skipToContent
🌐All

Mbadi aonekana kujipanga kuwa kigogo Nyanza baada ya mauti ya Raila

Mbadi aonekana kujipanga kuwa kigogo Nyanza baada ya mauti ya Raila
WAZIRI wa Fedha John Mbadi anaonekana kuimarisha juhudi za kudhibiti siasa za Luo Nyanza na kuamua mwelekeo wa ODM baada ya mauti ya marehemu Raila Odinga. Akiwa kati ya wanasiasa walioshirikiana na marehemu Odinga kwa miaka min gi, Bw Mbadi anaonekana kuchukua mwelekeo ambao utahakikisha ana ushawishi mkubwa eneo hilo 2027 na hata 2032. Waziri huyo, alitangaza kuwa hatawania kiti chochote cha kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao. Kauli ya waziri huyo kwenye video aliyoweka kwenye ukurasa wake wa Facebook kutokana na mkutano wa ODM mnamo Mei 4, jijini Mombasa, umezua mdahalo baadhi wakifasiri alimkosea heshima marehemu Raila. “Huwezi kutuambia kuwa baba alisema hili au baba hakusema lile. Huyo baba yuko wapi atupee ushahidi kuhusu kile alichosema au hakusema,” akasema Bw Mbadi akionekana kuwa na hasira. “Ni miezi sita na baba alitufanyia mengi lakini nasi tulipigania baba. Haingekuwa sisi, basi baba hangekuwa mtu wa hadhi yake alipokufa,” akasema Bw Mbadi. Kauli yake imezua maoni mseto miongoni mwa wafuasi wa ODM kwenye mitandao ya kijamii. Wakati baadhi waliiona kama kutoheshimu Raila, wengine walimtetea Bw Mbadi wakisema chama kinapaswa kukubali ukweli kwamba kiongozi wake wa muda mrefu hayupo tena na kuanza kujipangia mustakabali wake. Matamshi hayo yamemweka Bw Mbadi kwenye mvutano na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kisumu Ruth Odinga, ambaye aliwashutumu baadhi ya viongozi kwa kushindwa kudumisha umoja wa ODM. Bi Odinga alimshutumu waziri huyo kwa kudharau jina la Odinga ambalo alilitumia kujikweza kisiasa. Katika mahojiano na Taifa Leo , Bw Mbadi alisema matamshi yake hayakuwa na chochote kibaya ila kila mtu ana hiari ya kuifasiri jinsi anavyotaka. “Raila alitujenga, lakini kama jamii ya Waluo, tulifanya kazi kubwa sana kumuunga mkono. Wapo wanaounga mkono nilichosema na wapo wanaopinga, na sioni tatizo lolote katika hilo,” akasema. “Sioni jambo lolote la kuomba msamaha kwa sababu mimi ndiye niliyeachia video hiyo hadharani, na sina uwezo wa kudhibiti jinsi mtu anavyoitafsiri,” akaongeza. Ijumaa iliyopita, Bw Mbadi alitawazwa kuwa mlezi wa Baraza la Wazee wa Luo, Tawi la Nairobi, hatua ambayo baadhi ya wachanganuzi wa kisiasa wanaiona kama sehemu ya mikakati ya kuimarisha nafasi yake kisiasa. “Muhimu zaidi, nataka kuwahakikishia wazee na jamii kwa ujumla kuhusu dhamira yangu ya kweli ya kuwatumikia kwa bidii na kwa uaminifu katika nafasi hii ya ulezi waliyonipa,” alisema. Katika miezi ya hivi karibuni, Bw Mbadi ameongeza kwa kiasi kikubwa shughuli zake za kisiasa kote Nyanza. Mara kwa mara amekuwa akitumia helikopta ku hudhuria mazishi, hafla za michango na mikutano ya kisiasa, huku akijaribu kuimarisha uungwaji mkono wa Rais Ruto katika eneo hilo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Bw Mbadi aliwahi kuwa Mbunge wa Gwasi kati ya mwaka 2007 na 2013 kabla ya kuchaguliwa tena mwaka 2013 na 2017 kama Mbunge wa Suba Kusini, baada ya eneo hilo kubadilishwa jina. Mwaka 2022, alikuwa ameonyesha nia ya kuwania ugavana wa Homa Bay, lakini alishawishiwa na marehemu Odinga kumuunga mkono Gladys Wanga. Hata hivyo, wakati wa hafla ya umma iliyohudhuriwa na Rais Ruto na marehemu Odinga huko Homa Bay mnamo Mei 30, 2025, Bw Mbadi alitangaza kuwa hatawania nafasi yoyote ya kisiasa mwaka 2027.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.