“RAIS wa Amerika, Donald Trump amesema kuwa makubaliano na Iran kuhusu vita vya Mashariki ya Kati, yakiwemo kufunguliwa tena kwa Mkondo wa Hormuz, “kwa kiasi kikubwa yameafikiwa” baada ya mazungumzo aliyofanya na Israeli pamoja na washirika wengine wa eneo hilo mwishoni mwa wiki. Hata hivyo, maafisa wengine walitoa tahadhari Jumapili, huku Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Amerika, Marco Rubio akisema kuwa “hatua kubwa imepigwa, ingawa si maelewano kamili” katika mazungumzo hayo. Rubio, ambaye yuko katika ziara ya siku nne nchini India kwa mikutano na maafisa wa India, Australia na Japan, alisema ana matumaini kuwa kutakuwa na habari njema katika saa zijazo. Rubio alisema mazungumzo hayo yamefanikisha moja ya malengo makuu ya Trump, “yaani dunia ambayo haitakuwa tena na hofu au wasiwasi kuhusu silaha ya nyuklia ya Iran.” Trump alisema Jumamosi kwamba alizungumza na viongozi wa Saudi Arabia, United Arab Emirates, Qatar, Pakistan, Turkey, Egypt, Jordan na Bahrain, na pia kwa njia tofauti na Israeli. “Vipengele na maelezo ya mwisho ya makubaliano hayo yanaendelea kujadiliwa kwa sasa, na yatatangazwa hivi karibuni,” Trump alisema kupitia mitandao ya kijamii bila kutoa maelezo zaidi. Tangazo hilo lilihitimisha wiki ambayo Amerika ilifikiria kufanya mashambulizi mapya dhidi ya Iran, hatua ambayo ingevunja usitishaji wa vita uliokuwapo. Makubaliano hayo yanayotarajiwa yatahusisha ahadi ya Iran kwamba haitatengeneza silaha ya nyuklia, huku Tehran ikikubali kuachana na akiba yake ya uranium iliyorutubishwa kwa kiwango cha juu, kwa mujibu wa maafisa wawili wa eneo hilo. Afisa mmoja mwenye ufahamu wa moja kwa moja wa mazungumzo hayo alisema suala la namna Iran itakavyoachana na uranium yake iliyorutubishwa bado linaendelea kujadiliwa katika kipindi cha siku 60 zijazo. Alisema kuna uwezekano mkubwa kuwa sehemu ya uranium hiyo itapunguzwa kiwango chake cha urutubishaji, huku sehemu iliyobaki ikipelekwa katika nchi ya tatu, ambayo huenda ikawa Urusi. Kwa mujibu wa International Atomic Energy Agency, Iran ina kilo 440.9 za uranium iliyorutubishwa hadi asilimia 60 ya usafi, kiwango ambacho kiko karibu sana na kiwango cha asilimia 90 kinachohitajika kutengeneza silaha za nyuklia. Afisa huyo alisema Mkondo wa Hormuz utafunguliwa taratibu sambamba na Amerika kusitisha mzingiro wake dhidi ya bandari za Iran. Amerika pia itairuhusu Iran kuuza mafuta yake kwa mujibu wa afisa wa pili aliyefahamishwa kuhusu mazungumzo hayo. Maafisa hao wawili walisema rasimu ya makubaliano hayo pia inajumuisha kumalizika kwa vita kati ya Israeli na Hezbollah, pamoja na ahadi ya kutokuingilia masuala ya ndani ya nchi za eneo hilo. Walizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina kwa sababu mazungumzo hayo yalikuwa ya siri. Wiki 12 zimepita tangu Amerikana Israeli kuishambulia Iran Februari 28, na kuwaua maafisa wakuu wa Iran akiwemo kiongozi wake mkuu, huku mashambulizi hayo yakivuruga mazungumzo ya nyuklia kati ya nchi hizo mbili kwa mara ya pili chini ya mwaka mmoja. Iran ilijibu kwa kushambulia Israeli na majirani wanaohifadhi majeshi ya Amerika, hali iliyotikisa mataifa ya Ghuba yaliyokuwa yakijiona salama katika eneo hilo lenye migogoro. Usitishaji vita umeendelea tangu Aprili 7. Hata hivyo, uamuzi wa Iran wa kufunga kwa kiasi kikubwa Mlango-Bahari wa Hormuz kwa meli zinazobeba mafuta, gesi asilia na bidhaa nyingine muhimu kutoka eneo hilo umeendelea kuwa chanzo kikubwa cha wasiwasi wa dunia na maumivu ya kiuchumi. Maafisa wa Israel wana wasiwasi kuwa Hezbollah, kundi la wanamgambo wa Lebanon linaloungwa mkono na Iran, bado ni tishio kubwa kwa Israel na kwamba Lebanon haina uwezo wa kulivua silaha. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alimwonya Trump kuwa Israel “inaendelea kuwa na uhuru wa kuchukua hatua dhidi ya vitisho katika maeneo yote, ikiwemo Lebanon,” kwa mujibu wa afisa aliyefahamu mazungumzo hayo. Afisa huyo alisema Trump aliweka wazi kwa Netanyahu kuwa hatatia saini makubaliano yoyote ya mwisho bila Iran kuvunja kabisa mpango wake wa nyuklia na kuondoa uranium yote iliyorutubishwa kutoka nchini humo. Waziri wa Sayansi na Teknolojia wa Israel Gila Gamliel, ambaye ni mwanachama wa chama cha Likud cha Netanyahu na pia mjumbe wa baraza lake la usalama wa taifa, aliiambia Redio ya Jeshi la Israel Jumapili asubuhi kwamba Israel inachukua msimamo wa “kusubiri na kuona.”
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
