skipToContent
🌐All

Obado, aliyekiri kuwa katika mapenzi na Sharon, kujua iwapo ana hatia ya mauaji yake

Obado, aliyekiri kuwa katika mapenzi na Sharon, kujua iwapo ana hatia ya mauaji yake
KWA karibu miaka minane sasa, mauaji ya Sharon Otieno na mwanawe yameendelea kuitikisa siasa na mfumo wa haki nchini Kenya. Kifo cha Sharon, aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo mwenye umri wa miaka 26, kilizua hasira kote nchini baada ya mwili wake kupatikana umetupwa kichakani katika kaunti ya Homa Bay mwaka wa 2018. Kesi hiyo ilitawala vichwa vya habari kwa miezi kadhaa huku ikifichua mchanganyiko wa siasa, mahusiano ya siri, usaliti na mauaji. Hivi leo, Mahakama Kuu inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu iwapo aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado pamoja na washukiwa wenzake wawili wana hatia ya kupanga mauaji hayo. Jaji Cecilia Githua atatoa hukumu hiyo katika Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi, kuanzia saa tatu asubuhi. Karibu miaka minane baada ya mwili wa Sharon kupatikana karibu na kijiji cha Owade, mahakama sasa itaamua ikiwa Bw Obado, aliyekuwa msaidizi wake Michael Oyamo na aliyekuwa Karani wa Kaunti ya Migori Caspal Obiero wanawajibika kwa mauaji hayo. Kesi hiyo ilivutia taifa kuanzia Septemba 3, 2018, Sharon alipotoweka baada ya kuondoka katika Hoteli ya Graca mjini Rongo akiwa na mwanahabari na wanaume wawili. Kiini cha kesi hiyo kilikuwa uhusiano wa siri kati ya Sharon na Bw Obado ambao uliwekwa wazi baada ya Sharon kupata ujauzito. Ripoti ya upasuaji wa maiti ilionyesha kuwa Sharon alikuwa na ujauzito wa wiki 28 alipouawa. Madaktari walisema alidungwa visu mara kadhaa shingoni, tumboni na mgongoni. Uchunguzi pia ulionyesha huenda alibakwa kabla ya kuuawa. Waendesha mashtaka waliambia mahakama kuwa mauaji hayo hayakuwa ya bahati mbaya bali yalipangwa kwa makusudi ili kumzima Sharon na kumlinda mwanasiasa huyo dhidi ya fedheha. Upande wa serikali ulisema ujauzito huo ulikuwa tishio kwa mustakabali wa kisiasa wa Bw Obado wakati wa muhula wake wa pili kama gavana. Bw Obado alikubali kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Sharon na kwamba alikuwa baba wa mtoto huyo ambaye alikuwa hajazaliwa, lakini akakanusha kuhusika katika mauaji hayo. “Sikumuua Sharon wala kushirikiana na washukiwa wenzangu kupanga mauaji hayo,” aliambia mahakama. Alisema alikuwa tayari amekubali jukumu la kulea mtoto huyo na alikuwa amepanga kumnunulia Sharon ardhi na kumjengea nyumba Homa Bay. Hata hivyo, upande wa mashtaka ulitegemea ushahidi wa rekodi za simu, ushahidi wa mashahidi pamoja na ushahidi wa kisayansi uliokusanywa kwa miaka kadhaa. Mwanahabari aliyekuwa ameandamana na Sharon usiku wa kutoweka kwake aliambia mahakama kuwa waliingizwa kwa nguvu ndani ya gari kabla yeye kuruka nje ya gari hilo lilipokuwa likienda na kutoroka. Ushahidi wake uligeuka kuwa sehemu muhimu ya kesi ya upande wa mashtaka. Baada ya kutoroka, aliripoti tukio hilo kwa polisi na mwili wa Sharon ukapatikana siku iliyofuata karibu na Mto Owade. Waendesha mashtaka waliwasilisha mashahidi 42 pamoja na vielelezo 81 wakati wa kesi hiyo ndefu. Mawakili wa utetezi walipinga ushahidi huo wakisema ulikuwa wa kubahatisha na haukuonyesha moja kwa moja kuwa Bw Obado alihusika na mauaji hayo. Sasa taifa linasubiri hukumu ambayo itajibu swali ambalo limekuwa likiandama siasa na mfumo wa haki nchini tangu mwaka wa 2018: Nani aliyemuua Sharon Otieno?
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.