skipToContent
🌐All

Padre John Pesa: Kiongozi wa kidini aliyeibua mijadala

Padre John Pesa: Kiongozi wa kidini aliyeibua mijadala
KWA miongo kadhaa, Padre John Pesa I alikuwa mmoja wa viongozi wa kidini waliovutia hisia kali zaidi katika eneo la Nyanza. Wapo waliomchukulia kama mtumishi wa Mungu mwenye uwezo wa kipekee wa kiroho, huku wengine wakimwona kama mhusika wa utata ambaye mara kwa mara alijikuta akipingana na wanaharakati wa haki za kibinadamu na mamlaka za serikali. Alikuwa mtu ambaye uwepo wake haukuweza kupuuzwa. Mara nyingi alionekana akizungukwa na kundi la wafuasi waaminifu, walinzi wa kibinafsi waliovalia suti nyeusi na maafisa wa polisi waliokuwa wakimlinda kana kwamba alikuwa kiongozi wa taifa. Alipopita mitaani au kuhubiri mbele ya waumini, kila macho yalielekezwa kwake. Hivyo basi, habari za kifo chake zilipoanza kusambaa Alhamisi asubuhi, majonzi makubwa yaliwakumba wafuasi wake. Katika Mochari ya Kwee ndani ya Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Jaramogi Oginga Odinga, huzuni ilitanda huku waumini wakikusanyika kwa makundi madogo, wakijaribu kukubaliana na ukweli kwamba kiongozi wao alikuwa ameaga dunia. Mwili wake uliripotiwa kufikishwa katika hospitali hiyo na viongozi wakuu wa kanisa baada ya kufariki. Awali ulipelekwa katika mochari kuu kabla ya kuhamishwa hadi Mochari ya Kwee. Kupitia kwa Mchungaji Kennedy Otieno, kanisa hilo lilikataa kutoa maelezo ya kina kuhusu kifo hicho, likisema taarifa rasmi ingetolewa baadaye kutokana na hadhi ya Padre Pesa ndani ya taasisi hiyo. Padre Pesa alijulikana zaidi kama mwanzilishi wa Kanisa la Holy Ghost Coptic Church of Africa lenye makao yake makuu eneo la Mamboleo, kando ya barabara ya Kisumu-Kakamega. Safari yake ilianza baada ya kutengwa na Kanisa Katoliki mwaka 1971. Tukio hilo lilimchochea kuanzisha dhehebu lake mwenyewe ambalo baadaye lilikua na kupata maelfu ya waumini katika maeneo mbalimbali ya nchi. Lakini pamoja na mafanikio hayo, jina lake liliendelea kuandamwa na utata. Mojawapo ya madai yaliyomletea ukosoaji mkubwa ni kwamba kanisa lake lilikuwa likiwahifadhi watu waliodaiwa kuwa na matatizo ya akili kwa lengo la kufanyiwa maombi ya uponyaji. Padre Pesa alisisitiza mara kwa mara kuwa watu waliokuwa wakifungwa minyororo katika kanisa lake walikuwa wale waliokuwa na tabia za vurugu na kwamba hatua hiyo ilikuwa ya kuwalinda wao wenyewe pamoja na watu waliowazunguka. Hata hivyo, wanaharakati wa haki za kibinadamu walihoji utaratibu huo. Ripoti moja ilidai kuwa baadhi ya wagonjwa walikuwa wakifungiwa katika mazingira yasiyoridhisha, kunyimwa huduma muhimu na kutengwa kwa muda mrefu. Mwaka 2023, alifikishwa mahakamani kwa madai ya kuwahifadhi watu 23 wenye matatizo ya akili katika mazingira yasiyofaa. Lakini baadaye alipata ushindi wa kisheria baada ya mahakama kutupilia mbali kesi iliyotaka kanisa lake libomolewe kutokana na madai hayo. Baada ya ushindi huo, Padre Pesa alieleza kuwa madai dhidi yake yalikuwa njama za kumchafua jina na alisisitiza kuwa hakuna mtu aliyekuwa akizuiliwa dhidi ya mapenzi yake na kwamba familia za waathiriwa zilikuwa zikitia saini fomu za idhini kabla ya kuwapeleka katika kanisa hilo. Mwaka huohuo, kamati maalumu iliyokuwa ikichunguza kuongezeka kwa makanisa yenye utata nchini ilitembelea kanisa lake. Wanachama wa kamati hiyo walieleza wasiwasi kuhusu hali ya makazi ya baadhi ya watu waliokuwa wakisubiri kuombewa. Kamati hiyo hata ilifananisha eneo hilo na “Shakahola ndogo” na kuwaokoa watu kadhaa waliokuwa humo. Mbali na masuala ya dini, Padre Pesa pia alihusishwa mara kwa mara na mijadala kuhusu ajali zilizokuwa zikitokea karibu na Mzunguko wa Coptic ulio karibu na kanisa lake. Baadhi ya wakazi waliamini kuwa misafara yake ya kidini ilihusishwa kwa njia fulani na ajali katika eneo hilo. Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa baadaye ulionyesha kuwa changamoto kubwa ilikuwa usanifu mbovu wa barabara. Hatimaye, Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu Kenya (KeNHA) ilitangaza mpango wa kuubadilisha mzunguko huo ili kupunguza ajali. Katika siasa, Padre Pesa alikuwa tofauti na viongozi wengi wa kidini kutoka Nyanza waliokuwa wakiegemea upande wa upinzani. Yeye alijulikana kwa kushirikiana na serikali iliyokuwa mamlakani bila kujali chama kilichokuwa madarakani. Katika ofisi yake kulining’inia picha zake akiwa pamoja na marais wote wa Kenya kuanzia Jomo Kenyatta, Daniel arap Moi, Mwai Kibaki, Uhuru Kenyatta hadi William Ruto. Alijulikana pia kwa ucheshi wake. Kauli yake maarufu zaidi iliyosambaa mitandaoni ni pale alipodai kuwa Mfalme Sulemani ndiye aliyemuua Goliathi badala ya Daudi, jambo lililozua vicheko na mjadala mkubwa. Kwa wanahabari waliomtembelea mara kwa mara, alikuwa na desturi ya kuwakaribisha kwa chupa ya soda ya mililita 500 na tabasamu pana usoni. Kwa Padre Pesa, umaarufu haukuwa mzigo. Habari zote zilizomhusu, iwe ni sifa au ukosoaji, zilikuwa zikibandikwa katika ubao wa matangazo ndani ya ofisi yake kama kumbukumbu za maisha yaliyojaa matukio.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.