skipToContent
🌐All

Oburu kuongoza mkutano wa ‘Azimio la Waluo’ kutoa mwelekeo wa siasa za 2027

Oburu kuongoza mkutano wa ‘Azimio la Waluo’ kutoa mwelekeo wa siasa za 2027
VIONGOZI wakuu wa chama cha ODM Jumapili wanatarajiwa kuongoza jamii ya Waluo kutangaza azimio muhimu kuhusu uchaguzi mkuu wa 2027 katika mkutano mkubwa wa kisiasa utakaofanyika Kisumu. Mkutano huo umepewa jina la ‘Azimio la Waluo’, viongozi wa chama hicho wakiulinganisha na mkutano wa mwaka wa 2002 ambapo eneo la Nyanza lilimuunga mkono aliyekuwa Rais Mwai Kibaki katika uchaguzi mkuu. Wachanganuzi wa siasa wanautazama mkutano huo kama mojawapo ya mikutano muhimu zaidi kuwahi kufanyika katika jamii hiyo tangu kifo cha aliyekuwa kiongozi wa ODM, Raila Odinga mnamo Oktoba mwaka wa 2025. Kifo cha Bw Odinga kiliacha pengo kubwa kisiasa katika eneo la Nyanza huku kukizuka vita vya urithi na mgawanyiko ndani ya ODM. Mgawanyiko huo umeibua makundi mawili yanayoshindana kuhusu mwelekeo wa chama. Kundi la Linda Ground linaongozwa na Oburu Oginga huku kundi la Linda Mwananchi likiongozwa na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna. Sasa viongozi wa juu wa chama pamoja na maafisa wakuu serikalini wanatarajiwa kutumia mkutano huo kujaribu kuunganisha jamii ya Waluo na kutoa msimamo mmoja kuelekea uchaguzi wa 2027. Dalili zote zinaonyesha kuwa mkutano huo utatumika kurai jamii hiyo kumuunga mkono Rais William Ruto kwa muhula wa pili wa urais. Miongoni mwa viongozi wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo ni Dkt Oburu Oginga, manaibu viongozi wa ODM Simba Arati na Abdulswamad Nassir pamoja na mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho Gladys Wanga. Mawaziri wa serikali akiwemo Waziri wa Fedha John Mbadi, Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na Waziri wa Madini Hassan Joho pia wanatarajiwa kushiriki mkutano huo. Viongozi hao wanatarajiwa kuelezea jamii hiyo umuhimu wa kushirikiana na serikali ya Kenya Kwanza na kuunga mkono ushirikiano wa kisiasa kati ya ODM na chama cha UDA cha Rais Ruto. Katika kikao cha viongozi wa ODM kilichofanyika Mombasa hivi majuzi, viongozi wa Nyanza walilaumiwa kwa kuchangia mgawanyiko unaoshuhudiwa ndani ya chama hicho. Dkt Oginga tayari ameonyesha msimamo wake kuhusu mkutano huo akisema yeyote ambaye hatahudhuria atakuwa amejiweka nje ya mwelekeo mpya wa kisiasa wa jamii ya Waluo. “Jumapili lazima tuonyeshe nguvu na umoja wetu. Hatujamfukuza mtu yeyote lakini atakaye kosa kuja atakuwa amejiondoa mwenyewe katika jamii na chama,” alisema Dkt Oginga. Aliongeza kuwa hawezi kuiongoza jamii yake nje ya serikali na ndio sababu wanataka kuhakikisha wako serikalini hata baada ya uchaguzi wa 2027. Mkutano huo tayari umeanza kuzua mvutano wa kisiasa miongoni mwa viongozi wa Nyanza wanaopinga ushirikiano kati ya ODM na serikali ya Rais Ruto. Gavana wa Siaya James Orengo ni mmoja wa viongozi wakuu wanaopinga msimamo wa kundi la Oburu Oginga. Bw Orengo anaegemea upande wa Linda Mwananchi unaopinga mpango wa kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi ujao. Mbunge wa Kisumu Central Joshua Oron alisema mkutano huo utatoa mwelekeo rasmi wa kisiasa ambao jamii ya Waluo itafuata mwaka wa 2027. “Kila mtu amealikwa Kisumu kwa sababu kama jamii tutatoa msimamo mmoja wa kisiasa. Jamii hii imekuwa na umoja kila mara na hatuwezi kugawanyika sasa kwa sababu Raila hayupo,” alisema Bw Oron. Kwa upande wake, Mbunge wa Alego Usonga Samuel Atandi alisema jamii ya Waluo sasa inalenga kuwa sehemu kamili ya serikali ijayo. “Tukikutana Kisumu tutajitangaza kama chama kimoja na watu walioungana. Umoja wetu ndio umeifanya jamii hii kuheshimiwa nchini,” alisema Bw Atandi ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Kitaifa. Bw Atandi aliwataka viongozi waliotengana na ODM kurejea na kusaidia jamii hiyo kujenga umoja. Waziri wa Fedha John Mbadi alisema jamii ya Waluo lazima ibaki na umoja kwani ndiyo msingi mkuu wa chama cha ODM. “Wale wanaomdharau Oburu wanadhoofisha ODM. Ni lazima tuwe na mwelekeo mmoja wa kisiasa,” alisema Bw Mbadi. Mbunge wa Ruaraka TJ Kajwang’ alisema viongozi wa ODM wako tayari kuonyesha nguvu zao katika mkutano huo wa Kisumu. “Tunaelekea Kisumu Mei 31 na tutajua walio upande wetu na wale wasiokuwa nasi,” alisema Bw Kajwang’.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.