skipToContent
🌐All

Matapeli wa ardhi wanyima wakazi wa Mavoko usingizi

Matapeli wa ardhi wanyima wakazi wa Mavoko usingizi
KILA siku katika eneo la Mavoko, Kaunti ya Machakos, kuna mtu anayekumbwa na hatari ya kupoteza ardhi yake; si kwa nguvu za silaha bali kwa karatasi na hila ofisini. Kughushi saini, kubadilishwa kwa rekodi katika sajili ya ardhi au hatimiliki yenye utata mara nyingi hutosha kufuta uwekezaji wa miaka mingi. Kuanzia maeneo ya Stone Athi, Athi River hadi Mlolongo na Katani, eneo hili linalostawi kwa kasi viungani mwa Nairobi limegeuka kuwa kitovu cha baadhi ya migogoro mikubwa na tata ya ardhi nchini Kenya. Rekodi za Mahakama ya Mazingira na Ardhi (ELC) zinaonyesha mtindo unaotia wasiwasi wa ugavi wa ardhi mara mbili, ulaghai, kufurushwa kwa watu kwa nguvu na kesi zinazochukua muda mrefu mahakamani zinazoweza kudumu kwa miaka mingi. Kiini cha mgogoro huo ni mfumo dhaifu wa usimamizi wa ardhi ambao, kulingana na maamuzi ya mahakama, umevamiwa na magenge yanayovuruga rekodi, kuwatisha wakazi na kutumia mianya ya sheria kujinufaisha. Katika moja ya kesi zilizotikisa eneo hilo, Luziki Holdings Limited dhidi ya Ngugi na wengine wawili mwaka wa 2026, mahakama ilisikia jinsi kipande cha ardhi cha Mavoko Town Block 12/326 kilivyovamiwa kwa nguvu. Kwa mujibu wa stakabadhi za mahakama, watu wenye silaha waliokuwa wakisindikizwa na maafisa wa polisi walivamia eneo hilo Mei 2024, wakawashambulia wafanyakazi, kuharibu mali na kuiba mifugo. “Shambulio hilo lilipangwa na kutekelezwa kwa makusudi,” mlalamishi aliambia mahakama. Kesi nyingine zinaonyesha jinsi ulaghai wa ardhi Mavoko ulivyoanza miongo kadhaa iliyopita. Katika kesi ya Mumo dhidi ya Mbondo mwaka wa 2026, mahakama ilichunguza madai yanayokinzana kuhusu ardhi iliyosajiliwa kama Mavoko Municipality Block 6/864 na 6/911. Mlalamishi Peter Maingi Mumo alisema alikuwa akiishi na kuendeleza ardhi hiyo tangu miaka ya 1980. Lakini baadaye, watu wengine waliibuka na barua za ugavi wa ardhi zilizodaiwa kutolewa mwaka wa 1995. Jaji Matheka alitilia shaka hati hizo. “Barua hizo zilikuwa na nambari sawa, zilitolewa siku moja na zilikuwa na maelezo yanayofanana,” mahakama ilisema. Jaji aliamua kuwa barua hizo zilikuwa za kughushi na akaagiza hati zinazobishaniwa kufutwa. “Ninaona barua hizi kuwa za kughushi,” Jaji Matheka alisema. “Mlalamishi ameonyesha umiliki na maendeleo ya muda mrefu ya ardhi hiyo.” Kwa Bw Mumo, huo ulikuwa ushindi nadra katika mfumo ambao kesi nyingi huishia bila hitimisho la wazi. Kwa wengine, vita si kuhusu uvamizi wa nguvu bali urasimu na ulaghai. Katika kesi nyingine ya Abuga na wengine wanne dhidi ya Mwanzo Development Company Limited mwaka wa 2025, wanunuzi wa ardhi walioinunua miaka ya 1990 waliishtaki kampuni hiyo kwa kushindwa kuwapatia hatimiliki huku ikiendelea kudai malipo zaidi. “Walikuwa wakituomba pesa zaidi kila mara huku wakitishia kuuza upya viwanja vyetu,” mmoja wa walalamishi alisema mahakamani. Jaji Annet Nyukuri alikiri kuwepo kwa tatizo kubwa la biashara zisizo rasmi za ardhi katika Kaunti ya Machakos. Katika kesi nyingine mwaka wa 2017, watu wanane walishtakiwa kwa kuvamia kwa nguvu ardhi iliyodaiwa na Kampuni ya East African Portland Cement pamoja na mpango wa makazi ya jamii. Ardhi hiyo ilikuwa tayari imeshuhudia vurugu, ikiwemo kuuawa kwa mwana wa msimamizi mmoja wa eneo hilo. Chanzo cha migogoro mingi Mavoko kinahusishwa na maelfu ya ekari zilizokuwa zikimilikiwa na Kampuni ya East African Portland Cement. Mwaka wa 2023, mamia ya familia ziliachwa bila makazi baada ya ubomoaji mkubwa katika ardhi yenye utata ya Portland Athi River, baada ya mahakama kuthibitisha kampuni hiyo inamiliki zaidi ya ekari 4,000. “Watu walinunua ardhi kwa nia njema lakini baadaye wakagundua haikuwa ikiuzwa kihalali,” alisema mwanaharakati wa haki za ardhi Athi River, Bw Mumo Musyimi. Mnamo Mei 2026, Bunge la Kaunti ya Machakos lilipokea ombi kutoka kwa wamiliki 124 wa ardhi Syokimau waliotaka kulindwa kwa haki zao za umiliki.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.