“KIONGOZI wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua yuko Uingereza kwa ziara ya mwezi mmoja inayolenga kutafuta angalau Sh1 bilioni za kufadhili maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2027. Bw Gachagua alisema fedha hizo zitasaidia chama chake kugharimia shughuli za mchujo wa wawaniaji na kampeni za uchaguzi, huku akisisitiza kuwa anataka DCP ijitegemee kifedha ili kuepuka ushawishi kutoka kwa wanaotaka tiketi za kisiasa. “Bajeti ya uchaguzi wa mchujo pekee ni Sh2 bilioni. Natarajia ada za wanaowania nafasi zitachangia nusu ya fedha hizo, na sasa ninaenda Uingereza kuimarisha juhudi za kuchangisha ili kufikia 2027 tuwe tayari,” alisema. Ziara hiyo imeibua maswali ya kisiasa kuhusu watu ambao Gachagua atakutana nao nje ya nchi, hasa kutokana na msimamo wake wa kuongoza kampeni za kuondoa serikali ya Rais William Ruto mamlakani mwaka 2027. Gachagua alisema anataka kuhakikisha chama chake hakitegemei fedha za wawaniaji kwa njia inayoweza kuathiri haki na uwazi wa kura za mchujo. “Sitaki hali ambapo ukosefu wa fedha unafanya chama kishinikizwe na wawaniaji. Watu wanaweza kusaidia chama kununua magari ya kampeni na vifaa vingine, lakini si kwa masharti ya kupewa tiketi,” alisema. Alionya kuwa vyama visivyo na fedha vya kutosha mara nyingi hujikuta vikitoa tiketi kwa watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha badala ya wale wanaoungwa mkono na wananchi. Katika mazingira ambayo mara nyingi kumekuwa na madai ya ushawishi wa mataifa ya nje katika siasa za Kenya, wachambuzi wanasema serikali itakuwa makini kufuatilia ziara hiyo ya Gachagua na watu atakaokutana nao. Aliyekuwa balozi wa Kenya nchini Ujerumani Kirore Mwaura alisema uchaguzi mkuu wowote duniani huvutia maslahi ya ndani na nje ya nchi. “Kuna maslahi ya kimataifa katika chaguzi nyingi duniani na Kenya si tofauti. Serikali huwa makini kufuatilia mienendo hiyo kama tahadhari,” alisema. Hii ni mara ya pili kwa Gachagua kusafiri nje ya nchi tangu alipoondolewa mamlakani kama Naibu Rais mwaka 2024. Kati ya Julai na Agosti mwaka 2025, alifanya ziara nchini Amerika ambako alikutana na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i pamoja na Wakenya wanaoishi ughaibuni. Katika ziara hiyo ya Amerika, Gachagua alifanya mikutano katika majimbo mbalimbali huku akijaribu kuimarisha ushawishi wa upinzani kuelekea uchaguzi wa 2027. Katika safari hii mpya, hakutaja moja kwa moja watu atakaokutana nao lakini alisema atashirikiana na “washirika na marafiki wa safari ya ukombozi.” Ziara yake imejiri huku kampeni za uchaguzi mdogo wa Ol Kalou zikishika kasi. DCP inamuunga mkono Kamau Ngotho huku chama tawala cha UDA kikimfadhili Simon Nyagah. Baadhi ya wachambuzi wanasema kuondoka kwake wakati huu kama mtihani kwa upinzani, hasa baada ya Gachagua kujijenga kama sauti kuu ya upinzani na mvumbuzi wa kauli mbiu ya “Wantam”. Hata hivyo, Gachagua amesema ameacha viongozi wake wa kisiasa kusimamia kampeni hizo akiwa nje ya nchi. Pia alisema atarejea nchini kwa muda katikati ya Juni kabla ya kusafiri tena kwenda Amerika kwa ziara nyingine ya kuchangisha fedha. Wachambuzi wanaamini safari hiyo inaonyesha jinsi mapambano ya kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027 yanavyoanza mapema huku vyama vikijipanga kifedha na kisiasa.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
