“HUZUNI na majonzi zilitanda katika mochari ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Naivasha jana huku familia, jamaa na marafiki wa wasichana 16 waliofariki katika mkasa wa moto katika Shule ya Upili ya Utumishi Girls wakianza shughuli ngumu ya kutambua miili ya wapendwa wao. Moto huo uliteketeza bweni la Meline Waithera Block B usiku wa Jumatano. Bweni hilo lilikuwa na wanafunzi 220 wa Gredi ya 10, Kidato cha Tatu na Kidato cha Nne. Wazazi wa wasichana hao 16, wakifuatana na jamaa zao, walifika hospitalini kwa shughuli ya uchunguzi wa maiti huku wakifarijiana katika kipindi hiki kigumu ambacho kimeacha nchi katika maombolezo. Madaktari watatu wa uchunguzi wa maiti wametumwa kuhakikisha zoezi hilo linakamilika haraka na kwa ufanisi. Uchunguzi huo unatarajiwa kusaidia kubaini chanzo halisi cha vifo hivyo pamoja na kurahisisha kutambua miili. Familia hizo pia zinasubiri matokeo ya vipimo vya DNA kabla ya kukabidhiwa miili kwa mazishi. Nje ya hifadhi ya maiti, jamaa walionekana wakiwa wamelemewa na huzuni. Wengine walikuwa wakisali huku wengine wakikumbuka maisha ya wasichana hao ambao ndoto zao zilikatizwa ghafla na moto huo. Wasichana wengine saba waliopata majeraha bado wamelazwa katika hospitali moja jijini Nairobi. Maafisa wa hospitali waliimarisha usalama katika eneo la mochari ili kudumisha utulivu wakati wa zoezi hilo muhimu. Ni wanafamilia wa karibu na wahudumu walioidhinishwa pekee kuingia. Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya pia limeweka mahema katika eneo hilo, ambapo washauri nasaha na wanasaikolojia wanatoa huduma kwa familia zilizoathirika. Magari mawili ya ambulensi yamewekwa tayari kushughulikia dharura zozote za kiafya. Baada ya kuona miili hiyo, mmoja wa jamaa, Bw Njuki Nthimba, alisema ni miili mitatu pekee iliyoweza kutambuliwa kwa urahisi huku mingine ikiwa imeungua vibaya kiasi cha kutotambulika.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
