“MJADALA kuhusu kizazi kipya cha viongozi nchini Kenya unaendelea kushika kasi huku baadhi ya wanasiasa vijana wakitaka mwisho wa siasa zinazotawaliwa na vigogo wa enzi za Kanu. Naibu kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens (DCP), Cleophas Malala, ni mmoja wa viongozi walioibua mjadala huo baada ya kusema kuwa uchaguzi wa 2027 unapaswa kuwa wa mwisho kwa viongozi waliokuwa katika mfumo wa Kanu kuendelea kushikilia mamlaka. Akizungumza katika mahojiano ya redio Ijumaa, Malala alisema Kenya inahitaji mageuzi ya kizazi katika uongozi, ingawa alisisitiza mabadiliko hayo hayawezi kufanyika ghafla. “Ni wakati wa mabadiliko ya kizazi, lakini hayawezi kufanywa kwa haraka. Lazima kuwe na kipindi cha mpito,” alihoji Malala. Kwa mujibu wake, ifikapo mwaka 2032 viongozi wote waliokuwa katika siasa za enzi za Kanu wanapaswa kuwa wameondoka jukwaani ili kutoa nafasi kwa kizazi kipya. Malala alionyesha kutoridhishwa na viongozi wanaotaka kuendelea kupiga siasa licha ya kuhudumu serikalini kwa miongo kadhaa. Alitoa mfano wa Rais William Ruto ambaye amekuwa katika siasa tangu 1992, na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye alikuwa waziri mwaka 1986 wakati yeye - Malala - akiwa mtoto mdogo. “Ni jambo la kusikitisha kuona kizazi hiki hakitaki kuachia wengine nafasi,” alisema. Kauli ya Malala inaonyesha jinsi vijana wengi nchini wanaanza kuchoshwa na siasa zinazozunguka majina yale yale miaka nenda rudi huku matatizo ya wananchi yakiongezeka. Mbunge wa Saboti Caleb Amisi pia amekuwa akihimiza kikomo cha siasa za “mabwanyenye wa kisiasa” wanaotegemea ukabila na historia zao za zamani kushinda uchaguzi. Kwa mujibu wa Amisi, wapigakura wa sasa wameelimika zaidi na hawatoshawishiwa na siasa za kikabila. Naibu kiongozi wa chama cha Safina, Willis Otieno, naye amesema Kenya haiwezi kusonga mbele bila kuondoa siasa za kizazi cha zamani. Lakini licha ya msukumo huo wa damu mpya, baadhi ya viongozi wa kizazi cha zamani bado wanaonekana kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za sasa za taifa. Katibu Mkuu wa Azimio na Mbunge wa Suba Kusini, Caroli Omondi, asema muungano huo unaopangwa upya utakuwa daraja la kuunganisha kizazi cha zamani na kile kipya katika uchaguzi wa 2027. Kwa mujibu wake tiketi ya urais inaweza kuwa matokeo ya maelewano kati ya viongozi wakongwe na vijana wanaoinukia kisiasa. Miongoni mwa wanasiasa wa kizazi kipya wanaotajwa ni Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna ambaye ameendelea kupata umaarufu mkubwa hasa miongoni mwa vijana wa Gen-Z. Sifuna amekuwa mmoja wa viongozi wanaojitokeza waziwazi kuikosoa serikali na kutetea masuala ya vijana, jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa ushawishi wake kisiasa. Ingawa vijana wanaonekana kushinikiza mabadiliko, wachambuzi wa siasa wanaamini bado kuna haja ya ushirikiano kati ya viongozi wakongwe na kizazi kipya, ili kuhakikisha mabadiliko ya kisiasa yanafanyika kwa utaratibu. Viongozi kama Gavana James Orengo wa Siaya wanaendelea kuonekana kama walimu wa kisiasa kwa vijana wengi wanaoinukia katika siasa za upinzani kutokana na historia yake katika mapambano ya demokrasia. Hata hivyo, ujumbe unaoendelea kujitokeza kuelekea uchaguzi wa 2027 ni kwamba Wakenya wengi, hasa vijana, wanataka viongozi wanaoweza kuelewa changamoto za kizazi cha sasa badala ya kutegemea historia za kisiasa za zamani. Msimamo wake kuhusu ushirikiano kati ya chama tawala United Democratic Alliance (UDA) na kile cha Orange Democratic Movement (ODM) - katika Serikali Jumuishi - ulimfanya aonekane kama muasi ndani ya ODM, hatua iliyochangia kuibuka kwa vuguvugu la Linda Mwananchi ambalo sasa limekuwa sauti muhimu ya upinzani.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
