“MBUNGE wa Bumula, Jack Wamboka ameondolewa rasmi katika Kamati yenye ushawishi mkubwa ya Uwekezaji wa Umma (PIC) mwezi mmoja baada ya kusimamishwa kama mwenyekiti wake kufuatia madai ya hongo. Katika mabadiliko mapya ya kamati za Bunge la Kitaifa, Bw Wamboka sasa amehamishwa kuwa mwanachama wa Kamati ya Uwiano wa Kitaifa na Fursa Sawa. Mbunge wa Luanda Dick Maungu, ambaye amekuwa mwenyekiti wa muda wa kamati hiyo, sasa anatarajiwa kuthibitishwa rasmi kama mwenyekiti mpya. Kamati ya PIC ni mojawapo ya kamati zinazochukuliwa kuwa zenye ushawishi mkubwa kwa wabunge kutokana na mamlaka yake ya kusimamia matumizi ya fedha za umma. Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, kamati hiyo huchunguza hesabu zilizokaguliwa za mashirika ya serikali, vyuo vikuu na taasisi za umma. Kuondolewa kwa Bw Wamboka kunafuatia hatua ya Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula aliyemsimamisha mwezi uliopita baada ya mashahidi waliokuwa wakifika mbele ya kamati hiyo kulalamikia unyanyasaji kutoka kwake. Tume ya Uwiano na Utengamano wa Kitaifa (NCIC), kupitia barua kwa Spika, ilidai maafisa wake walidhalilishwa na kunyanyaswa walipofika mbele ya kamati hiyo. Kwa mujibu wa malalamishi hayo, NCIC ilidai Bw Wamboka aliwataka maafisa kutoa hongo ili wapendelewe mbele ya kamati. Mbunge huyo hata hivyo alikanusha madai hayo bungeni akisema alikuwa anaadhibiwa kwa kusisitiza uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma. Mabadiliko hayo pia yamewaathiri wandani wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ambao wameondolewa katika kamati zenye ushawishi na kuhamishwa katika kamati zisizo na nguvu kubwa. Mbunge maalum wa UDA Teresia Mwangi atachukua nafasi ya mbunge wa Manyatta, John Mukunji katika Kamati ya Utekelezaji wa Katiba (CIOC). Bw Mukunji amehamishiwa Kamati ya Huduma za Wanachama maarufu kama “kamati ya upishi”. Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba sasa amepelekwa Kamati ya Fedha na Mipango ya Kitaifa huku mbunge wa Kirinyaga Betty Maina Njeri akihamishwa hadi Kamati ya Uchukuzi. Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah alisema mabadiliko hayo yamelenga kuwapa wabunge wapya nafasi katika kamati kulingana na kanuni za bunge. Hata hivyo, mchambuzi wa siasa Ahmed Dahir amesema hatua hiyo pia inalenga kuipa serikali udhibiti kamili wa kamati muhimu za bunge. “Kamati ndizo vituo vya nguvu bungeni. Kumwondoa mtu katika PIC si jambo la kawaida, kuna uzito wa kisiasa na kitaasisi,” alisema.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
