skipToContent
🌐All

Oburu aelekeza Nyanza kwa Ruto, Linda Mwananchi ikimsifu Kalonzo

Taifa Leo (Swahili) Global
Oburu aelekeza Nyanza kwa Ruto, Linda Mwananchi ikimsifu Kalonzo
VIONGOZI wa ODM jana walitangaza kuwa wataongoza eneo la Luo Nyanza kumuunga mkono Rais William Ruto kuwahi muhula wa pili huku wakisisitiza kuwa eneo hilo lazima liwe sehemu ya serikali itakayoundwa mnamo 2027. Kiongozi wa ODM Dkt Oburu Oginga na Mwenyekiti wa chama Gladys Wanga, waliongoza viongozi kutoka eneo hilo kusema kuwa ni ngoma ya Rais Ruto pekee watakayoirindima mwakani. Bi Wanga alisoma stakabadhi yenye hoja saba ambazo walisema zimesababisha waafikie kuunga mkono azma ya Rais Ruto. “Tunasisitiza kuwa tutaendelea kusalia ndani ya Serikali Jumuishi na serikali itakayokuja kwa sababu tunashirikiana kutwaa mamlaka. Tunashinikiza kutekelezwa kwa ajenda 10 hasa kuhusu kuwalipa wale ambao ni wahanga wa ghasia za baada ya uchaguzi,” akasema Bi Wanga. Dkt Oginga naye alisema kuwa ODM itasalia ndani ya Serikali Jumuishi na haitazungumza na upinzani unaoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. “Wanaoshindana nasi wanastahili kujua kuwa tunasaka mamlaka mnamo 2027 na tutawashinda. Binafsi siwezi kuwaongoza watu wangu waende kwa Gachagua. Tutazungumza na UDA pamoja na vyama vingine kwa ajili ya kutwaa mamlaka,” akasema Dkt Oginga. Aliongeza kuwa ataendelea kuongoza ODM wala hakujiteua katika wadhifa huo baada ya mauti ya Raila Odinga. “Baadhi ya watu waliona natosha na wale wanaonionea wivu wanastahili kujua kuwa mimi ndiye niliangukiwa na roho,” akaongeza. Alisisitiza kuwa iwapo yeye ndiye chanzo cha mgawanyiko katika jamii ya Waluo, basi angekuwa amejiuzulu. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Gavana wa Kisii Simba Arati na mwenzake wa Kakamega Ferndandes Barasa ambao walisema kuwa maeneo yao yataendelea kusalia ndani ya ODM. Katika eneo la Ukambani, mrengo wa Linda Mwananchi jana ulisema upo tayari kushirikiana na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka ili kama ‘kurudisha’ mkono kutokana na uungwaji mkono wao kwa Raila Odinga mnamo 2013, 2017 na 2022. “Kalonzo ni shujaa ambaye ana maslahi ya nchi rohoni,” akasema Gavana wa Siaya James Orengo. Bw Orengo na wenzake walihutubia mikutano ya kisiasa katika miji ya Mutituni, Machakos na Mlolongo. Alikuwa ameandamana na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino. Bw Orengo na Mbunge wa Kathiani Robert Mbui ambaye ni katibu mtendaji wa Wiper walifichua kuwa kuna mipango ya kuhakikisha upinzani na viongozi wa Linda Mwananchi wanafanya kazi pamoja. Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi alisema muungano huo una baraka za Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Waziri wa zamani wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangí.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.