skipToContent
🌐All

MAONI: Asasi ya urais isifanywe kama mkeka wa kuchezewa na raia

MAONI: Asasi ya urais isifanywe kama mkeka wa kuchezewa na raia
JUMAPILI iliyopita katika ibada ya shukran ya katibu katika Wizara ya Vijana Fikirini Jacobs Bamba Kilifi, kisa kilichotokea katika hafla hiyo kinatakiwa kuchukuliwa kwa uzito na kisirudiwe tena. Kijana alichomoka ghafla kutoka kwa umati na kumshika mabegani Rais Ruto. Kwa watazamaji wa mtandaoni, baadhi walishika roho mikononi. Rais wa Jamhuri ya Kenya ambaye pia ni amiri jeshi mkuu wa Kenya anasogelewa na raia bila haya wala soni. Walinzi wa Rais waliamka kama waliopigwa na radi. Wakamwinua kijana wa Kichonyi kihobelahobela. Rais akawakanya pupa. Kijana wa watu wanasema “alifinywa” baadaye, wapi ni suala la mjadala. Hotuba ya Rais Ruto ikavurugika kiasi. Wakosoaji wa Ruto wakasema ni kiki jinsi wanavyotaja vijana wa mitaani. Kwangu, asasi ya Urais haitakiwi kufanywa kama mkeka wa kuchezewa na watu. Inahitaji heshima kubwa kwa watu wa wantam na wenzao wa tutam. Urais si sebule ya wageni kuingia wakati wanaotaka na kufanya yanayowapendeza. Ni kiungo muhimu katika Jamhuri ya Kenya. Haitoshi mkuu wa polisi Douglas Kanja kutangaza kuwa kikosi kilichokuwa kikimlinda Rais kimevunjiliwa mbali na kingine kubuniwa. Si kwa faida yetu Naibu Mkuu wa polisi Eliud Lagat kutoa orodha ya maafisa wapya na kueleza wanakotoka na wanakoenda. Hoja ya usalama wa Rais. Kisa kama hiki kilitokea Wajir. Kabla ya hapo, kuna bwana mmoja alimrushia Rais Ruto kiatu katika kaunti ya Migori. Rais anaweza kutaka kukaribiana na hadhira yake kila wakati lakini hili linaweza kumponza na kuitia nchi katika taharuki kubwa ya ghafla. Yeye ni Rais wa nchi si wa UDA ambao wanataka kumkaribia kumsalimia katika mikutano ya hadhara na dharura. Washauri wa Rais wa usalama wamelala usingizi kwa muda mrefu, atakayewaamsha ni tukio ambalo halitakuwa ajali bali msiba wa kujitakia. Kuna mifano kadhaa ya vituko kama hivi ambavyo serikali ya Rais Ruto haswa Wizara ya Usalama isipochukua tahadhari huenda yatukie makubwa ya kutisha. Nchi zenye uwezo wa ulinzi na uchumi kama vile Marekani zimekuwa zikiwalinda Marais wao lakini kosa dogo tu limekuwa likiathiri mambo. Rais wa 35 wa Marekani J.F Kennedy alipigwa risasi mnamo 1963 na kufariki, mwenzake wa 40 Ronald Reagan alipigwa risasi 1981. Papa Mtakatifu John Paul wa pili akiwa kiongozi wa Kanisa Katoliki 1981 alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya alipokuwa akiingia kanisani St Peters Square. Alijeruhiwa vibaya japo alinusurika kifo. Sijawa mtabiri wa matukio mabaya kama hayo Kenya lakini inaweza kutukia tusipomlinda Rais kama mboni za macho yetu kiusalama. Paul Naibiswa ni mhariri NTV
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.