“KIONGOZI wa familia ya marehemu Raila Odinga, Raila Junior, jana aliwataka baadhi ya wanasiasa wa ODM kuheshimu familia hiyo. Kumekuwa na vuta nikuvute kati ya Waziri wa Fedha John Mbadi na familia ya Raila kutokana na matamshi ambayo waziri alitoa Mei 4 katika warsha ya ODM jijini Mombasa. Matamshi ya Mbadi yalifasiriwa na baadhi ya watu kama ya kumdhalilisha marehemu Raila, na yameshuhudia majibizano makali kati yake na mjane Ida Odinga, Mbunge wa EALA Winnie Odinga na Mbunge Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Kisumu Ruth Odinga. Akiongea katika uwanja wa Jacaranda, Nairobi, jana alipokutana na wakazi wa eneo hilo, Junior alifichua kuwa alifanya kikao na kinara wa sasa wa ODM, Dkt Oburu Oginga, ambapo alihimiza kuchukuliwe hatua kali dhidi ya viongozi wanaomkosea heshima marehemu babake. “Kuna matamshi mengi hasi yanatolewa dhidi ya familia. Tunachoomba viongozi ni wawe wavumilivu, na kuonyesha heshima wanapotaja familia yetu na namna wanavyoizungumzia,” akasema Junior. Alieleza kwamba alikuwa amekimya na kujiepusha na siasa tangu mauti ya babake, ila sasa itabidi ajitokeze kupambana na wanaoshambulia familia hiyo na kuidhalilisha. Kuhusu uongozi ndani ya ODM, Junior alisema wanamheshimu Dkt Oginga kama kinara wa chama hicho lakini pia wanataka kama familia washirikishwe katika masuala yanayohusu chama hicho. “Kama familia ya Raila tunataka kuwa na usemi kuhusu yanayoendelea ndani ya ODM. Kama mwanawe Raila nahisi vibaya jinsi watu wanazungumza hapa nje na mkondo ambao mambo yanachukua. “Tafadhali koma kuzungumzia familia ya baba, uwe waziri au katibu. Hii tabia lazima ikome,” akahoji. Junior alidokeza kuwa ana maelezo kuhusu jinsi marehemu babake alitaka familia hiyo iongozwe kwa sababu alikuwa akiandamana naye kwenye mikutano mingi kabla ya mauti yake. Alikataa kuzungumza iwapo wanaegemea mrengo wa Linda Mwananchi au Linda Ground, akisema yeye si mwanasiasa na wanafuata mwelekeo wa dada yake, Winnie. Hata hivyo, alisema babake hafai kushambuliwa mautini ilhali baadhi ya viongozi ambao wanafanya hivyo ndiyo walikuwa wakinufaka kutokana na uongozi wake na hata aliwakuza na kuwalea kisiasa. Mnamo Jumamosi, Mbadi alimkabili Winnie vikali akimtaka awanie kiti cha kisiasa kisha achaguliwe ndipo amzungumzie kuhusu masuala ya kiuchumi katika wizara ya fedha.
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
