“FREDRICK Njoroge Kariuki alikuwa na umri wa miaka 12 alipogunduliwa kuwa na ugonjwa wa mkamba (bronchitis) unaosababishwa na hewa chafu aliyokuwa akivuta kila siku mjini Naivasha. Madaktari walihusisha hali yake na moshi mzito kutoka kwa magari, hasa matatu na pikipiki, unaotanda katika barabara nyingi nchini Kenya. Lakini tofauti na wengi ambao huona hali hiyo kama jambo la kawaida, Fredrick aliamua kupambana nayo. “Nadhani hapo ndipo maisha yangu yalibadilika. Nilijua lazima nifanye jambo,” alisema katika mahojiano. Sasa akiwa na umri wa miaka 17, Fredrick pamoja na mwenzake Miron Onsarigo wameibuka washindi wa Afrika katika tuzo za kimataifa za mazingira za Earth Prize 2026 kutokana na uvumbuzi wao wa kifaa kinachopunguza moshi wa magari. Kifaa hicho kinachoitwa HewaSafi hutengenezwa kwa kutumia vifaa vya kawaida vinavyopatikana kwa urahisi kama maganda ya nazi, taka za kilimo na mwani. “Tunatumia aina ya mwani unaofanana na ukungu unaoota kwenye kuta zenye unyevunyevu,” alisema Fredrick. Kwa mujibu wa vijana hao, kifaa hicho huwekwa moja kwa moja kwenye bomba la moshi wa matatu ili kuchuja hewa chafu gari linapoendelea kusafiri. “Inachuja zaidi ya asilimia 90 ya chembechembe hatari na pia hupunguza hewa sumu,” alisema Miron ambaye anatoka Kisumu. Uvumbuzi huo ulianza kutokana na hali waliyozoea kuona kila siku. “Kisumu watu wengi huugua kutokana na moshi wa magari lakini imekuwa jambo la kawaida. Mimi nilihisi si sawa na nilitaka kusaidia,” alisema Miron. Uchafuzi wa hewa ni tatizo kubwa nchini Kenya. Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa kiwango cha uchafuzi wa hewa Nairobi ni zaidi ya mara tatu ya kiwango kinachopendekezwa. Wataalamu wa afya wanakadiria kuwa mamia ya watu hufariki kila mwaka jijini Nairobi kutokana na maradhi yanayohusishwa na hewa chafu. Fredrick alisema matatu nyingi Kenya zina injini za zamani zisizo na vifaa vya kisasa vya kudhibiti moshi. Kifaa hicho kiligharimu takriban Sh16,000 kutengeneza na tayari vijana hao wamefanya majaribio na chama kimoja cha matatu huku wakipanga kushirikiana na chama cha Akiba na Mikopo cha Matatu (SACC) cha Eastleigh ili kupanua matumizi yake. Washindi hao walizawadiwa zaidi ya Sh1.6 milioni ili kuendeleza mradi wao. “Vijana wengi wana mawazo mazuri lakini changamoto ni ukosefu wa ufadhili na usaidizi,” alisema Fredrick. Kwa sasa, wawili hao ambao ni wanafunzi katika M-Pesa Academy wanapanga kutengeneza matoleo tofauti ya kifaa hicho kwa watumiaji mbalimbali wa sekta ya usafiri wa umma. “Nataka vijana wajue kuwa hakuna kisichowezekana. Ukiamua unaweza kufanya chochote,” alisema Miron.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
