skipToContent
🌐All

MALUMBANO: Wanga amjibu Orengo, ataka wanasiasa wa kike waheshimiwe

Taifa Leo (Swahili) Global
MALUMBANO: Wanga amjibu Orengo, ataka wanasiasa wa kike waheshimiwe
GAVANA wa Kaunti ya Homa Bay, Gladys Nyasuna Wanga, amemjibu mwenzake wa Siaya James Orengo kufuatia kauli alizomwelekezea ambazo zimekosolewa vikali. Katika barua ya wazi aliyomwandikia Bw Orengo, Bi Wanga ambaye ni mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha ODM alitoa wito wa kuheshimiwa kwa wanawake viongozi, akisisitiza kuwa kukosolewa kisiasa hakupaswi kuvuka mipaka na kuwa chanzo cha kudhalilisha au kupunguza utu wa wanawake. Katika barua hiyo, Bi Wanga amesema aliamua kuiandika baada ya kutafakari kauli zilizotolewa dhidi yake, akieleza kuwa zilimuumiza licha ya kuwa amekuwa akiheshimu viongozi wa kizazi cha zamani kama Orengo. “Nilichagua ukimya mwanzoni kwa sababu si kila tofauti inahitaji majibizano hadharani. Hata hivyo, kuna wakati ukimya hauwezi kubeba uzito wa maumivu,” alisema Wanga katika barua hiyo. Gavana huyo amesema amekuwa akimheshimu Orengo kama kiongozi mkongwe na mfano wa ujasiri katika siasa za nchi, akimchukulia kama mlezi wa kisiasa kwa viongozi wengi vijana waliokuja baada yake. Hata hivyo, alisema kauli zilizotolewa zilimfanya atafakari jinsi maneno ya viongozi yanaweza kuathiri wanawake wanaoshikilia nyadhifa za umma, akieleza kuwa yanaweza kuimarisha au kuvunja heshima yao katika jamii. Wanga alisisitiza kuwa wanawake wengi katika jamii bado wanakumbana na changamoto za kupuuzwa na kudhalilishwa katika uongozi, hali ambayo amesema inahitaji kubadilishwa kupitia uongozi wenye heshima na usawa. “Heshima na uongozi wa kweli hauhitaji kudhalilisha wengine,” alisema. Wanga hata hivyo amesema bado anamheshimu Orengo kama kiongozi na mzee , akiongeza kuwa anachagua kusamehe na kufungua mlango wa mazungumzo na ushirikiano katika masuala ya maendeleo.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.