skipToContent
🌐All

Orengo: Niko tayari kupambana na Ruto 2027

Orengo: Niko tayari kupambana na Ruto 2027
GAVANA wa Siaya James Orengo jana alitangaza azma yake ya kugombea urais mwaka 2027, hatua inayoashiria mwanzo wa kile ambacho wachanganuzi wanasema ni mkakati mkali dhidi ya Rais William Ruto kutetea kiti chake. Tangazo hilo limejiri baada ya wiki kadhaa za mashauriano ya kina na mikutano ya kisiasa katika maeneo ya Nairobi, Magharibi mwa Kenya na Nyanza ambako kumekuwa na shinikizo kutoka kwa wafuasi wake wakimtaka aingie siasa za kitaifa. Kilichoanza kama mikutano ya kawaida ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) sasa kimegeuka kuwa kampeni kamili ya kumweka Orengo kama sura ya upinzani kuelekea uchaguzi wa 2027. Orengo, akifanya kazi kwa karibu na kundi la “Linda Mwananchi” ndani ya ODM pamoja na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, amekuwa akisisitiza kuwa chama hicho hakikosi viongozi wenye uwezo wa kuwania urais. Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanasema hatua yake si tu kuhusu Ikulu, bali pia ni mkakati wa kujijenga kama kinara wa kisiasa wa jamii ya Waluo, huku akijipanga kwa mazungumzo na miungano ya kisiasa ijayo. Akizungumza katika mikutano ya kisiasa Muhoroni na Nyakach, Kaunti ya Kisumu, Orengo alisema jamii ya Waluo inapaswa kuwa na mgombea urais ili kujipatia nafasi imara ya mazungumzo katika siasa za kitaifa. “Sikuona jina la mtu kutoka jamii ya Waluo kwenye orodha ya wanaowania urais. Tunawezaje kujadiliana na vyama vingine bila kuwa na mgombea urais?” alisema. Alijitaja kama mrithi wa kisiasa wa marehemu Jaramogi Oginga Odinga na mtu anayeweza kumtoa jasho Rais Ruto uchaguzini. Alisema pia hawezi kushirikiana na serikali bila masharti kutokana na gharama ya juu ya maisha na changamoto nyingine zinazowakabili wananchi. Alitaja pia changamoto za kiuchumi kama kufungwa kwa viwanda vya sukari vya Miwani, Chemelil na Muhoroni, hali mbaya ya barabara na migogoro ya mara kwa mara eneo la Sondu kwenye mpaka wa Kisumu na Kericho. Aidha alisema mradi wa bwawa la Koru-Soin umesuasua, hali inayowafanya wakazi wa Nyakach kuendelea kukumbwa na mafuriko kila mwaka. “Kwa kuwa mifumo imefeli, ni lazima tuache kuwa watu wa kuombaomba kisiasa na badala yake tujitokeze kuwania urais kwa nguvu,” alisema Orengo. Aliongeza kuwa iwapo atapata nafasi, atahakikisha viwanda vya sukari vinarejeshwa chini ya umiliki wa umma badala ya kupewa wawekezaji binafsi. Gavana huyo pia aliwataka viongozi wanaotaka kuchaguliwa tena kujiunga naye au wakabiliane na hatari ya kushindwa 2027, akisema timu yake ndiyo yenye uwezo wa kuongoza nchi. Hata hivyo, hakufafanua kama atagombea kupitia ODM au chama kingine, lakini alisisitiza kuwa yeye ndiye kiongozi wa chama hicho. Hatua yake inajiri wakati ambapo mijadala ya ndani ya ODM kuhusu uongozi na mgombea urais wa 2027 inaendelea, huku vikao na makundi mbalimbali yakishinikiza mabadiliko. Iwapo atagombea rasmi, itakuwa mara ya pili kwa Orengo kuwania urais, baada ya jaribio lake la kwanza mwaka 2002 kupitia Social Democratic Party (SDP).
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.