skipToContent
🌐All

Mpasuko watokota Linda Mwananchi

Mpasuko watokota Linda Mwananchi
Miezi michache baada ya kujitokeza kama moja ya sauti kali zaidi za upinzani dhidi ya Rais William Ruto, vuguvugu la Linda Mwananchi sasa linakabiliwa na changamoto ambayo inaweza kuamua mustakabali wake wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Vuguvugu hilo, linalowaleta pamoja viongozi kutoka ODM, Jubilee, Wiper, Ford Kenya na vyama vingine vidogo, limepata umaarufu mkubwa miongoni mwa wafuasi wa upinzani wanaokerwa na ushirikiano unaozidi kuimarika kati ya baadhi ya viongozi wa ODM na serikali ya Kenya Kwanza.Lakini licha ya kuonekana kuwa jukwaa jipya la matumaini kwa sehemu ya wapiga kura wa upinzani, mjadala mkali umeibuka kuhusu mwelekeo wake wa baadaye. Je, Linda Mwananchi inapaswa kubadilika na kuwa chama cha kisiasa, kubaki kama vuguvugu la kisiasa, au kujiunga na muungano mpana wa upinzani unaolenga kumng’atua Rais Ruto mwaka ujao?Mjadala huo umeibua tofauti za wazi kati ya baadhi ya viongozi wake wakuu akiwemo Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Gavana wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na mwenzake wa Saboti Caleb Amisi .Tofauti hizo zimejitokeza zaidi baada ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa kukataa ombi la kuhifadhi jina la chama cha Linda Mwananchi Party of Kenya, hatua iliyozima kwa muda juhudi za kukisajili kama chama rasmi cha kisiasa.Kwa Seneta Sifuna, njia pekee ya kuondoa Kenya Kwanza mamlakani ni kwa upinzani kuungana chini ya mgombea mmoja. “Sisi kama Linda Mwananchi tumekubaliana kwamba hatutatumika kumsaidia Ruto kupata muhula wa pili. Tunaamini hakuna njia nyingine isipokuwa kuwa na tiketi moja ya upinzani,” amesema. Msimamo wake unaonekana kuendana na juhudi za kuunda muungano mpana wa upinzani unaohusisha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na viongozi wengine wanaopinga serikali.Hata hivyo, si viongozi wote wa Linda Mwananchi wanaokubaliana na mtazamo huo. Gavana Orengo amesisitiza kuwa mapambano yao ni ya kurejesha ODM katika misingi yake ya awali badala ya kuondoka ndani ya chama hicho. Amekuwa mkosoaji mkubwa wa ushirikiano kati ya ODM na serikali ya Rais Ruto, akidai kuwa hatua hiyo inahatarisha urithi wa kisiasa wa Raila Odinga.“Sisi bado ni wanachama wa ODM. Tunapigania chama kutoka ndani,” amesema Orengo. Kwa mujibu wake, ODM inapaswa kuendelea kuwa chama huru chenye uwezo wa kusimamisha mgombea wake wa urais mnamo 2027 badala ya kujiunga haraka katika miungano ya kisiasa.Wakati huo huo, matarajio binafsi ya baadhi ya viongozi yameanza kujitokeza waziwazi.Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amesema hana nia ya kuendelea kufanya kazi chini ya kiongozi mwingine wa chama. “Raila Odinga ndiye alikuwa kiongozi wa mwisho wa chama niliyemtumikia. Sasa ni wakati wangu kuwa kiongozi wa chama,” alisema.Ameongeza kuwa ikiwa Linda Mwananchi itaingia katika muungano wowote wa kisiasa, basi inapaswa kufanya hivyo kupitia chama chake. Kauli hiyo imeungwa mkono na Mbunge Caleb Amisi ambaye anaamini kuwa vuguvugu hilo linaweza kupoteza utambulisho wake ikiwa litaunganishwa na makundi mengine kabla ya kujijenga kisiasa. “Linda Mwananchi haina chaguo ila kuwa na chama chake. Hatukuanza harakati hizi ili kujiunga na wengine,” amesema.Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanaonya kuwa changamoto kubwa inayolikabili vuguvugu hilo si upinzani wake kwa serikali bali ukosefu wa mwafaka kuhusu uongozi, sera na muundo wake wa kisiasa.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.