skipToContent
🌐All policy

ODM kuelekea Afrika Kusini na Ghana kujifunza uteuzi wa wagombea kuimarisha demokrasia ya ndani

ODM kuelekea Afrika Kusini na Ghana kujifunza uteuzi wa wagombea kuimarisha demokrasia ya ndani
VIONGOZI wa Kamati ya Uchaguzi ya chama cha ODM wanajiandaa kusafiri Afrika Kusini kujifunza jinsi chama tawala cha African National Congress (ANC) kinavyoendesha uteuzi wa wagombea wake. Ujumbe mwingine wa chama hicho pia unatarajiwa kuelekea Ghana kwa lengo kama hilo huku ODM ikijaribu kukabiliana na changamoto za uteuzi zilizokikumba katika chaguzi zilizopita. Chama hicho kimechagua nchi hizo mbili kutokana na mifumo yao imara ya kidemokrasia. ANC imeendelea kuwa moja ya vyama vya kisiasa vilivyo na ushawishi mkubwa barani Afrika tangu kuingia mamlakani mwaka 1994 baada ya kumalizika kwa ubaguzi wa rangi. Ghana nayo imejijengea sifa ya kuwa na uchaguzi wa mara kwa mara ulio huru na wa amani. Mwenyekiti wa Kitaifa wa ODM, Bi Gladys Wanga, alisema lengo ni kujifunza mbinu zitakazosaidia chama hicho kuendesha uteuzi wa haki na unaoaminika kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. “Kamati yetu ya Kitaifa ya Uchaguzi na Uratibu inachunguza mifumo mbalimbali, ukiwemo wa ANC. Tunataka kuboresha taratibu zetu na kuwapa wanachama imani kuwa uteuzi utakuwa wa haki na uwazi,” alisema Bi Wanga. Wakati huo huo, ODM imeanzisha mikutano ya mashinani katika maeneo mbalimbali nchini ili kufufua mitandao yake ya kisiasa na kuimarisha ushawishi wake kabla ya uchaguzi mkuu. Baada ya mkutano mkubwa uliofanyika Kisumu, chama hicho kinapanga kufanya mikutano mingine katika maeneo ya Magharibi, Turkana na Narok. Kiongozi wa chama hicho, Dkt Oburu Oginga, pia ameongeza juhudi za kuwaunganisha wanachama na viongozi wa zamani wa ODM. Hivi majuzi alikutana na Katibu Mkuu wa kwanza wa chama hicho na Gavana wa Kisumu, Profesa Anyang’ Nyong’o. Katika kikao cha hivi majuzi kilichofanyika Mombasa, ODM iliagiza kamati yake ya uchaguzi kuweka mifumo madhubuti ya kuhakikisha uteuzi wa wagombea unakuwa huru, wa haki na unaoaminika. Chama hicho pia kimetangaza kuwa hakitatoa tiketi za moja kwa moja kwa wagombea kama ilivyofanyika katika baadhi ya maeneo katika uchaguzi uliopita. Hatua hiyo inafuatia ripoti ya ukaguzi wa ndani ya chama mwaka 2023, iliyobaini kuwa mfumo wa kidijitali uliotumika katika uteuzi wa mwaka 2022, ulivurugwa na kusababisha baadhi ya wagombea kunufaika kwa njia isiyo halali.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.