“KWA miaka 22 mashabiki wa Arsenal walivumilia dhihaka, uchungu, maumivu, mateso na kila aina ya nui katika Ligi Kuu Uingereza (EPL). Hakuna shabiki wa Arsenal ambaye alikuwa na amani kila baada ya msimu kukamilika. Ilibidi wayazoee majina kama ‘pacesetters’, ‘bottlers’ na majina mengine ya dhihaka na ajabu kutoka kwa mashabiki wa timu pinzani. Msimu ukianza mnamo Agosti, Arsenal ilikuwa ikiongoza EPL lakini ikifika Aprili ilikuwa ikiporomoka na kupitwa na wapinzani ambao mwishowe walikuwa wakishinda EPL. Katika misimu mitatu iliyopita, walifanya hivyo na Liverpool na Manchester City wakatwaa EPL. Hata hivyo, mara hii mambo yamebadilika na kuwanyonyokea Arsenal, wamewahi EPL ikiwa imesalia mechi moja kabla ya msimu kukunja jamvi. Bournemouth iliagana sare ya 1-1 na Manchester City mnamo Jumanne usiku na kuwapa Arsenal ubingwa. Kwa mashabiki ambao hawakubanduka klabuni, wakasononeka, wakavumilia kejeli na matusi, huu mwaka wamefika ‘Canaan’ ardhi ya maziwa na asali. [caption id="attachment_188322" align="alignnone" width="2000"] Mshambuliaji wa Arsenal Viktor Gyokeres akisherehekea kufunga bao dhidi ya Leeds United mechi ya EPL uwanjani Emirates mnamo Agosti 23, 2025. PICHA | REUTERS[/caption] Katika uga wa Emirates Kaskazini mwa London, mashabiki wakiongozwa na mchezaji wa zamani Ian Wright walikusanyika na kusherehekea taji jipya hata kabla hawajakabidhiwa. Kocha Mikel Arteta, 44 ambaye ni mchezaji wa zamani wa Arsenal, Mhispania kutoka San Sebastian ndiye ameipa Arsenal atasalia kwenye kumbukumbu kwa kuwaongoza kushinda EPL. Wengi wa wachezaji wa sasa kambini mwa Arsenal aidha walikuwa wadogo au hawakuwa wamezaliwa klabu hiyo iliposhinda ubingwa wa EPL mara ya mwisho 2003/2004 bila kushindwa. Kati ya wanasoka hao ni winga Bukayo Sako ambaye nguzo kwa The Gunners na Three Lions. “Tumeandikisha historia pamoja. Najivunia kila mtu ndani ya timu hii na tusherehekee ushindi huu kwa sababu ni bidii na juhudi zetu,” akasema Arteta. Hakika miaka 22 ni muda mrefu zaidi kusubiri kitu. Muda huu unatosha kwa mtoto kuzaliwa, kusoma hadi amalize shule na hata baadhi wameishia kuingia ndoa na kuwapata watoto. Kila mara baada ya msimu, mashabiki wa Arsenal walikuwa wakijifariji kwa kauli ‘si matokeo yaliyotarajiwa’ ama ‘msimu ujao tutashinda’ Hata hivyo, baada kuwahi ubingwa Jumanne usiku, wengi waliamkia maamkizi ya ‘sisi ni mabingwa’. Salamu hii ilitawala kote mitandaoni iwe Facebook, X, TikTok, Instagram na makundi ya WhatsApp. Yaani kila mahali mashabiki wa Arsenal walikuwa wakisalimiana hivyo. Kimataifa wanasiasa wa hadhi hawakuficha furaha yao kutokana na jinsi ambavyo wanashabikia The Gunners. “Miaka 22 lakini sasa sisi ni mabingwa,” akaandika Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer. Hata hivyo, baadhi ya mashabiki walimkabili vikali kutokana na siasa za Uingereza. “Hukuwa uwanjani,” akaandika na raia mmoja. “Sote tumeamua huwezi kushabikia Arsenal,” mwengine akamwaandikia. Kwa mashabiki wengi wa Arsenal, bado hawajatosheka. Sasa wanalenga ushindi mnamo Mei 30 katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ambapo watakuwa wakicheza dhidi ya PSG jijini Budapest, Hungary. Itakumbukwa Arsenal iliyokuwa na wachezaji 10 ilipoteza 2-1 dhidi ya Barcelona katika fainali iliyosakatwa Paris mnamo 2006.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
