“Rais William Ruto ameelekeza Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama (NTSA) kusitisha marufuku yake na mpango uliokuwa umeandaliwa wa kukabiliana na matatu zilizo michoro ya graffiti, mapambo ya kisanii na vioo vyeusi. Akizungumza katika Ikulu ya Mombasa, kufuatia mazungumzo na wadau wa sekta ya usafiri wa umma, Rais Ruto aliitaka NTSA kusitisha mipango hiyo ambayo ilikuwa tayari imeidhinishwa na Mahakama Kuu. Maagizo hayo yanatoa afueni kwa wamiliki wa magari ya usafiri wa umma (PSV) na wasanii baada ya kipindi cha mvutano mkali wa kisheria kuhusu utamaduni maarufu wa “nganya” nchini Kenya. “Nimeelekeza NTSA kuweka mazingira yanayowaruhusu wamiliki wa matatu kuendelea kutumia michoro ya kisanii na graffiti kwenye magari yao kwa njia inayozingatia usalama na heshima kwa watumiaji wengine wa barabara,” Ruto alisema. Mnamo Mei 2025, NTSA ilitoa agizo kwa magari ya usafiri wa umma kuondoa graffiti, mapambo ya nje na vioo vyeusi vilivyowekwa baada ya utengenezaji wa awali, hatua iliyozua mvutano wa mwaka mzima kuhusu utamaduni wa kipekee wa matatu nchini. Mamlaka hiyo, chini ya Mkurugenzi Mkuu George Njao, ilisema wamiliki wa matatu ambao watashindwa kutii wangekabiliwa na adhabu ikiwemo kukamatwa kwa magari, kusimamishwa kwa leseni za kuhudumu na kufutwa kwa uwezo wa kutumia mfumo wa huduma za taasisi hiyo. NTSA ilitetea agizo hilo kwa misingi ya usalama, ikisema kuwa michoro mingi ya nje na vioo vyeusi hupunguza uwezo wa madereva kuona barabara na pia huzuia polisi kufuatilia kinachoendelea ndani ya magari. Pia ilisema mapambo hayo huficha alama muhimu za utambulisho kama majina ya SACCO zilizosajiliwa, njia zilizopangiwa kila sacco na mstari wa manjano wa udhibiti unaotambulisha magari ya usafiri wa umma. Wamiliki wa matatu walipinga agizo hilo katika Mahakama ya Milimani jijini Nairobi, wakidai kuwa marufuku hiyo inakiuka haki ya kikatiba ya uhuru wa kujieleza kiutamaduni na kisanii. Kupitia mawakili wao, pia walidai kuwa mamlaka ilitoa agizo hilo bila ushahidi unaoonyesha uhusiano kati ya michoro ya magari na ajali za barabarani. Mnamo Aprili 29 2026, Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye alitupilia mbali ombi hilo, hatua iliyokuwa pigo kwa sekta hiyo inayowapa ajira mamia ya vijana wa Kenya. Alisema agizo hilo lilikuwa la kisheria na la kikatiba, na kwamba usalama wa umma una uzito zaidi kuliko uhuru wa kisanii. Mahakama pia ilipata kuwa mamlaka ilifuata taratibu sahihi za kisheria, na hivyo kufungua njia ya msako wa kitaifa wa magari ya usafiri wa umma yenye mapambo. Katika hotuba yake, Rais Ruto alionyesha kutoridhishwa na agizo hilo la NTSA, akisema: “Wamiliki wa matatu wamenieleza kuwa wameambiwa waondoe graffiti, na ninajiuliza, kwa nini?”
Original story
Continue reading at Taifa Leo (Swahili)
taifaleo.nation.co.ke
Summary generated from the RSS feed of Taifa Leo (Swahili). All article rights belong to the original publisher. Click through to read the full piece on taifaleo.nation.co.ke.
