“VIONGOZI wa upinzani Kaunti ya Meru wameingia katika mvutano wa kisiasa na vita vya ubabe, hali inayotishia kuvuruga mikutano ya kisiasa inayopangwa kufanyika eneo hilo. Kiongozi wa chama cha PNU Peter Munya, na Katibu wa Kitaifa wa Uratibu wa chama cha DCP Mithika Linturi, wamezidisha tofauti zao huku maandalizi ya mikutano ya pamoja ya upinzani ya siku tano katika kaunti za Meru na Isiolo yakishika kasi. Mikutano hiyo, inayotarajiwa kuanza Alhamisi hadi Jumatatu, iliahirishwa mwezi uliopita kutokana na maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya mafuta yaliyotikisa nchi. Bw Munya amesema viongozi wa upinzani akiwemo Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka, Fred Matiang’i, Martha Karua na Eugene Wamalwa wataungana naye katika mikutano hiyo inayolenga kuimarisha ushawishi wa upinzani katika eneo hilo. Hata hivyo, Bw Linturi amemshutumu Bw Munya kwa kutumia picha za kiongozi wa chama chake kwenye mabango ili kuvutia umati wa watu. Pia, alijitenga na mikutano hiyo akisema kuwa licha ya kuwa mratibu mkuu wa shughuli za DCP, hakuwa na habari yoyote kuhusu mikutano inayopigiwa debe na PNU. “Kama Katibu wa Kitaifa wa Uratibu wa DCP, nimearifiwa kuhusu bango linalosambazwa likidaiwa kuwa la kuvutia umati kwa niaba ya kundi fulani la kisiasa ambalo halina ushawishi mkubwa. Hatuna habari kuhusu mikutano hiyo na ratiba yetu imejaa shughuli nyingine,” alisema Bw Linturi kupitia ukurasa wake wa Facebook. Aliwataka wafuasi wa DCP kupuuza matangazo hayo, akisema PNU iko huru kuendesha shughuli zake za kisiasa lakini isiwadanganye wakazi wa Meru kwa kutumia picha za viongozi wengine. Akizungumza na Taifa Leo jana, Bw Linturi alisema chama chake kimeamua kutoshiriki mikutano iliyoandaliwa na PNU kwa kuwa Bw Munya naye hashiriki shughuli za DCP. “Kwa mtazamo wangu, Munya na mimi ni washindani wa kisiasa. Tunakubaliana tu katika wito wa rais kuhudumu muhula mmoja. Meru ni ngome ya DCP na hatutaruhusu atumie chama chetu kujijenga kisiasa. Tutalinda eneo letu dhidi ya uvamizi wowote,” alisema Bw Linturi. Waziri huyo wa zamani wa Kilimo amesema analenga kumtupa Bw Munya katika dimbwi la kusahaulika kisiasa huku wawili hao wakitarajiwa kuwania ugavana wa Meru mwaka wa 2027. “Munya ni mtu anayependa kufanya mambo peke yake na hana nia ya kushirikiana na viongozi wengine. Ndiyo maana hafai kuwa gavana wa Meru,” alisema. Mwezi uliopita, Bw Linturi pia alipinga mikutano hiyo na kuwataka wafuasi wa DCP kutoshiriki kabla ya kuahirishwa kutokana na maandamano ya bei ya mafuta. Kwa upande wake, Bw Munya alipuuza kauli za Bw Linturi akisema mikutano hiyo imeandaliwa na viongozi wakuu wa muungano wa upinzani. "Kama kiongozi wa PNU, mimi ni mwanachama wa Kamati ya Viongozi Wakuu wa Muungano wa Upinzani. Tunajadili masuala haya katika ngazi hiyo. Mimi ndiye mwenyeji wa viongozi wengine wa upinzani na ndiye mwenye mamlaka ya kuzungumzia mipango ya mikutano hii. Wengine wanaojaribu kuzungumza wanapaswa kusubiri maelekezo kutoka kwa viongozi wa vyama vyao," alisema Bw Munya. Uhasama wa kisiasa kati ya viongozi hao wawili umeongezeka katika siku za hivi karibuni, huku wakirushiana maneno wakati wa mazishi yaliyofanyika Tigania Magharibi.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
