“MAAFISA wa usalama wanaochunguza mauaji ya watu saba katika kijiji cha Kwa Kamari, Kaunti ya Kitui, sasa wanachunguza uwezekano wa makundi ya kigaidi kuhusika. Duru ya usalama karibu na uchunguzi huo ambayo haikutaka kutajwa, ilidokezea Taifa Leo kuwa hali ya mashambulizi ya kulipizana kisasi imeibua wasiwasi mkubwa. “Asili ya mashambulizi haya ya kulipizana kisasi ni ya kutatanisha. Tunachunguza uwezekano wa kuingiliwa na wahalifu kutoka nchi jirani inayokumbwa na migogoro,” ilisema duru hiyo. Watu hao saba walidaiwa kuuawa na washukiwa wa wafugaji ngamia. Ufichuzi wa sasa wa uwezekano wa kuhusika kwa magaidi unajiri huku Naibu Rais Kithure Kindiki akitoa ishara za wazi kuwa maafisa wa usalama wanawakaribia watu waliohusika na mauaji hayo yaliyotokea wiki mbili zilizopita. Akizungumza na wanahabari katika Chuo Kikuu cha South Eastern Kenya mjini Kitui Jumatano, Profesa Kindiki, alisema serikali imejitolea kurejesha amani na kukomesha mizozo ya mara kwa mara inayoshuhudiwa katika eneo linalopakana na Kaunti ya Tana River. Aliwaonya wanasiasa na maafisa wa serikali dhidi ya kuchochea jamii zinazohusika katika migogoro hiyo. “Tumeona maendeleo katika kuwawajibisha waliohusika lakini hilo pekee halitoshi. Serikali itahakikisha wananchi wa Kitui wako salama,” alisema Prof Kindiki. Kauli hiyo ilitolewa huku hali ya taharuki ikiendelea katika eneo la Mwingi kufuatia kuuawa kwa mvulana wa miaka 14 anayedaiwa kuuawa na wafugaji ngamia wiki iliyopita. Kijana huyo, Joseph Mutemi, aliuawa siku mbili tu baada ya washukiwa wanoadaiwa kuwa wafugaji ngamia kuvamia kijiji cha Kwa Kamari katika eneo la Tseikuru na kuwaua watu saba kwa risasi na mapanga. Wavamizi hao pia walipora mali na kuchoma maduka katika kituo cha biashara cha Kwa Kamari. Kwa mujibu wa polisi, shambulizi la Aprili 25 lilikuwa ni kisasi kufuatia kuuawa kwa wafugaji watatu wa ngamia waliodaiwa kuuawa na wakulima. Wafugaji hao ni Musa Abdirhaman, Mohammed Aden Ahmed na Abdi Dakane. Polisi wanasema mauaji yalikuwa ni kisasi baada ya mfugaji mmoja kumuua mkulima kwa mapanga siku moja iliyotangulia. Taifa Leo imebaini kuwa mkulima huyo, aliyetambuliwa kama Stephen Kyalo Kimwele, aliuawa baada ya ngamia kuuawa na watu wasiojulikana. Inaaminika kuwa mashambulizi hayo yanachochewa na migogoro ya malisho na maji kati ya wakulima na wafugaji wa ngamia. Profesa Kindiki aliwakosoa wafugaji wanaoruhusu ngamia wao kula mazao ya wakulima. “Ingawa kuokoa mifugo dhidi ya ukame ni jambo halali, hilo haliwezi kutumika kuvunja haki ya watu wengine ya kumiliki mali. Hakuna mtu ana haki ya kulisha mifugo wake kwenye mashamba ya watu wengine,” alisema.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
