skipToContent
🌐All

MPAKA LINI? Huzuni, maswali tele wanafunzi wakifa tena kwenye mkasa wa moto shuleni

MPAKA LINI? Huzuni, maswali tele wanafunzi wakifa tena kwenye mkasa wa moto shuleni
MASWALI yanaendelea kuzuka kuhusu chanzo cha moto ulioteketeza bweni la Shule ya Wasichana ya Sekondari ya Utumishi iliyoko Kaunti ya Nakuru huku visa kama hivyo vikiendelea kutokea. Wakenya walieleza hisia kali wakishangaa wanafunzi wataendelea kuangamia mpaka lini katika mabweni huku viwango vya usalama vikididimia. Haya yanajiri huku taarifa mpya zikiibuka kuonyesha kuwa huenda moto huo uliosababisha vifo vya wanafunzi 16 uliwashwa kimakusudi. Wanafunzi wengine 79 walijeruhiwa.Viongozi na maafisa wa usalama waliotembelea shule hiyo Alhamisi walisema uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo halisi cha moto huo. Hata hivyo, taarifa za awali zinaeleza kuwa, huenda moto huo ulianzia kwenye godoro lililokuwa likiwaka ndani ya bweni moja la shule hiyo. Katika mahojiano ya kipekee, mzazi wa mwanafunzi wa Kidato cha Tatu aliyenusurika katika janga hilo, ambaye alikataa kutajwa jina, alisema moto ulianza katikati ya bweni lililokuwa na wanafunzi wa Kidato cha Tatu, Gredi10 na Kidato cha Nne. Mzazi huyo alisema binti yake alieleza kuwa, kundi la wanafunzi wa Kidato cha Tatu lilichochea moto huo kwa kuchoma godoro wakati wa kile kilichoelezwa kuwa malalamishi dhidi ya kile walichodai kuwa ukali wa uongozi wa shule. Moto huo ulienea kwa kasi na kuathiri bweni lijulikanalo kama Meline Waithera. “Binti yangu aliniambia kuwa majira ya saa kumi usiku kuelekea alfajiri, kundi la wanafunzi wa Kidato cha Tatu walichoma godoro, na cheche za moto zilienea haraka katika bweni lote,” alisema mzazi huyo. “Kwa kuwa kitanda chake kilikuwa karibu na mlango wa kutokea, aliweza kutoroka bila kujeruhiwa.” Kwa mujibu wa uongozi wa shule, bweni lililochomeka lilikuwa na takriban wanafunzi 220. Janga hilo lilisababisha vifo vya wanafunzi 16 huku wengine 79 wakipata majeraha mbalimbali. Waziri wa Elimu, Julius Ogamba, alisema wanafunzi saba kati ya waliolazwa walisafirishwa Nairobi kwa matibabu maalumu, huku wengine 71 wakiruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kupata nafuu. Alisema shule hiyo ilikuwa na jumla ya wanafunzi 815, na wakati wa tukio hilo 809 walikuwa shuleni. “Wanafunzi saba bado wamelazwa hospitalini. Tuna vifo 16 vilivyothibitishwa,” alisema waziri huyo. Waziri huyo aliongeza kuwa moto huo ulizuka majira ya saa sita na dakika arobaini na tano usiku na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali ya thamani ya mamilioni ya pesa. Walionusurika walisimulia jinsi moto ulivyoenea kwa kasi kutokana na mbao zilizotumika kugawa sehemu za bweni hilo. Walisema moshi mzito uliwafanya wengi washindwe kutoka kupitia lango kuu. “Moto ulianza katikati ya bweni karibu na kitanda changu. Nilipoona moshi unazidi kujaa na mlango haupitiki, niliruka kupitia dirishani nikajeruhi mikono na miguu,” alisema mwanafunzi mmoja anayepokea matibabu katika Hospitali ya St Mary’s. Walimu wanaoishi ndani ya shule walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika eneo la tukio na kusaidia kuwahamisha wanafunzi kabla ya vikosi vya dharura kufika. Polisi walisema mkuu wa shule, Bi Joycelene Muraguri, alitoa taarifa mapema baada ya moto kuanza, na hivyo kuruhusu hatua za haraka kuchukuliwa na vikosi vya dharura. Vikosi hivyo vilijumuisha zimamoto kutoka Naivasha, Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), kikosi cha Polisi wa Kukabiliana na Wizi wa Mifugo (ASTU), Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), pamoja na Shirika la Msalaba Mwekundu. Kamanda wa Polisi wa Gilgil, Winston Mwakio, alisema vikosi hivyo kwa pamoja vilifanikiwa kudhibiti moto huo baada ya takriban saa moja ya juhudi za pamoja. Waathiriwa walikimbizwa katika hospitali mbalimbali za Gilgil na Naivasha, ambapo wengi waliripotiwa kutokuwa hatarini licha ya kupata majeraha ya kuungua na majeraha wakijaribu kutoroka. Muuguzi katika Hospitali ya Kaunti ndogo ya Gilgil alisema wengi waliolazwa hawakuwa kwenye hatari, ingawa walikuwa na majeraha ya viwango tofauti kutokana na moshi na moto. Uchunguzi pia umebaini wasiwasi kuhusu muundo wa bweni hilo, huku wazazi na wanafunzi wakilalamikia msongamano, madirisha yenye vyuma, na ukosefu wa milango ya dharura. Baadhi ya wanafunzi walisema wale waliokuwa mbali na mlango mkuu walilazimika kujibana kupitia lango nyembamba au kuruka kutoka ghorofa ili kujiokoa. Wazazi sasa wanataka serikali kupitia upya viwango vya usalama shuleni, wakisema mabweni yana wanafunzi wengi kupita kiasi na hayana njia za kutosha za dharura. “Bweni lina wanafunzi wengi sana na hakuna njia za dharura za kutosha. Tunataka Wizara ya Elimu ichunguze upya usalama wa wanafunzi,” alisema mzazi mmoja. Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin na Naibu Inspekta Jenerali Edward Lagat walitembelea shule hiyo na kuahidi uchunguzi wa kina kubaini chanzo halisi cha moto huo. DCI inaendelea na uchunguzi huku familia zikisubiri majibu kamili kuhusu tukio hilo ambalo limeelezwa kuwa mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya moto shuleni nchini katika miaka ya hivi karibuni.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.