skipToContent
🌐All

Polisi walenga kuzima mtandao wa wizi wa pikipiki mpakani

Polisi walenga kuzima mtandao wa wizi wa pikipiki mpakani
NOAH Simiyu alikuwa akitoka kazini Februari 17 akielekea nyumbani kwa kutumia pikipiki yake alipokutana na wanaume wawili na mwanamke mmoja waliomwashiria asimame katika eneo la Daraja Guywa, Kaunti ya Bungoma. Simiyu alisimama, mmoja kati ya wanaume hao akaomba usafiri, lakini Simiyu akakataa akieleza kuwa pikipiki hiyo haikuwa ya biashara ya kubeba abiria. Dakika chache baadaye kundi hilo liligeuka kuwa hatari. Mwanamke huyo pamoja na mmoja wa wanaume walitoa panga, wakamvuta Simiyu kutoka kwa pikipiki na kutorokea upande wa mpaka wa Uganda. Akiwa amejeruhiwa na kuvuja damu, Simiyu alitumia apu ya Mogo kuwasiliana na kikosi cha dharura cha uokoaji kabla ya kuripoti tukio hilo polisi. Kwa ushirikiano na maafisa wa polisi, timu hiyo ilifuatilia pikipiki hiyo na kuipata ikiwa imefichwa kichakani eneo la Lwakhakha karibu na mpaka wa Kenya na Uganda chini ya saa mbili baadaye. Wachunguzi walibaini kuwa wezi hao walikuwa tayari wameondoa vifaa viwili vya kuifuatilia na kubadilisha betri ya pikipiki, ishara kwamba walikuwa na ujuzi wa kuzima mifumo ya ufuatiliaji kabla ya kuisafirisha kuvuka mpaka. Kisa hiki kilizua hofu miongoni mwa maafisa wa usalama kwamba pikipiki nyingi zinazoibwa husafirishwa haraka kupitia njia zisizo rasmi kabla hazijafuatiliwa. Katika tukio jingine Januari 26, pikipiki iliyoibwa Nandi Hills ilipatikana Kisumu saa chache kabla ya wachunguzi kuamini kuwa ingesafirishwa kuelekea Uganda. Pikipiki hiyo ilikuwa ya John Bitok ambaye alikuwa ameikodisha kwa mhudumu wa bodaboda. Majira ya saa nane usiku, wezi waliingia katika nyumba ya kukodisha aliyokuwa akiishi dereva huyo na kuvunja kufuli kabla ya kutoroka na pikipiki hiyo. Kwa bahati nzuri kifaa cha ufuatiliaji kilikuwa bado kinafanya kazi. Bitok aliwasiliana haraka na kikosi cha dharura cha Mogo na kuripoti wizi huo katika kituo cha polisi cha Nandi Hills. Pamoja na polisi, timu ya uokoaji ilifuatilia pikipiki hiyo hadi eneo la kuosha magari mjini Kisumu kufikia saa moja asubuhi iliyofuata. Wachunguzi wanaamini pikipiki hiyo ilikuwa ikisubiri kusafirishwa kupitia Busia kuelekea Uganda kabla ya operesheni hiyo kuvurugwa. Mashirika ya usalama sasa yanasema wizi huo unafanywa na mitandao ya uhalifu iliyopangwa ambapo kundi moja huiba pikipiki, jingine husafirisha na wengine husimamia uuzaji. Tatizo hilo pia limeenea Kaskazini mwa Kenya ambapo pikipiki zinazoibwa kutoka maeneo mbalimbali husafirishwa hadi kaunti za mpakani kabla ya kutoweka katika mataifa jirani. Kwa maelfu ya wahudumu wa bodaboda nchini Kenya, pikipiki ni zaidi ya chombo cha usafiri. Ni chanzo cha riziki na mali pekee inayotenganisha familia nyingi na umaskini. Lakini ongezeko la wizi wa kutumia nguvu sasa limefichua shughuli za magenge yaliyopangwa yanayosafirisha pikipiki zilizoibwa kwenda nchi jirani ambapo huuzwa, kuvunjwa kupata vipuri au kupewa usajili mpya. Maafisa wa usalama Kenya na Uganda wanaamini uhalifu huo si matukio ya kawaida tena bali biashara kubwa ya kimataifa inayohusisha maeneo ya magharibi mwa Kenya hadi mipaka ya Ethiopia.
Share
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Read full article

Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.