Mahakama yapiga mhuri mkataba wa Ruto na Trump uliozua hofu ya data za Wakenya
MAHAKAMA ya Rufaa imeondoa agizo lililozuia Kenya kutekeleza mfumo wa ushirikiano wa afya wa thamani ya mabilioni ya pesa kati ya Kenya na Amerika uliotiwa saini jijini Washington, Amerika mnamo Desemba 2025. Jopo la majaji watatu liliondoa agizo hilo ambalo lilikuwa limesimamisha utekelezaji wa makubaliano hayo hadi kesi itakaposikizwa Oktoba 30, 2026. Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor pamoja na Wizara ya Afya waliambia mahakama kuwa kusimamishwa kwa makubaliano hayo kulisababisha pengo kubwa katika sekta ya afya, hasa wakati ambapo magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi, kifua kikuu na malaria yanaendelea kuongezeka. Serikali ilisema mfumo huo uliundwa kusaidia Kenya kutimiza wajibu wake wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na kusaidia kupambana na Ukimwi, malaria, kifua kikuu pamoja na magonjwa mengine ya kuambukiza. Kupitia makubaliano hayo, serikali ya Amerika imejitolea kutoa Dola bilioni 1.6 kwa kipindi cha miaka mitano kusaidia sekta ya afya nchini Kenya. Fedha hizo zitatumika kununua vifaa vya matibabu, kuongeza dawa hospitalini, kuajiri wahudumu wa afya na kupanua huduma za bima ya afya. Makubaliano hayo yalikuwa yamepingwa kortini na Seneta wa Busia, Okiya Omtatah aliyedai kuwa yalikiuka Katiba kwa kutopata ushirikishaji wa umma na idhini ya Bunge. Shirika la watumiaji nchini (COFEK), pia lilionyesha wasiwasi kuhusu uwezekano wa data za afya za Wakenya kuvuja au kutumiwa vibaya nje ya nchi. Hata hivyo, serikali ilihakikishia wananchi kuwa hakuna taarifa binafsi zitakazotolewa. Mwanasheria Mkuu alisema data zitakazotolewa zitakuwa za jumla tu na haziwezi kumtambulisha mtu binafsi. “Serikali haitatoa data nyeti za wananchi bali taarifa za jumla zinazohitajika kutekeleza mfumo huo wa ushirikiano,” ilisema serikali kupitia stakabadhi za mahakama. Cofek ilionya kuwa mara data za kiafya za Wakenya zitakapotumwa nje ya nchi, itakuwa vigumu kuzidhibiti au kuzirejesha iwapo zitatumiwa vibaya.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.